Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Agosti 11, 2020

Jumanne, Agosti 11, 2020,
Juma la 19 la Mwaka


Ez 2:8 -3:4;
Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131;
Mt 18: 1-5, 10, 12-14


NI NANI MKUBWA KATIKA UFALME WA MUNGU?

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Nabii Ezekiel akipewa kitabu ili akile. Hiki kitabu kilikuwa ni neno la Mungu kuhusu wale wana wa Israeli. Yeye basi ilimpasa alijue hili neno, alimumunye, na kuliacha liingie ndani ya moyo wake na kulijua lote.

Lakini basi kitabu hiki kilikuwa na uchungu wa ajabu ikimaanisha kwamba neno hili lilikuwa chungu ajabu kwani ujumbe wake ulikuwa ni mgumu na mzito kwa wale ambao wangeupokea. Ujumbe wake ulikuwa mzito sana hasa kwa wale wana wa Israeli kwani uliwahusu kwa kiasi kikubwa wao na hasa juu ya dhambi na uovu wao, na kweli ulibeba adhabu na maonyo makali na hivyo basi hata kwa Ezekiel, ujumbe huu ulikuwa mchungu na mzito kwake. Lakini mtamu mdomoni na hili likamanisha kwamba nirahisi kuliongea na kuhubiri ila kulishika kuna uchungu mkali.
Lakini basi huu ndio ujumbe aliopewa kuusema na ilimpasa auseme bila kuficha au kudanganyadanganya.

Nasi ndugu zangu tunahitaji watu akina Ezekieli nyakati zetu. Mara nyingi kusema ukweli kwa mapana yake sio kitu rahisi kwani ukweli japokuwa hutuweka huru, lakini bado ni mchungu sana. Hivyo ni wachache wenye ujasiri wa kuusema. Watu wengi ni wezi, wafisadi na wakatili kwa sababu tumekosa akina Ezekieli wa kuwaaeleza ukweli. Wengi wetu tunakuwaga kama wale manabii wa uongo. Tunasifia ili watupatie kitu Fulani. Tuachane na tabia za namna hii ndugu zangu. Hii inatukosesha manabii.

Kwenye somo la Injili tunaalikwa kuishi na moyo wa unyoofu kama watoto wachanga. Wao kweli ni manabii, wao wapo tayari kusema ukweli kama ulivyo. Sisi tuwe kama hawa watoto, tuuseme ukweli jinsi ulivyo.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni