Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 22, 2020

Jumatano, Julai 22, 2020,
Juma la 15 la Mwaka
Sikukuu ya Mt. Maria Magdalena

Wim 3:1-4 or 2Kor 5:14-17;
Zab 63: 1-5, 7-8;
Yn 20:1-2, 11-18.

KUZAMA KATIKA KRISTO!

Maria Magdalena anachukuliwa kama mwanamke muhimu wa pili katika Agano Jipya baada ya Bikira Maria, Mama wa Yesu. Alisafiri na Yesu katika maisha yake ya utume na alishuhudia matukio mawili ya katika maisha ya Yesu, Mateso na ufufuko. Injili inamuelezea kama Mwanamke jasiri aliye simama na Yesu wakati wa mateso, kifo.
Maria Mgadalene ni mfano wa kweli na ulio kamili katika kuinjilisha, Mwinjilishaji wa ujumbe kamili wa furaha ya Pasaka. Mwanamke huyu “ambaye alimpenda sana Bwana na Bwana alimpenda”. Alikuwa ni mmoja wapo wa wafuasi waliomfuata Yesu, alimsindikiza hata katika safari yake ya mateso na hata bustanini alipokutana naye, alikuwa ni shuhuda wa kwanza wa “huruma ya Kimungu”. Injili ya Yohane inatuambia kuwa Maria Magdalena alilia kwasababu hakuona mwili wa Yesu (Yn 20:11); na Yesu alikuwa na huruma kwake kwa kujionesha kwake kama Mwalimu wake, na kugeuza machozi yake kuwa furaha ya Pasaka.
Alikuwa na heshima ya kuwa shuhuda wa kwanza wa ufufuko wa Yesu, wa kwanza kuona kaburi li wazi na wa kwanza kusikia habari za ufufuko. Yesu anaonesha kujali kwa namna ya pekee kwa huyu mwananmke na kumuonesha huyu mwanamke huruma ya pekee kwasababu mwanamke huyu alionesha mapendo kwa Kristo kwa kumtafuta katika bustani na hata katika mateso. Katika hali hii tunaweza kulinganisha mwanamke aliye anguka katika bustani ya Edeni na mwanamke huyu katika bustani wakati wa ufufuko. Wakwanza alileta kifo kwa mwanandamu na wa pili anatangaza uzima akiwa kaburini.
Katika bustani ya ufufuko Bwana wetu alimwambia Maria “usinishike” (Yn 20:17). Huu ni mwaliko wa kuingia katika Imani inayo zidi mambo yanayo onekana na zaidi ya akili ya mwanadamu baada ya kukutana na mafumbo ya Kimungu ambayo hayatangazwi kwa Maria tu bali kwa Kanisa zima. Huu ni mwaliko kwa kila mfuasi wa Yesu aache kutafuta utukufu binafsi au utukufu wa dunia hii, lakini kwa Imani kumtafuta Mungu anaye ishi na mfufuka.
Alikuwa shuhuda wa kwanza wakumuona Bwana mfufuka, alikuwa pia wa kwanza kutoa ushuhuda kwa mitume wake. Alitimiza amri ya Bwana mfufuka: “nenda ukawaambie ndugu zangu, napaa kwa Baba yangu na Baba yenu, kwa Mungu wangu na Mungu wenu”. Maria Magdalena aliondoka na kutangaza kwamba amemuona Bwana na kwamba amemuambia mambo haya (Yn 20:17-18). Na hivyo, akawa muinjilishaji, mjumbe anaye hubiri habari njema za ufufuko wa Bwana. Alitangaza kwa mitume kitu ambacho wangekuja kukitangaza baadae katika ulimwengu wote. Na hivyo anaitwa “Mtume kwa Mitume”. Yeye ni shuhuda wa Yesu mfufuka na ametangaza ujumbe huu kama Mitume wengine walivyofanya. Utume huu wa wamanamke huyu ni mfano kamili wa wanawake wote katika kanisa la sasa!
Tafakari tamaa ya Bwana wetu kwamba sisi siku moja tufurahi naye mbinguni. Tumsikie akituambia “Napaa kwa Baba na kualika kujiunga nami kwa moyo wako wote. Nikaribishe ndani mwako na niruhusu mimi niweze kuungana nawe. Ninakupenda Bwana na ninatamani kuwa mmoja pamoja nawe. Bwana niruhusu niingie moyoni mwako nawe uwe moyoni mwangu.

Sala:
Bwana, ninataka kuzama ndani yako. Ninatamani kuungana nawe katika hali zote. Njoo uishi moyoni mwangu na nifanye niwe mmoja nawe. Yesu, nakutumainia wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni