Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Agosti 13, 2020

Alhamisi, Agosti 13 2020
Juma la 19 la Mwaka

Eze. 12:1 – 12
Zab 114: 1-6;
Mt 18: 21-19:1

MSAMAHA KATIKA MAISHA YA KIKRISTO!


Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanzia kwenye somo la kwanza ambapo tunakutana na nabii Ezekieli akijaribu kufanya tendo kuonesha kwamba wana wa Israeli watapelekwa utumwani. Anavaa kabisa kama mtu anayekwenda utumwani na kujivika mizigo yake watu wakiangalia. Lakini basi hakuna anayemsikiliza. Mungu anawaita kwa kutumia jina la watu waasi. Lakini yeye hakukata tamaa.

Kweli Ezekiel alikuwa na moyo wa ujasiri wa kufanya tendo kama hili bila ya yeye kuogopa basi. Na kweli manabii kama akina Yeremia-kuna vitu waliambiwa wafanye hadharani ambavyo kweli kama mtu hukuwa na roho wa Mungu ama kweli wasingalithubutu. Kwa baadhi yetu tungalifikiri kwamba vinatudhalilisha na kusema ati wee sifanya, lakini tutambue kwamba hii ndio njia Mungu alikuwa ametaka kutumia ili kutoa ujumbe. Hivyo ilipaswa ipokelewe na nabii.

Ndivyo ilivyo na kwetu ndugu zangu.Tunapaswa kuwa watu wenye utii kwa sauti ya Mungu. Matendo tunayoagizwa kufanya kwenye liturjia lazima tuyafuate. Tusiseme haya ni mambo mambo tu ya nje. Ukweli ni kwamba Mungu ana mpango na hayo matendo. Wengine tunaonaga mzigo kupiga magoti kanisani, au tukiambiwa tusimame tunaona mzigo au kwenye ile ijumaa kuu ile kupiga magoti na kusimama tunaona kama mchezo. Tusifanye hivi, lazima tuziheshimu alama hizi kama takatifu kabisa na tusione aibu kuzitenda. Tukumbuke kwamba akina Ezekiel waliamriwa kutekeleza matendo ya ajabu nao wakatii. Nasi tusiache kutii kutekeleza vitendo kama hivi.

Kwenye somo la Injili basi tunakutana na Yesu akisisitizia juu ya kusamehe kwamba yatubidi kusamehe saba mara sabini; kusamehe kila wakati. Huu ndugu zangu bado ni ujumbe mgumu au somo gumu kwetu sisi wakristo. Bado hili somo halijaingia mioyoni mwetu. Hii ni kwa sababu kweli wengi wetu hatujaweza kusamehe; tukitendewa kosa hatusamehi bali tunataka ati yule aliyetukosea, apewe na yeye adhabu yaani naye apate mateso, aumie na yeye, na ndipo tunaridhika. Wengi wetu tunaponywa na ile adhabu inayotolewa zaidi kuliko kutoa msamaha hivi hivi. Nakueleza, kama Mungu angekuwa na ufikiri kama wa kwetu, ama kweli sisi tusingalikuwa tumeweza kulipa adhabu zetu zote.

Sisi ndugu zangu tusingalikuwa na Msamaha wa Mungu; tungalikuwa na madeni makubwa ajabu au makovu makubuwa ajabu ndani ya miili yetu. Tuombe kuwa watu wenye kusamehe Zaidi na zaidi.
Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni