Jumamosi, Agosti 22, 2020
Jumamosi, Agosti 22, 2018,
Juma la 20 la Mwaka
Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia
Is 9: 2-7;
Zab 113: 1-8;
Lk 1: 26-38;
SALAMU, MALKIA !
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa Takatifu asubuhi ya leo ikiwa basi tunaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia. Hii ni kumbukumbu iliyoanzishwa mwaka 1954, miaka minne tangu Papa huyu huyu atangaze Dogma ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni na Pia ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka mia moja tangu Papa Pio wa wa tisa atangaze dogma ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili hapo mwaka 1854.
Mwaka huu wa 1954 ilikuwa pia ni mwaka wa kwanza kwa ajili ya kumheshimu Mama Maria kuwahi kuwekwa na kanisa yaani “Mwaka kwa heshima ya Mama Bikira Maria.” Maria anapewa hadhi ya Malkia na mama yetu. Malkia ni mama Mtawala, mwenye uwezo na madaraka. Mama Maria basi kwa kitendo chake tu cha kuwa Mama wa Yesu, basi moja kwa moja alikabidhiwa madaraka ya kuwa Malkia huko mbinguni, Mama wa enzi ya kifalme aliyepewa madaraka hayo na mwanae. Ndiyo basi tunakuwa na kila sababu ya kwenda kwake kuomba msaada kwani yeye ni Malkia, mama mwenye madaraka.
Maria pia ni mama yetu kwani basi yeye alikabidhiwa kanisa alitunze na aliombee kama Mama. Sisi sote ni viungo vya kanisa kwa ubatizo wetu. Hivyo basi kwa pamoja tumkimbilie Mama huyu. Yesu aliamua kumpatia nafasi na nguvu za kipekee kabisa. Nguvu hizi hakuzipata kutoka kwake yeye kama yeye. Hata kati ya wanadamu wapo waliobarikiwa na kupatiwa uwezo wa kipekee kabisa-kuna wanaoweza kukaa chini na kubuni dawa za ajabu, kubuni ndege, kubuni vifaa vya kwenda anga za mbali na hata kubuni majengo na barabara za ajabu. Wapo waliojaliwa vipaji hivi-na wengine hawana. Mama Maria alijaliwa uwezo na mamlaka ya kimalkia na Yesu. Sisi basi twende kwake tukiomba kila siku kupitia kwake kama injili inavyofundisha.
Katika masomo yetu, somo la kwanza tunakutana basi na lile somo tunalosomaga kwenye ile vijilia ya Noeli. Ni somo lenye maneno kama “wale waliokwenda kwenye giza la mauti mwanga umewaangaza, na maneno mengine ni kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, mtoto mwenye enzi ya kifalme.” Huu ni unabii wa isaya uliotokana na yale mazingira ya mateso ya kipindi hicho. Kipindi hiki kulikuwa na ukandamizaji; mateka na wafungwa hasa wale wa kisiasa walionekana kuwa tishio na wenye uwezo kiakili wa wakati huo waliteswa kwenye jela za mateso za kwenye handaki, zenye giza kabisa. Huko walifungwa ili wawe wajinga na wasijue ukweli wa kinachotendeka tena ili basi wasije wakaleta mapinduzi au kuwafundisha watu ukweli. Ukitaka kujua ukweli wa matukio haya, basi soma maandiko ya mwanafalsafa aitwaye Plato hasa kuhusu ule mfano wake au "allegory of the cave."
Lakini basi nabii anatangaza enzi ya matumaini kwa mtoto atakayezaliwa na atakayeleta mwanga, mwenye enzi ya kifalme na kuleta heri zaidi.
Yesu ndiye aliyetangaza ujio wa enzi hizi, sisi sote tulikuwa basi tupo gizani kama wale wafungwa na Yesu ndiye aliyetuletea mwanga. Ameitangazia dunia Amani na upendo, hadi leo basi tunu zinazotamaniwa kila mahali ni upendo, kupokeleana, na kusameheana na kupatana. Hizi zilitangazwa na Yesu.
Huyu Yesu basi alizaliwa na mama Maria ambaye basi Yesu mwenyewe aliamua kumpatia mamlaka kwa kitendo cha yeye kuwa mama yake.
Sote basi leo tumfanye Maria kuwa Malkia yetu. tukimbilie ulinzi wake, twende kwake tuombe msaada. Tuanze siku yetu na Mama Bikira Maria. Yeye kwetu ni Malkia, Amina!
Maoni
Ingia utoe maoni