Jumanne, Julai 14, 2020
Jumanne, Julai 14, 2020,
Juma la 15 la Mwaka
SOMO 1
Isa. 7: 1 – 9
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 48: 1 – 7 (K) 8
Mt 11:20-24
AMKA NA UITIKE WITO!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuuangalia wimbo wetu wa katikati ambapo tunamkuta mzaburi akielezea jinsi ulinzi wa Mungu ulivyo mkuu kwa mji wake mtakatifu yaani Sion. Mji huu unaelezewa kwamba unalindwa salama na Mungu, Mungu ndio kaweka kambi yake pale na hakika utabakia imara milele.
Zaburi hii inatumika kwenye kuelezea ujumbe wetu wa somo la kwanza leo. Hapa tunakutana na wafalme wawili:mfalme wa Arama na wa Israel wakijiandaa kuuvamia ufalme wa Yuda. Watu wanaogopa, mioyo yao inashtuka na kuona kana kwamba kila kitu kimefikia mwisho-ndio muda wao wa kuangamia basi. Lakini Isaya anatumwa na Mungu kuwatia moyo wana wa Yuda kwamba wamtumainie Mungu naye atawaokoa, wasiogope kabisa, mioyo yao iwe hodari.
Maneno ya kutia moyo kama ya Isaya alivyowatia moyo wana wa Yuda ndio yanayohitajika kwa nyakati zetu ndugu zangu. Hii ni kwa sababu tunakosa watu wa kututumainisha kwa Mungu, wengi wanatuogopesha, na hata hadithi wanazotusimulia ni za kutuogopesha-hadithi nyingi au habari nyingi tunazoambiana sisi kwa sisi ni namna jinsi shetani alivyo na nguvu au namna jinsi mizimu fulani fulani ilivyo na nguvu au jinsi mganga fulani alivyoweza kuwatesa watu fulani. Au jinsi watu Fulani walivyoweza kulaaniwa au watu ambao hawakufanya mila fulani wakaishia kuangamia.
Hizi ndizo habari tunazoambianaga. Wengi wetu tukisikia habari kama hizi tunabakia kwenye kuogopa, Imani yetu inaanguka, tunakosa matumaini kabisa na tunashindwa kumtumainia Mungu-tunaishia kuwa washirikina, waabudu mizimu, na watu waliokosa Imani kabisa. Hivyo, tunahitaji watu kama Isaya, watupatie habari za matumaini, watueleze jinsi Mwenyezi Mungu alivyo na nguvu za ajabu, jinsi alivyoweza kuifumua ile bahari ya shamu na watu wakapita, jinsi alivyomuumba mwanadamu kwa neno la kinywa chake tu, jinsi alivyoponya viziwi, viwete, vipofu, jinsi kwa miujiza ya watakatifu kama akina Papa Yohane Paul watu wengi wameweza kupona. Hizi ndizo habari tunazohitaji. Hatutaki mahabari ya waganga au mahirizi yenye nguvu hapa. Hizi zinatuogopesha tu na kutufanya tuwe watu waliokosa Imani.
Yesu leo katika somo la Injili analaumu ile miji ambapo alitenda miujiza mingi halafu hakuna aliyeonesha kuwa na imani, Imani yao ikabakia kuwa kidunchu. Anawaambia kwamba huu ni uzembe na lazima wabadilike kwani siku ya mwisho watakiona cha mtema kuni. Sisi nasi ndugu zangu Mungu ameshatutendea miujiza mingi mnoo, kutuepusha na ajali mbalimbali, kutetea watoto wetu wakafaulu shuleni nk. Tusisahau wema huu na kugeukia dhambi! Sisi tunaokujaga kanisani kila siku, tusikubali kuendelea kuogopeshwa na hadidhi au habari zinazosambaa huku mitaani kwetu juu ya waganga fulani au nini. Sisi tuoneshe kuwa watu wa tumaini kubwa kwa Mungu na hakuna kiumbe kinachomshinda Muumbaji. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni