Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Agosti 17, 2020

Jumatatu, Agosti 17, 2020.
Juma la 20 la Mwaka


Ez 24: 15-24
Lumb 32:18-21;
Mt 19: 16-22

TUNAITWA KUWA MASKINI WA ROHO

Karibuni sana ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi katika neno la Bwana tunaanza kwa kuingalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na mzaburi akituambia kwamba umemsahau Bwana Mungu wako aliyekuumba na kuupatia utukufu miungu mingine.

Zaburi hii ndugu zangu inatumika kusisitiza ujumbe wa somo la kwanza leo ambapo basi tunakutana na nabii Ezekiel akiendelea kutoa unabii wa adhabu itakayowapata watu wa taifa la Israeli. Anasema kwamba adhabu hii itakuwa ni ngumu na chungu; uchungu wa zaidi hata ya ule wa kufiwa na mpendwa wako wa karibu-sasa itakuwa ni zaidi. Leo Ezekiel anaoneshwa ishara ya kifo cha mkewe, na anapatwa na uchungu lakini anaambiwa asiomboleze lengo likiwa ni kuwafundisha wale wana wa Yuda kwamba nao watakumbana na matendo kama haya; yaani watakao kufa siku hiyo ya adhabu itakayokuja watakuwa ni wengi na watakuwa katika mikiki mikiki kiasi kwamba watakosa hata muda wa kuomboleza na kulia.

Sisi ndugu zangu lazima tunaalikwa kutambua matendo yote yanayotufanya tumsahau Bwana Mungu wetu. Kila mmoja wetu anapaswa kuangalia ni nini kinachomfanya basi Mungu ahasaulike ndani ya moyo wake ashindwe kutembea naye, kila siku, labda wakati wa kusali nishindwe kutumia ule muda vizuri, ni kipi ninachokifikiria au ni matendo gani niyatendayo nishindwe kutulia na kumpatia Mungu sifa, nikose utulivu wa ndani.

Dhambi ndiyo yenye kutufanya tushindwe kutulia kila wakati. Hutufanya tuweweseke na kuona aibu hata ya kuongea ukweli au hata ya kuweza kusimama mbele za Mungu na kumweleza shida zetu au hata kumuonya mtu. Inatukosesha nguvu na ujasiri wa kuongea. Tuombe kwa maombezi ya mtakatifu Bernad kuacha dhambi.

Kwenye somo la Injili ya leo tunakutana na kijana mmoja aliyekuwa na mali nyingi lakini basi anakataa kuwa mkamilifu kwa kushindwa kuuza mali yake. Yeye basi alikataa kuachilia mali aliyokuwa nayo ili kuwa mkamilifu; hakuwa tayari kujitoa sadaka. Maisha ya kumfuata Yesu ni kujitoa sadaka na sadaka lazima ikuuume kama ilivyomuuma huyu kijana.

Hapa najaribu kufananisha mawazo ya kijana na baadhi yetu tunavyofikiri kwamba tutaanza kuwa watu wema tufikapo uzeeni; tunasema bado muda, hatuko tayari kutoa sadaka kwa sasa tukijihurumia na kusema kwamba kwa kweli muda ni bado. Tuepukane na mawazo kama haya. Mtakatifu Augustino alikumbwa na mawazo kama haya sana mwanzoni lakin basi ilibidi ifike wakati akafanya maamuzi magumu na kuachana na maisha yake ya kipotofu na kuanza kumfuata Bwana. Sisi tutambue kwamba sasa ndio wakati wa kujitoa sadaka. Tuombe kupitia maombezi ya Mt. Bernad tuweze kuwa watu wenye kujitoa sadaka Zaidi na Zaidi. Tuumie zaidi pale tunapo poteza uhusiano wetu na Mungu na sio kwa kupoteza mali au vitu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni