Ijumaa, Agosti 14, 2020
Ijumaa, Agosti 14, 2020,
Juma la 19 la mwaka wa Kanisa
Ez 16: 1-15, 60, 63;
Is 12: 2-6;
Mt 19: 3-12
NDOA-AGANO LA UPENDO!
Karibuni ndugu kwenye adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi Mungu kupitia kinywa cha nabii Ezekiel, anaamua kutoa matumaini kwa taifa la Israeli. Yeye anaanza kwa kumuonesha Israeli hali aliyokuwa nayo kabla, na jinsi alivyomuokota kwenye hali ya udogo. Lengo ni kutaka Israeli abadilike ndugu zangu kwa yeye kuikumbuka historia yake ya udogo.
Israeli alipofanikiwa, alijisahau kabisa, akashindwa kujua alikotoka, akawa anatumia hata rasilimali alizopewa na Mungu kumtukana Mungu. Huu ni mwaliko kwetu ndugu zangu.
Kila mmoja wetu akumbuke historia yake ya udogo na kumrudia Mungu. Angalia wewe unayetukana wenzako-ulianzia wapi? Hujui kwamba mwanzoni ulikuwa kama mtoto tu, ulizaliwa bila kitu, ulilishwa, ukabebwa na kaka, dada na mama, sasa majivuno yanatoka wapi sasa? Kwa kweli tubadilike ndugu zangu. Kuna tuliowahi kumtukana Mungu kwa kuwanyanyasa hawa wadogo zake tuwaonao kila siku huku duniani. Tusiishi hivi ndugu zangu.
Kwenye Injili yetu ya leo Yesu anazungumzia juu ya ndoa kwamba talaka ni mwiko, hakuna talaka. Na anasema kwamba kwenye ndoa lazima sote wanandoa tuwe mwili mmoja na roho moja. Hili sio jambo rahisi ndugu zangu. Kwa kweli hapa wengi bado tupo mbali. Hii ni kwa sababu wanandoa wengi sio mwili mmoja tena, talaka zinazidi kila siku. Tabia za kupepesa pepesa macho na kuiga kumewafanya wanandoa wengi kuwa na tamaa na kuishia kuvunja ndoa kila siku. Tuache tabia za kupepesa macho jamani. Tukipita njiani tusitazame na kutamani kila kitu.
Halafu tusipende kuiga wale wanamuziki na wasanii. Wengi wetu basi ndio tumewafanya kuwa model wetu. Mnaishi ndoa kwa kutumia maisha ya waigizaji wa filamu. Sisi tunaye Kristo aliyemwaminifu kwa kanisa lake kila wakati. Huyu ndiye wa kufuatwa katika suala lolote lihusulo mahusiano ndani ya ndoa zetu.
Lakini pia heshima ni muhimu sana kwani kuna hatari ya kuzoeana na kuanza kudharauliana, msamaha, mawasiliano na upendo wenyewe hulinda ndoa.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni