Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Agosti 25, 2020

Jumanne, Agosti 25, 2020,
Juma la 21 la Mwaka wa Kanisa


2Thes 2:1-3, 14-17;
Zab 95:10-13;
Mt 23:23-26


UHURU KWAKUACHANA NA UNAFIKI!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana litaanza kwa kuiangalia Injiili ambapo basi tunakutana na Yesu akitoa onyo kali sana na karipio kubwa sana kwa Wafarisayo. Anawalaumu kwa kuyaacha mambo ya msingi-haki, huruma na imani na kukazania yale yasiyo ya msingi, yale wanayojua ya kwamba watapata sifa tu.

Wengi kati ya Wafarisayo walithamini sifa toka kwa mwanadamu kuliko toka kwa Mungu. Hivyo waliweza kufaulu kuwapumbaza baadhi ya wanadamu kwamba ni wema lakini basi baadhi ya matendo yao waliyoyafanya kisirisiri yalikuwa ni mabaya sana na hiki kingaliwakosesha ufalme wa mbinguni. Ndio maana wanaambiwa kwamba wanachuja mbu na kumeza ngamia au kwamba wanaosha nje ya kikombe kumbe ndani kimejaa uchafu mwingi.

Ndugu zangu, somo hili basi linatuhusu sana hasa sisi tunaopendelea mambo ya dini, kuja kanisani, kutoa zaka, kwenda jumuiya, kutoa misaada kwa watoto yatima-tunaambiwa kwamba matendo haya ya nje yaambatane na kilichondani ya moyo wetu na kile tunachokifanya sirini. Tunavyoonekana mbele za watu tukiwa tunakwenda kutoa ile misaada au zaka zetu basi tuwe hivyo hivyo na tunapokuwa sirini. Macho ya watu yasitufanye tuishi maisha ya ndumbila kuwili. Tutajipotezea mbingu hivihivi.

Alichowalaumu nacho Wafarisayo, bado kinaendelea hadi leo. Mfano: kila mmoja leo akichunguza maisha yake yalivyo anapokuwa sehemu ya kificho, wakati asipoonekana na umati kweli tutagundua kwamba wakati huu ndio wakati tunapotenda dhambi nyingi sana. Wengi tunaogopa kutenda dhambi kwa sababu ya macho ya watu lakini tukiwa wenyewe, tunatenda matendo ya ajabu. Hapa ni lazima tufanye kitu-tukishajiona kwamba tupo mazingira ya 'private'-labda tunapata vinywaji sehemu za 'private', tusipoonekana na watu au kujulikana na watu, ukishakuwa sehemu ya kificho tu-basi tuanze kumwomba Mungu Zaidi tukijua kwamba hapa shetani yupo karibu zaidi kwani sehemu za namna hii ndipo tunapowehuka na kufikiri kwamba watu hawatuoni, basi na Mungu hatuoni na tutende uovu wowote.

Pia tujifunze umuhimu wa jumuiya. Jumuiya ina mchango mkubwa sana wa kutufinyanga ili tusidumbukie kwenye dhambi. Uwepo wao basi hutufanya tuendane na maadili fulani. Kila mmoja athamini mchango unaopatikana kwa kuishi maisha ya jumuiya. Zaidi ni kutambua kwamba Mungu anaona kila mahali na kila kitu. Hivyo tusibakie kwenye kuogopa macho ya mwanadamu Zaidi kuliko ya Mungu. wengi tunatenda dhambi kwa sababu tunayaogopa macho ya wanadamu zaidi kuliko ya Mungu. Hivyo tuache kujitafutia umaarufu machoni pa watu-kama ni kusaidia tusaidie sehemu zote na sio tu sehemu zile tunapoonekana na watu na pia tuwasaidie watu wa aina zote na sio tu kwenda pale ambapo tunajipatia umaarufu.

Kwenye somo la kwanza tunakutana na mtume Paulo akizungumza na wakristo wa Thesalonike hasa wale waliotegemea ujio wa pili kwa haraka na kuacha kutenda kazi na kuanza kuwaogopesha wengine. Yeye anawaambia kwamba ujio wa Bwana utakuja siku na wakati alioupanga Bwana mwenyewe; wao haina haja ya kuogopa ila waendelee kuishi kuendana na zile taratibu za Kikristo walizofundishwa, wasihangaishwe na aina yoyote ya mafundisho bali waishi tu kawaida, wabakie kwenye walichofundishwa na hapa wataweza kuupokea ujio huu. Sisi ndugu zangu tubakie kuishi kile tulichofundishwa siku zote na imani yetu. Hiki kitatuokoa.

Maoni


Ingia utoe maoni