Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Agosti 05, 2020

Jumatano, Agosti 5, 2020,
Juma la 18 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Dominiko

Yer 31: 1-7;
Yer 31: 10-13;
Mt 15: 21-28

WOTE NI WATOTO WA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na ujumbe wa matumaini. Baada ya kutenda dhambi, na kuwaletea maneno na ujumbe mkali wa kuwaonya, sasa Israeli anawapatia tena ujumbe wa matumaini kuonyesha kwamba Mungu ni mwenye huruma nyingi sana japokuwa yeye hafurahishwi hata kidogo na uovu. Akiona uovu anakuja mara moja na kuukemea, na kuukataa. Hauvumilii hata kwa dawa.

Ndivyo tunavyofundishwa na sisi ndugu zangu. Tuwe watu wa msimamo na wasiovumilia ubaya. Lakini tutambue kwamba huruma inahitajika pia. Baadhi yetu tunajidai kwamba tupo wakali kila wakati, lazima tuwe makini kila wakati lakini tutambue kwamba huruma inahitajika na ni ya muhimu sana. Duniani tunatakiwa kuwa na huruma kwani sote tunaokolewa kwa huruma ya Mungu. Hakuna awezaye kuokoka bila huruma ya Mungu. Hata huyu asiyehurumia wengine aambiwe kwamba yeye pia anahitaji huruma ya Mungu.

Somo hili linatoa ujumbe mkali hasa kwa baadhi yetu ambao huwa tunahusishwaga kwenye kusuluhisha kesi mbalimbali kwenye jamii yetu. Tusuluhishe tukiwa na huruma na tutoe hukumu yenye huruma kwa wakosaji. Wakosaji wengi wanakwazika kwa sababu ya kutokuonewa huruma na baadhi yetu. Mara nyingi, inatakiwa hata baada ya kesi kumalizika, yaani mkosaji ajisikie matumaini tena kwamba jamani hata mimi ni kiumbe cha Mungu na hivyo basi atoke na Moyo wa kubadilika na kutaka maisha mapya. Ukisuluhisha kesi halafu mwishoni mkosaji akaondoka katika hali ya kukata tamaa-akilalamika kwamba kaonewa, jamani nashauri ni vizuri kuangalia tena kesi hizi na kurudia tena hukumu hii.

Katika hukumu, inatakiwa kila mmoja atoke na matumaini, akiwa na moyo dhabiti wa kujirudi na kusonga mbele. Na hii ndio maana ya usuluhishaji. Hivyo sisi tunaopataga nafasi za kusuluhisa kesi za watu jamani tujue kwamba tunakwenda kuwapa watu matumaini na si kuwatangazia dhambi zao au kuwasema vibaya. Hili ni la muhimu sana.

Katika injili ya leo, tunamkuta Yesu akimjibu mama wa kikanaani kwamba haifai chakula cha watoto wapewe mbwa. Ndugu zangu, Yesu alikuwa na maana kubwa sana kutumia maneno haya. Hii ni kwa sababu yule mama mkananayo alitokea kwenye Imani za kipagani waliokuwa na wanamazingaumbwe walioweza kufanya ishara na baadhi zilizoweza kufanana na zile za Yesu. Hivyo ilimbidi Yesu kumjibu hivi kuonesha kwamba ishara na miujiza ya Yesu ni kwa ajili ya watu wenye Imani na si mazingaumbwe. Ile ni miujiza mitakatifu, na lazima ipokewe na imani. Hivyo ilimbidi yule mwanamke apewe msisitizo ili asije akaishia kumwona Yesu kama mwanamazingaumbwe na kushindwa kuishia kutokuwa na imani. Lakini kwa jibu hili, yule mama alidhihirisha kwamba ana imani na hivyo basi alistahili kuponywa.

Nasi tutambue kwamba mara nyingi hatupati kile tunachokiomba kwa sababu tunamuona Yesu kama mwanamazingaumbwe bila kuwa na imani naye. Tunakuja kanisani na kumtaka Yesu atufanyie ishara na ishara hizi tunazitaka zifanyike kwa mfumo wa wale waigizaji wa kinigeria wanavyozifanyaga kweli zile video zao na maigizo. Tusimjaribu mwenyezi Mungu jamani. Tuwe na imani. Tusione kwamba ishara lazima zifanyike kwa mtindo wa waigizaji wa kinigeria. Wapo wengi wameanza kuigiza hivyo hata kwenye makanisa lakini sisi yabidi tuwe watu wa imani na kujua kwamba Yesu anataka imani; yeye si mwanamazingaumbwe.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni