Jumamosi, Agosti 08, 2020
Jumamosi, Agosti, 8, 2020,
Juma la 18 la Mwaka
Kumbukumbu ya Mt. Dominiko
Hab 1:12 – 2:4;
Zab 9: 8-13;
Mt 17: 14-20.
TUOMBEANE
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana tunaanza kwa kuingalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na ujumbe kwamba hakika Mungu hatamtupa au kumwacha yeyote anayemkimbilia. Yeyote anayemkimbilia, hakika ataokolewa naye kwani Mungu atampigania. Hata kama itatokea nyakati ambapo mtu huyu atakumbana na maadui wengi, hakika basi Mungu ataendelea kumpigania kwani Imani kwa Mungu huokoa.
Hii zaburi inatumika kusisitizia kile Habakuki anachotuambia kwenye somo la kwanza leo.
Yeye anamalizia somo lake la leo kwa kusema kwamba mwenye haki ataishi kwa imani yake. Hii ni kwa sababu tangu mwanzo Mungu ni mtetezi wa wanyonge, yeye haungani kabisa na waovu ili kuwakandamiza watu wema, hafurahishwi na uovu kamwe. Hivyo Habakuki anamwambia Mwenyezi Mungu kwamba jamani aendelee kuwapigania wenye haki, asikae kimya huku akiwaona wakitendewa kila aina ya ubaya.
Somo hili ni la muhimu kwetu sisi ndugu zangu na lina ujumbe mzito wa kutuambia leo. Cha kwanza linatuambia kwamba mwenye haki ataishi kwa imani. Hivyo basi tujitahidi kuwa kwenye kundi la wenye haki. Tuepuke na kudhulumu mali za watu au kuwadhulumu mayatima au kugombania mali za wajane. Tuwakemee baadhi yetu hasa wale wanaokwendaga kugombania mali za mayatima na wajane na wasiojiweza. Nasi kati yetu kama tumewahi kushiriki kwenye matendo kama haya, basi tumwombe Mungu msamaha.
Cha pili ndugu zangu ni kwamba tujitahidi kuwa watu wa imani. Imani hujengwa kwa njia ya sala, kusoma maandiko matakatifu, na kufanya matendo mema, na kumwomba Mungu kila siku atukuzie Imani yetu. Hii ndio itakayotuokoa. Itatusaidia kupambana na magumu mbalimbali hapa ulimwenguni na hii ndiyo itakayotualika machoni pa Baba. Ukweli ni kwamba mwenye imani, akipatwa na matatizo, huyashughulikia kwa utulivu na ubora zaidi kuliko yule asiyekuwa na imani. Asiye na imani, ataonesha hali ya kukata tamaa kwa kiasi kikubwa saana.
Kwenye somo letu la injili tunaona jinsi imani inavyookoa na leo basi tumesikia Yesu akisema kwamba inaweza hata kufanya mambo ya ajabu kabisa-yaweza hata kuhamisha miti na milima. Inaponya magonjwa mbalimbali. Sisi ndugu zangu yapaswa kumwambia Mwenyezi Mungu atupatie Imani kila siku. Hii ni kwa sababu bado imani yetu ni ndogo sana, bado hatujaweza kuwa na Imani hadi kwenye kile kiwango cha juu. Basi kila siku tuwe tukimwambia Mungu kwamba Ee Mungu naomba unipatie imani, nifanye niwe mtoto wako bora na unisaidie nikue kiimani. Ee Yesu nisaidie. Hii iwe ndio sala yetu ya kila siku.
Maoni
Ingia utoe maoni