Jumamosi, Julai 11, 2020
Jumamosi, Julai 11, 2020,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Is 6: 1- 8;
Zab 92: 1-5;
Mt 10: 24 -33
USIOGOPE!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Tisa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika zaburi ya wimbo wetu wa katikati inatueleza juu ya utakatifu wa Bwana-kwamba ni mtakatifu mno, utukufu wake u juu ya kila kitu, na hakuna awezaye kuufikia. Hivyo ana ukuu, kiti chake cha enzi ni imara, na utukufu wake umekuwako tokea nyakati zote.
Zaburi hii inatumika kusisitizia kile kinachoelezwa kwenye somo la kwanza leo ambapo nabii Isaya anapata kuona maono makuu ya utukufu wa Bwana. Yeye anapoona maono haya, anaogopa, anajiona kana kwamba ndio mwisho wake-kwani utukufu huu wa Bwana ni mkuu mno na kamwe mtu kama yeye hastahili hata kuinua macho yake na kuutazama. Na kweli Mungu alituma Malaika kumtakasa Isaya na kumpatia nguvu ya kuweza kunena na Bwana na kuutangaza utukufu wake na kuweza kuwa nabii wa Mungu na kuupeleka ujumbe wake.
Nasi ndugu zangu tuoneshe unyenyekevu wa pekee kila tukikaribiapo kiti cha Mungu:tuwe kama Isaya, tuoneshe kwamba sisi ni wadhambi tunayemuomba Bwana atakase kinywa na mioyo yetu ili tuweze kustahili kuongea naye. Mara nyingi tunakaribia mbele ya Bwana tukiwa katika dhambi, kinywa kichafu kwa kusengenya, kutukana na kukwaza wengine. Pia tunakaribia mbele yake tukiwa na dhambi nyingine nyingi kama dhuluma, kiburi, majivuno na ukosefu wa ushirikiano na ukatili. Tunapokaribia kiti cha Bwana namna hii hapa ni kukikufuru na kamwe hatutaweza kupata rehema zake na Mungu hataweza kututumia kwa kazi yake.
Kama Isaya twende mbele za Mungu na kulia na kusema Ee Bwana tazama mimi ni mdhambi, nihurumie Bwana, nitakase uovu wangu. Huku ni kuukiri ukuu wa Bwana na tukishafanya haya, naye Bwana ataanza kututumia, atafanya kazi pamoja nasi na kweli tutaweza kuvuna Baraka nyingi kutoka kwake. Tufanye hivyo kila tujapo mbele ya Bwana.
Katika somo letu la injili leo, tunakutana na Yesu akituambia kwamba mwanafunzi sio mkuu kuliko Bwana wake lakini sasa mwanafunzi lazima ajitahidi akazane na kukua ili apate kufanana na Bwana wake. Hivyo basi tujitahidi kufanana na Yesu, hili liwe lengo letu. Yeye alikuwa mnyenyekevu, aliwaonea huruma maskini, wagonjwa aliwafariji pia. Alikuwa mtii kwa Baba na utii huu uliweza kumfanya atende mengi yaliyo mazuri kwa watu, utii ulimfanya awe na faida kwa watu. Nasi tukumbuke kwamba utii utatufanya tuwe na faida kwa watu, utatufanya tuwe mkono wa vilema, miguu kwa viwete na tumaini kwa maskini na dawa kwa wagonjwa.
Isaya kwa utii wake aliweza kuwa wa namna hii. Sisi tujtahidi kufanana hivi. Kwa namna hii tutaweza kuleta heri duniani hasa kwa hawa ndugu zetu wanaopatwa na matatizo makali hapa duniani. Matatizo haya yapo kwa sababu ya ukosefu wa ushirikiano. Tuombe kuwa na utii ili tuweze kuwa watu wa msaada.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni