Jumatatu, Julai 27, 2020
Jumatatu, 27 Julai, 2020,
Juma la 17 la Mwaka
Mt 13:31-35
UKUBWA MACHONI MWA MUNGU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi tafakari ya neno la Mungu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo Mungu anaonyesha ni kwa namna gani Israeli asivyofaa mbele yake. Tena anatumia mfano wa ajabu kabisa unaohusu nguo ya siri ya mwanadamu. Hii ni nguo kweli yenye uhusiano mkubwa sana na mwanadamu na mwanadamu lazima aiheshimu na mara nyingi huiheshimu sana na kuipa usiri na heshima ya pekee kuliko nguo nyingine. Lakini hii nguo ikishaharibika, huwa inakosa heshima yake na huwa ni aibu sana hata kuiweka kiunoni kwani itakuaibisha na kukupatia sifa mbaya sana. Hivyo cha kufanya ni kuiteketeza. Ndivyo sasa ilivyo kwa Israeli.
Kweli lilikuwa ni taifa lililokuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu kuliko mataifa yote na ndio maana Mungu anatumia hata nguo ya ndani kuonyesha huu ukaribu. Lakini wakajiharibu na kuwa wabaya na sasa ikabidi wawekwe pembeni kwani kama Mungu angaliendelea kuhusiana nao, hakika angalijishushia heshima mwenyewe; angaliishia kudharauliwa na wengine na kuonekana kama asiyekuwa na maadili au sheria njema. Na hivyo Israeli ilibidi atupwe pembeni.
Ndivyo ilivyo mbele ya Mungu hadi siku hii ya leo ndugu zangu. Kweli tukitenda dhambi, mara nyingi Mungu inambidi avunje angalau kwa muda ule uhusiano na sisi na wakati huu huwa tunapatwaga na matatizo fulani fulani lengo likiwa ni kuwafanya wengine wasikwazike, wasije wakaacha kumtii Mungu kwa sababu ya sisi kuwa na miongozo mibaya. Kwani uhusiano ukiendelea, ni kwamba watakaoendelea kukwazika watakuwa ni wengi zaidi na zaidi. Hapa Mungu hulazimika kuvunja uhusiano.
Hivyo basi ndugu zangu tutambue kwamba tunapotenda dhambi, kweli ni chukizo kubwa sana kwa Mungu. Huwa tunamtesa Mungu kwani kwa asili yeye haungani na dhambi halafu kwenye kufanya yale maamuzi ya kutoa adhabu ni kwamba yeye analazimika kuyafanya haya maamuzi na si ati unakuta anapenda. Unakuta inabidi ayafanye kwa ajili ya Amani na usalama wa wa mwanadamu. Hivyo tuchukie dhambi jamani.
Na kingine tutambue kwamba zile dhambi za makwazo Mungu anazichukia sana na humfanya Mungu akasirike na adhabu yake ni kubwa. Adhabu yake ilishatangazwa na Yesu. Na ndio maana anayekwaza kwa kweli huadhibiwa vikali kwani maanguko ayaletayo ni makubwa.
Kwenye injili Yesu anaelezea mfano wa ufalme wa Mungu kwa kuulinganisha na chembe ya haradali ambayo ni ndogo lakini matunda yapatikanayo ni makubwa. Ni mfano kwetu na himizo kwamba hata sisi kwenye udogo wetu na umaskini wetu, bado tunaweza kuwa na kitu cha kufanya na kuweza kuwafanya wengi waje na kutafuta makao chini yetu. Chembe ya haradaili huwa haijidharau kwa udogo wake. Na sisi ni hivyo hivyo, bado tunauwezo wa kufanya kitu. Tusijidharau hata kama ni maskini.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni