Alhamisi, Agosti 20, 2020
Alhamisi, Agosti 20, 2020,
Juma la 20 la Mwaka wa Kanisa
KUMBUKUMBU YA MT. BERNARDO (Abate)
Ez 36:23-28;
Zab 50:12-15, 18-19;
Mt 22:1-14
SHEREHE YA HARUSI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu Asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na ile zaburi ya kuomba msamaha aliyoitumia Daudi baada ya kumtendea Mungu dhambi kubwa. Kwa njia ya Zaburi hii basi aliweza kujinyenyekesha na kutumia maneno haya kuomba msamaha na Mungu alimsamehe. Ni jukumu letu basi tutumie vyema haya maneno yaliyoandikwa na Daudi, nasi tuombe msamaha kama yeye ili nasi tujaliwe neema na tuepuke kuteswa na madhambi yetu yanayotuongezea shida kila siku na kutunyima neema.
Lakini leo zaburi hii inasisitizia kile ambacho taifa la Israeli lingalipaswa kufanya leo kwenye somo la kwanza. Wao walimkosea sana Mungu kwa matendo yao maovu. Wangalipaswa kuomba msamaha kama Daudi ili Mungu awasafishe maovu yao. Lakini kwenye somo la kwanza, tunagundua kwamba kweli hawakuomba msamaha. Mungu mwenyewe aliamua basi kuanza kuwapatia moyo mpya na kuwatoa kwenye utumwa na si kwamba alifanya hivyo kwa kuwa wao waliomba msamaha bali kwa kuwa yeye alitaka kuhifadhi utakatifu na Umungu wake mtakatifu-kwamba taifa la Israel ni mali yake takatifu na labidi liheshimiwe.
Ajabu ni kwamba yawezekana kwamba hata baada ya Mungu kuonesha juhudi hii ya kutaka kuwatakasa, kuna baadhi waliokataa kuupokea mwaliko huu na kumchukiza Mungu Zaidi na kusema hatutaki huo moyo wako mpya utuwekee au hatutaki utusafishe. Acha tubaki kwenye uchafu wetu. Hili linafanana moja kwa moja na kile tukionacho katika injili ya leo.
Mfalme ameandaa karambu lakini walioalikwa wanaikataa na kuikimbia na ndivyo kweli itakavyokuwa kwenye mwisho wa dunia. Watu wataalikwa lakini watakimbilia kwenye mambo yao na mwishowe kuanguka.
Hili linafanana na kinachoendelea kutendeka kila siku tuhudhuriapo kanisani. Yesu anatualika kwenye karamu ya Ekaristi lakini ni wachache tuonao umuhimu wa hili wa kukubali kuingia kwenye mwaliko huu. Au kwenye sakramenti ya kitubio. Anaita ili tusafishwe lakini ni wachache tunaokubali. Sisi tuwe watu wa kukubali mwaliko huu mtakatifu wa Yesu. Tusipuuzie, hasa kwenye sakramenti zake. Wengi wetu tumezidisha kupuuzia na ndio maana tumeishia kwenye kuanguka na kushindwa kuona neema za Mwenyezi Mungu. tuache kupuuzia. Pale tuliposhindwa kupokea sakramenti zake vyema, tuombe Mungu msamaha kwa dhambi zetu kama Daudi anavyosisitiza leo kwenye zaburi.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni