Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Julai 03, 2016

Jumapili, Julai, 3, 2016.
Dominika ya 14 ya mwaka wa Kanisa

Isa 66: 10-14;
Zab 66: 1-7, 16, 20;
Gal 6: 14-18;
Lk 10: 1-12, 17-20.

WAFANYAKAZI WA AMANI!

“Mavuno ni mengi lakini wafanyakazi ni wachache.” Hakika usemi huu wa Yesu ulionekana wazi wazi katika jumuiya ndogo ya wakristo wa Kwanza. Wakati huo, Kanisa lilikuwa kama mbegu ndogo ya haradali iliofunikwa kwenye kipande kikubwa cha ardhi. Leo hii duniani kuna Wakristo zaidi ya billioni moja. Kwakweli wafanyakazi wa mwanzo hawakufanya kazi bure. Mbegu ya haradali imekuwa na kuwa mti mkubwa kwaajili ya makao ya watu maelfu. Chachu ndogo ya Amira imafanya unga wote ukaumuka. Kwakuiweka vizuri zaidi ni kwamba, nne kati ya tano hawajaupokea ujumbe wa Kristo bado

Kati ya mabilioni haya ni wangapi wanaweza kuwa wafanyakazi hodari katika Shamba la Bwana? Kwani mavuno bado ni mengi na kwa ujumla “wafanyakazi” tunadhani ni mapadre au mabruda au masister, ndio “walioitwa”. Lakini, nina mashaka kwamba Yesu alikuwa aikiwafikiria Mapare au watawa wakati akiongea maneno haya. Katika hali ya kweli, kipindi cha mwanzoni mwa Agano la Jipya hakukuwa na mapadre au masister kama tunavyoelewa siku hizi. Katika akili ya Yesu na pia kwa wahubiri wa kwanza- kila mmoja aliyejulikana kama mfuasi wa Yesu alijulikana kuwa mfanyakazi katika shamba la Bwana. Mfano, Mt. Paulo, alikuwa mtume, na muhubiri maarufu lakini hakuwa Askofu wala Padre. Sisi tunadhani kufanya kazi katika shamba la Bwana ni lazima uwe Padre au mtawa.

Kuwa Mkristo sio mwisho. Bali ni muda muafaka, wakuamini, njia iliyo sahihi zaidi ya kuwa viumbe vipya ambao Yesu na Paulo waliongelea. Kuwa watu wapya inamaana kuzama ndani ya Mungu aliye ukweli wa yote na mweza wa yote, Mungu anayetuita kila siku zaidi ya sehemu tuliopo na ambaye, kwa wakati huo anaingia ndani kabisa ya nafsi zetu na yote tunayofanya. Mtu huyu mpya huishi maisha ya utu na ukweli, maisha ya huruma ya kweli na kujali. Mtu huyu huishi katika uhuru wa kweli na Amani. Neno moja ambalo linatokea katika masomo yote matatu leo ni “Amani”. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anasema Mungu “atatuelekezea Amani kama mto”. Paulo anaongelea kuhusu Amani na rehema itakayokuja kwa wote walio viumbe vipya ndani ya Kristo. Na katika Injili, Yesu anawaambia wafuasi wake walete Amani kila watakapo ingia. Amani hii sio tegemezi kwa mambo ya nje. Inaweza ikawapo hata kukiwa na machafungo. Ni Amani aliopata Yesu baada ya sala yake bustanini. Ni Amani ambayo Paulo aliipata, kwa “kushiriki msalaba wa Kristo” na kubeba alama za majeraha na mateso ya Yesu katika mwili mwake.

Kwahiyo kazi yetu kama Wakristo ni kuleta Amani. Na zaidi ya yote, tunahitaji Amani na usalama ndani ya roho zetu kabla ya vyote. Ni Amani ambayo mfuasi wa Karibu wa Yesu anaweza kuileta. Tunaitwa leo na Yesu kuwa wafanyakazi pamoja na Yesu katika shamba lake ambalo ni jamii zetu tunamoishi. Pengine ni jamii inayo onekana kuwa na mafanikio ya nje na watu wanasitawi lakini kwa bahati mbaya ni jamii iliyokosa Amani na iliyo maskini kiroho na yenye utapia mlo wa kiroho. Tunaitwa leo tuwe wafanyakazi ili jamii zetu zibadilike na thamani ya Injili ambayo inajulikana kidogo sana hata kwetu iweze kuonekana. Tuwaombee wale wote walioitwa kwa namna ya pekee kulitumikia kundi la Mungu. Baba Mtakatifu wetu Fransisko, Maaskofu wote, Mapadre, Mashemasi, Watawa, Walei wote, ili Mungu awajaliye neema yakutimiza majukumu yao yakumtangaza Kristo kwa watu wote. Pia kwa namna ya Pekee, tuwaombee wale watakao pewa daraja la upadre wiki hii, Jimbo la Moshi na leo hii katika jimbo la Zanzibar Mungu awabariki siku zote na awajaliye hekima itakayo kaa nao na kufanya kazi ndani yao. Mungu awe nao daima.

Sala: Bwana! Tusaidie tuwe wajumbe wa Amani yako duniani. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni