Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Julai 25, 2020

Jumamosi, 25 Julai, 2020,
Juma la 16 la Mwaka wa Kanisa

Sikukuu ya Mt. Yakobo, Mtume

2 Kor 4: 7-15;
Zab 125: 1-6;
Mt 20: 20-28


KUJITENGENEZA KATIKA KRISTO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi kanisa linasherekea sikukuu ya Mt. Yakobo mtume. Huyu tunamsikia leo katika injili yetu akiombewa na mama yake sehemu maalumu kwenye utawala wa Yesu. Mama yake alikuwa na mategemeo kwamba Yesu angekuja kuwa mfalme mkuu na jemedari atakayepindua kaisari wa Roma na kuanzisha ufalme wake ulio mkuu sana. Hivyo basi mama yake huyu Yakobo leo katika injili anawahi lengo likiwa ni kumwombea mtoto wake nafasi ya juu kwenye utawala atakaoanzisha Yesu. Yesu anamshangaa huyu mama na kumwambia kwamba hajui aombalo; yeye yuko kidunia Zaidi-na bado hajamtambua Yesu zaidi.
Yesu anamweleza kwamba suala la mtoto wake kukaa kuume au kushoto katika utawala wake hawezi kulitolea majibu sasa kwa sababu bado safari ni ndefu kwa hawa watoto wake. Bado anasafari ya kuenenda na kwenye safari hii ni lazima aoneshe mapambano ya kutosha. Cha ajabu ni kwamba huyu aliyeombewa nafasi kwenye ufalme wa Yesu alijikuta anakuwa miongoni mwa mitume wa kwanza kabisa kufa kishahidi akiitetea Imani ya Yesu. Alikufa kishahidi mwaka 44AD (Mdo 12:1-2). Kweli alijitahidi kuitetea injili na kuishia kukinywea kikombe kama kile alichokunywa Yesu. Hivyo alifanya bidii sana kuishi imani yake. Tunaamini kwamba yule mama yake aliyekuwa amemuombea nafasi kwenye mkono wa kulia wa Yesu kwa kufikiri kwamba Yesu angekuwa mfalme kama wafalme wa dunia, naamini aliweza kupokea hali hii ya kumwona mtoto wake akiuawa na Herode kwa kukatwa kichwa.
Ndivyo maisha ya kumfuata Kristo yalivyo ndugu zangu. Ni maisha ya sadaka, maisha ya kumfia Yesu, ndugu zako wanaweza kuwa na matumaini makubwa na tofauti sana juu yako; wanaweza kuwa wanategemea wapate hiki na hiki toka kwako na wao wafurahi lakini mwisho wa siku lazima tuwe kama huyu Yakobo-lazima tuishi kwa ajili ya Kristo kama Yakobo alivyoishi. Tukiwa katika utume wetu, tumuombe Mungu awabariki ndugu zetu pia, na wazazi, na kaka, wajomba na mashangazi-wale wanaotegemea msaada wa kifedha toka kwetu lakini basi hatuwezi kuwapatia. Tumuombe Mungu awapatie na moyo wa kupokea maisha yetu, na kutuelewa na abariki na kazi za mikono yao ndugu zangu.Wengi wakati mwingine hudhania mapadre wana fedha nyingi na wanapaswa kusomesha watoto wao, tuwaombee watambue upadre nikujitoa na kufanya kazi ya Kristo tofauti na wanavyodhani.
Katika somo la kwanza, tunakutana na mtume Paulo akiwaeleza wakristo wa Korintho kwamba wao ni kama vyombo vya udongo vilivyobeba hazina kubwa. Hazina inayozungumziwa hapa ni injili ya Kristo na vyombo vya udongo ni wahubiri wa injili. Wao kama wahubiri ni watu dhaifu sana wasiokuwa na chochote. Lakini injili wanayoihubiri ina thamani kubwa ajabu, ni ya thamani kuliko hata dhahabu na uwezo iliyo nayo ni mkuu ajabu. Ndivyo injili ilivyo. Ina nguvu ya kuokoa, ina nguvu ya kubadilisha ulimwengu na kuugeuza kwa Kristo na kuufanya uokoke.
Sisi wahubiri wa injili tuikubali nguvu hii. Tuiheshimu injili, tujitoe kwa ajili ya kuhubiri injili. Na sisi wahubiri tuache kujivuna, tunajiona kwamba sisi tunayonguvu kuliko injili-kwamba kinachotupatia thamani ni injili yenyewe na si kingine. Mwenye ndoa kinachompatia heshima ni kuishi kiinjili kama ndoa yake isemavyo. Kadhalika na Padre kinachompatia thamani ni uaminifu wa kuishi kiinjili katika upadre wake. Hivyo tuikweze injili kuliko vyote. Tuache majivuno, tuiishi injili, tuongee injili na tuachane na kuongea vionjo vyetu, tufikirie injili na tuache kufikiria malimwengu. Hili ndilo litakalotupatia wokovu, namna hii tutaweza kuifahamu nguvu ya injili.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni