Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Julai 13, 2020

Jumatatu, Julai 13, 2020,
Juma la 15 la Mwaka

SOMO 1
Isa. 1:10 – 17
Zab. 50: 8 – 9, 16 – 17, 21, 23 (K) 23
Mt 10: 34 - 11: 1.


MFUASI WA KRISTO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati inasisitizia kwamba Bwana ataonyesha wokovu wake kwa wanyofu wa moyo. Anasisitiza kwamba wanyofu wa moyo sio wale ati wanaojidai kutoa sadaka nyingi na za kuteketezwa kama za kondoo na mbuzi: ni wale wanaowahangaikia mayatima, wajane, wanaonewa, na kuwapa moyo waliokata tamaa.
Zaburi hii imetumika kwenye kusisitizia juu ya ujumbe tuupatao kwenye somo la kwanza toka kwenye kitabu cha nabii Isaya. Yeye anasema kwamba amechoka kutolewa moshi wa sadaka za kuteketezwa-kwa sababu anatolea sadaka kwa wanaotenda maovu, wasiomsikiliza, kwa wanaoonea wengine, na kwa wasiotenda haki. Hivyo anataka wabadilike, sio kutoa tu sadaka bali na matendo yao yabadilike na yawe ya kutia moyo Zaidi na zaidi.
Somo hili lina mengi ya kutuambia: linapinga sana maisha ya kujionesha na kujipendekeza: unakuta watu tunatumia kanisa kama sehemu ya kujionesha, sehemu ya kutoa mengi: baadhi yetu wafanyabiashara baada ya kudhulumu watu na kupata faida labda tunakuja kanisani na kutoa kidogo ili kujionesha kwamba sisi ni wema lengo likiwa ni kuficha uovu tunaotendaga. Pia wapo baadhi yetu tunakwenda kwa vituo vya watoto yatima na kujionesha kutoa lengo likiwa ni ili tusifiwe. Halafu zile sifa kidogo tunazozipata zinatuvimbisha kichwa ajabu, pale kanisani unaposifiwa unajiona kwamba kweli wewe ni mwema na unafanya vizuri sana. Lakini kumbe kwa ndani tunapalilia mzigo wa madhambi yetu mengi ajabu. Basi leo tujichunguze hasa baadhi yetu tunaokujaga kutoa shukrani zetu kanisani-tuhakikishe kwamba zile shukrani zimeambatana na moyo mwema, moyo safi, ile shukrani iambatane na haki, utu wema na huruma.
Kingine tunachojifunza ni kwamba ni lazima tukiwaona mayatima, wajane, maskini, yaani tukiwaona hawa ni lazima tushikwe na moyo wa huruma kwao, tuone watu wanateseka na kwa njia hii tubadilike jamani.
Katika injili, miongoni mwa vitu anavyosisitiza Yesu ni juu ya kuubeba msalaba wako na kumfuata, anasema tena kwamba amkaribishaye nabii kwa vile ni nabii hakika atapata baraka na zawadi ya kinabii. Sisi tusikubali kuwanyanyapaa maskini wetu au wajane au mayatima: watu hawa watufanye tumfikie Yesu kwa ukaribu Zaidi na Zaidi. Tuwe wakarimu pia kuwatunza mapadre wetu tusikubali wakate tamaa katika wito wao. Tukumbuke tukimsaidia nabii/Padre kwasababu ni nabii tuna baraka ya pakee kwani Mungu hurudisha baraka hiyo hiyo katika nyumba yako mwenyewe. Hii ni baraka ya pekee kwani Yesu alijua kabisa katika wito huu, nabii wake aweza kukata tamaa, hawana mishahara na hivyo kujiona pweke, ndio maana Yesu ametoa baraka ya pekee kwa yule anayemsaidia nabii kwasababu ni nabii. Tuchote baraka hizi kwakusaidia mapadre wetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni