Alhamisi, Julai 23, 2020
Alhamisi, Julai 23, 2020,
Juma la 16 la mwaka wa Kanisa
Yer 2: 1-3.7-8, 12-13;
Zab 36: 5-10,
Mt 13: 36-43
KUITWA ILI KUMSIKILIZA NA KUMUONA MUNGU!
Masomo nimechagua ya siku ya kawaida. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na zaburi hii inasisitizia kwamba ni kwa Bwana peke yake kunakopatikana uzima. Hivyo mzaburi anawaalika watu wamtumainie Bwana peke yake, na kamwe wasimuache kumtegemea.
Haya maneno ya zaburi yanatumika kutia nguvu ule ujumbe tunaokutana nao kwenye somo la kwanza toka kitabu cha nabii Yeremia. Wana wa Yuda wanalaumiwa kwa kuacha kumtumainia Mungu; wamechimba visima vyao wenyewe ili wapate huko uhai, ili waache kumtegemea Mungu. Lakini cha ajabu hivi visima ni visima vinavyovuja au kutoboka na hivyo havishiki maji hata kidogo. Na labda tuelewe kwamba kisima kinachovuja ni hasara tu kwani ni vigumu kukirepea-na ukweli ni kwamba popote pale kujenga kisima ni gharama kubwa. Hivyo unakuta umekwisha tumia gharama kubwa kwenye kukijenga kisima hicho lakini mwisho wa siku kinaishia kuja kuvuja. Kweli ni hasara sana. Haya yote ni maneno ya lugha ya picha yanayomaanisha kwamba Israeli amemuacha Mungu na kujitafutia vimungu vyake yeye mwenyewe na visanamu vyake ili ati vimsaidie na kumwacha Bwana Mungu wa Israeli.
Na unakuta wanatumia gharama na muda mwingi mno kwenye kujitegenezea hivyo vimungu lakini mwisho wa siku hawafanyi chochote; kwani miungu hiyo sio kitu. Ni kama sisi nyakati zetu ndugu zangu. Tunakazana kutumia gharama na muda mwingi kwenye kuhakikisha kwamba tuna smart phone au simu za touch. Tuko tayari hata kubana sehemu zote au hata kuiba ili tuwe nayo. Na ikikosa salio la kuiwezesha kupata internet tupo tayari kufanya lolote ipate. Tunakazana kila siku, tunatembea na hizi simu, tunahakikisha kwamba kila mahali lazima niwe nayo-ukiikosa unachanyanyikiwa na kukosa amani. Lakini ndugu zangu, kama hatutaonesha hekima kwenye matumizi yake, basi simu hii itakuwa kama kisima tulichojichimbia lakini kikawa kinavuja na hivyo kutuingiza hasara kubwa sana. Kwani ndani ya simu hiyo hiyo kama hatutaonesha hekima basi unakuta ndio inatufilisi kwa kumaliza fedha zetu-percent kubwa ya fedha itaishia kwenye kuitengeneza endapo itaharibika vitu kama screen, au kwenye ununuzi wa salio. Pia ndani yake twaweza kujifunza kila aina ya uchafu na kuchafua roho zetu, na pia tutatumia muda mwingi kwenye simu tu na kusahau kwamba muda unahitajika kwenye mambo mengine yalioyo muhimu Zaidi. Huku ndiko kuvuja kwa kisima tulichokichimba, hii ndiyo gharama kubwa ya hiki kisima tulicho kichimba.
Vipo visima vingi vya namna hii tulivyovichimba na huwa vinatuingizia hasara kila siku. Hivyo lazima tujitahidi kuvitambua na kuachana navyo kwani kisima kinachovuja kinatupatia hasara kama simu zinavyotupatia hasara hasa kwa baadhi yetu tuliokosa hekima kwenye matumizi yake.
Kwenye somo la injili, tunakutana na Yesu akiwaambia wanafunzi wake kwamba kwa wao wamebahatika kujaliwa bahati ya kutambua siri za mbinguni. Na hizi siri walibahatika kwa sababu ya kukaa muda mrefu na Yesu na kumwomba awafafanulie siri hizo. Hii yamaanisha kwamba walichimba kisima chao sehemu salama na inayostahili. Sisi ndugu zangu tukazane kukaa karibu na Yesu wa Ekaristi, atupatie ufahamu wa siri zake na kutufanya tuzitambue siri za ufalme wa mbinguni Zaidi na zaidi. Huku ndiko kuchimba kisima kisichovuja bali chenye maji ya kutulisha na kutupeleka mbinguni. Achana na visma vinavyovuja-hutupatia gharama kubwa sana kwetu. Garama ya kutunza nyumba ndogo, pesa zote unazomalizia huko, garama ya kuhifadhi siri ili mke wako/mume wako asijue nimateso. Hivi vyote nivisima vilivyo toboka na hakika haviwezi kuhifadhi maji. Kaa na Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni