Jumanne, Agosti 18, 2020
Jumanne, Agosti 18, 2020,
Juma la 20 la Mwaka Kanisa
Ez 28:1-10;
Kumb 32:26-28, 30, 35-36;
Mt 19:23- 30
KUACHA YOTE NA KUMFUATA KRISTO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na nabii Ezekiel juu ya mfalme wa Tiro. Huyu alikuwa mfalme maarufu, mwenye maarifa, uwezo mkubwa wa kuongea na kushawishi watu, kila alichoweza kupanga kilifanikiwa na aliweza kujizolea sifa na utajiri mkubwa sana machoni pa watu. Lakini cha ajabu ni kwamba alishindwa kuzimpatia Mwenyezi Mungu hizi sifa-alizielekeza sifa zote kwake na akaishia kujiita Mungu. Hivyo basi alijifanya Mungu na kunyanyasa wenzake kama apendavyo na kuwanyanyasa watu wa taifa la Yuda.
Basi siku ya leo Mungu anamtuma nabii Ezekieli kumwambia kwamba alijikweza mno, aliacha kumwelekezea Mwenyezi Mungu sifa hizo na kuishia kuchukua nafasi ya Mungu. Hivyo basi Mungu anaagiza mapigo makuu kwake. Anaapa kumwaibisha kwa kumwua kifo cha aibu ili atambue kwamba yeye sio Mungu.
Somo hili linatoa onyo kali hasa kwa baadhi yetu tuliowahi kupewa uwezo wa kiakili, maarifa, au uwezo wa kujieleza au hata uwezo wa kifedha. Ni lazima tutambue kwamba hivi ni vipaji vya Mungu na tuvitumie kwa ajili ya utukufu na sifa zake. Wengi kati ya wanasayansi na wanafalsafa wamepewa uwezo mkubwa darasani na kwenye ujuzi lakini basi wakaishia kujivuna, wakatumia ule uwezo kumtukana Mungu na kusema Mungu hayupo. Hii ni dhambi kubwa. Ni kama mtu aliyepewa kamkopo kadogo toka kwa tajiri mwenye uwezo halafu akaanza kutumia kale kamkopo kumtukana yule tajri. Hakika yule tajiri atakuja siku moja na kukummaliza.
Hivyo basi tutumie, uwezo wetu wa kuongea, ujuzi, na nguvu zetu kwenye kumsifu Bwana na si kusema kwamba Bwana hayupo.
Kwenye somo letu la Injili tunakutana na Yesu akisema namna ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia kwenye ufalme wa mbinguni. Hawa ni wale wenye uchu wa mali, wenye uroho wa kulimbikiza ili basi wawe na nguvu juu ya wengine-watawale wengine na watukuke juu yao kama miungu. Kweli hawa kuiridhi mbingu si rahisi kwani huishia kupambana na Mungu ili kupata madaraka ya kutawala wengine kama huyu mfalme wa Tiro.
Sisi tusiwe na uchu wa namna hii; hiki kitatukosesha mbingu kwani tunaishia kwenye kushindana na Mungu na kuwa na kiburi badala ya kunyenyekea mbele yake. Utajiri unaozungumziwa hapa ni ile hali ya kujiona kwamba una kila kitu na hivyo basi hakuna haja ya kumtumainia Mungu; unataka uwe huru bila kubughudhiwa na yeyote.
Sisi tusiwe watu wa nanmna hii ndugu zangu. Tujione kama maskini tunaohitaji huruma ya Mungu. ama kweli Mungu hatatuacha kamwe
Maoni
Ingia utoe maoni