Jumatatu, Julai 20, 2020
Jumatatu, Julai 20, 2020.
Juma la 16 la Mwaka
Mik 6: 1-4, 6-8
Zab 49: 5-6, 8-9, 16-17, 21, 23;
Mt 12: 38-42
MKUBWA KULIKO YONA
Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunamkuta Mungu akiwaeleza wana wa Israeli juu ya wema aliowatendea, makuu yake aliowafanyia. Jinsi alivyowakwisha kuwatuma Musa, na Aron na Miriam kuwaongoza. Jinsi alivyowahi kuwakomboa utumwani na kuwapigania ili wasinyanyaswe. Kweli Mungu amewatendea mambo makubwa kwa kweli ukiangalia.
Mika anawaambia kwamba kama watakumbuka wema huu wote, hawana cha kuweza kumlipa Mwenyezi Mungu. Cha kufanya tu ni kuwa waaminifu kwake na kuutangaza huu wema wa Bwana na kuupeleka huu wema wake wakautangaze kwa watu wote. Hiki tu ndicho Mungu anachotaka.
Hili ni somo muhimu sana kwetu ndugu zangu. Sisi tumetendewa makubwa sana na Mwenyezi Mungu. Amekuwa akitutetea kwa kiasi kikubwa sana. Amekuwa akitulisha chakula, wengine ametuganga magonjwa yetu, wengine ametufanya tukafaulu mitihani, wengine tukaweza kulipa madeni yetu, akatuepusha na watesi wetu, akatufanya tusiabike. Tukifikiria wema kama huu kweli huwa hatunaga cha kumlipa; cha kufanya ni kukiri haya makubwa aliyokutendea Mungu na kuupeleka huu wema kwa wengine. Hilo ndilo la muhimu.
Mimi kama padre Mungu amenitendea makubwa kwa kunileta altareni pake nimtumikie. Mungu kanipigania. Sina cha kumlipa Zaidi ya kuutangaza wema huu wa Bwana kwa wale ninaoishi nao, niwapende Zaidi, niwatie moyo, niwaambie kwamba kwa Mungu zipo fadhili tupu. Wale wanaokata tamaa nao waimarike kwa maneno hayo. Mungu anatutendea wema ili walio wa karibu waufurahie, hivyo tuhakikishe kwamba tunaanzia wema wetu na wale tunaoishi nao. Hili ndilo Mungu analotaka.
Katika Injili yetu basi tunakutana na Yesu akiwalaumu Wayahudi kwa sababu wanangangania kuona ishara, wanataka ishara. Yeye anawaambia kwamba hatawapatia ishara nyingine isipokuwa ile ya Yona. Hawa walikuwa ni watu wasio na Imani waliokuwa wanataka kutumia ishara kwao wazione kama kichekesho au kitu cha kuwafurahisha, kusisimue akili zao na mioyo yao; wapate cha kuongea na kutolea umbea na si ati wapate cha kutangazia wema wa Bwana. Kama walitaka ishara ya kuwasaidia ili waweze kutangaza wema wa Bwana hakika walikuwa wanazo nyingi tayari; walikwisha kupewa maishani.
Sisi hadi tuutangaze wema wa Bwana tusitafute ya ziada sana. Mungu tayari amekwisha kuwa ishara kwetu kwa namna anavyotulinda kila siku. Tuutangaze wema wake daima. Kutafuta ya ziada ni dalili za kukosa imani.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni