Ijumaa, Julai 31, 2020
Ijumaa, Julai 31, 2020,
Juma la 17 la Mwaka wa Kanisa
Yer 26: 1-9;
Zab 68: 5, 8-10, 14;
Mt. 13: 54-58.
UDONGO WENYE RUTUBA ILI KUPOKEA BARAKA ZA MUNGU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi katika neno la Bwana tunakutana na nabii Yeremia kwenye somo la kwanza akitoa unabii mkali juu ya hekalu la Yerusalem kwamba litakuwa sehemu ya mahame, isiyokuwa na chochote, itakayolaaniwa kama ilivyokuwa ile altare ya Shilo ambapo kutokana na ubovu wa makuhani wake, iliishia kuwa altare iliyolaaniwa kabisa, na cha ajabu makuhani wake walikufa kifo cha aibu na ukuhani wa wale makuhani waliohudumia Shilo ulihamishiwa kwa familia nyingine.
Ndivyo hivyo leo Yeremia anavyowaeleza wana wa Yuda kwamba nao wasipobadilika, lile hekalu lao litapatwa na kile kilichokipata Shilo kwamba nayo itakuwa sehemu ya laana, sehemu itakayosababisha vifo kuanzia vya makuhani wake na kusababisha mji wote kupata madhara makubwa. Unabii huu wa Yeremia ulitimia mwaka 587BC ambapo Nebukadneza alikuja na kuliteketeza hekalu lile, akawauwa manabii wake na kupafanya pale hekaluni kuwa sehemu ya laana. Yote haya yalitokea kwa sababu ya ukaidi na uchafu wa wale makuhani na taifa lote la Yuda. Lakini sasa kwa kitendo cha Yeremia kutoa unabii wa namna hii kilisababisha sana shida kwake kwani wengi kati ya watu wake walifikiri kwamba kwa kitendo cha lile hekalu kuwako kati yao, basi Mungu atawalinda na kuwafanya wasipatwe na chochote licha ya kwamba wao hawakuwa na imani yoyote. Hivyo walimkamata Yeremia na kumpiga Sana.
Ndugu zangu, wana wa Yida walitegemea waokolewe kwa kitendo cha hekalu kuwako pale mjini Yerusalem. Kwa hili walitegemea wapatiwe ulinzi bila ya wao kuonesha moyo wa sala na toba. Hili linafanana na baadhi yetu wakristo tunaolalia Biblia ati zitukinge na maadui bila ya sisi kusali au kuamini kile kilichoko kwenye Biblia. Au wengine tunavaa misalaba na rozari tukitegemea itukinge na maadui bila ya sisi wenyewe kubadilika na kuamini kinachomaanishwa na msalaba huo yaani Yesu Kristo. Mungu leo amemtuma Yeremia awatolee unabii huu mkali kwamba hekalu lao litaharibiwa ili wabadilike wajue kwamba hawaokolewi kwa kitendo cha wao tu kuwa na hekalu bali kwa kuwa na Imani kwa kile kinachomaanishwa na hekalu. Nasi ndugu zangu tuwe hivyo hivyo. Tuwe na imani kwa kile kinachomaaanishwa na misalaba na Biblia na sakramenti zetu mbalimbali.
Kwenye somo la Injili, tunakutana na Yesu akidharauliwa na watu wa nyumbani kwake wakidai kwamba wanamfahamu. Hivyo, walikataa kumwamini kwa madai kwamba ati hawaoni cha ziada kwake. Hivyo, watu wa nyumbani kwake waliilishia kutokupata neema zilizoletwa na Yesu.
Ndivyo ilivyo kwa wengi wetu hasa tuliowazoea mambo matakatifu na mapadre na masista. Tumeishia kuwa kama hawa watu wa kijiji cha Yesu: tunaishiaga kusema-aah, haya mambo tunayafahamu, hakuna jipya, mbona tunayashikaga shikaga tu? Hakuna jipya hapa. Mbona huyu Padre namfahu? Tena nilimpa ofa juzi ya kinywaji yukaongea!-unashindwa kupokea ujumbe wa Injili anao uhubiri! Mbana haka kapadre nilikaona tangu kakiwa kadogo sanaa, kataniambia nini? Na tunaishia kutokupata neema za kutosha. Lakini wanaoamini, wale wasio onesha mazoea kila siku wanabarikiwa. Sisi tuogope mazoea na mambo matakatifu ni adui wa imani yetu. Ameni.
Maoni
Ingia utoe maoni