Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Julai 16, 2020

Alhamisi, Julai 16, 2020
Juma la 15 la Mwaka

Isa. 26:7 – 9, 12, 16 – 19
Zab. 102:12 – 20 (K) 19
Mt 11:28-30

MWALIKO KUTOKA KWA YESU

Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la Tisa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza lasisitiza kwamba njia ya mwenye haki ni nyofu na Mungu mwenyewe huinyoosha njia ya huyu mwenye haki. Kutokana na njia yake kuwa nyofu, watu humkimbilia kwani kutoka kwake huona tumaini, huona haki, patokeapo na shida huyu mwenye haki ndiye atakayekimbiliwa, ili awaletee watu tumaini, atatutue kesi zao. Lakini wasiokuwa na haki hukimbiwa kwani wao hupindisha mambo, hula rushwa, kama ni kesi wao wataipindishapindisha tu, hivyo huishia kuwaumiza watu na kuwaletea watu madhara makubwa.
Basi kila mmoja wetu leo anganganie kuwa mwenye haki, ahakikishe kwamba yeye si mtu wa kupindisha mambo, penye shida tusaidie kutatua migogoro yote na kwa namna hii kweli tutaweza kuwa tumaini kwa watu. Mara nyingi tunakimbiwa kwa sababu tumewaumiza wengi kwa matendo yetu. na pale tulipowaumiza wenzetu kwa kukosa kuwa watu wa haki, basi leo tuombe msamaha mbele ya Mungu na sala yetu leo iwe ni kwa ajili ya kuomba ili njia zetu zinyooshwe, tusiwe watu wa kupindisha mambo.
Yesu katika Injili anawaalika wote wenye shida na kulemewa na mizigo waje mbele yake na kupata pumziko. Anaweza kuwapumzisha kwani Yesu alikuwa mtu wa haki na njia yake ilikuwa nyofu. Sisi nasi tukiwa na njia nyofu tutaweza kuwakaribisha wale wenye shida na kulemewa na mizigo na kuwapumzisha. Tuachane na upendeleo-huu hutufanya tushindwe kuwapokea wale wenye shida na wenye kulemewa na taaabu mbalimbali za kimaisha. Ulafi na tamaa mbalimbali pia ndio unaotufanya tushindwe kushiriki kwenye shida za watu. Tuepukane na haya ili tuweze kushiriki kwenye shida za watu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni