Alhamisi, Julai 09, 2020
Alhamisi, Julai 9, 2020,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Hos 11:1-4, 8-9;
Zab 79:2-3, 15-16;
Mt 10:7-15
UWEZO KATIKA UTUME!
Ndugu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo linaanza kwa kuliangalia somo letu la kwanza ambapo tunakutana na nabii Hosea akiwakumbushia wana wa Israeli juu ya upendo Mungu alionao juu yao.
Anawakumbushia jinsi alivyowaokoa utumwani Misri, alivyokaa nao akiwafundisha, alivyowachukua mikononi mwake akiwa kule jangwani, na jinsi alivyoshiriki kwenye kuwaponya. Anawakumbushia jinsi alivyoandika chakula mbele yao tayari kule jangwani wakala wakashiba. Hivyo, anakumbushia kwamba kamwe hataweza kumwacha Efraimu na huruma zake zitawaka juu yake tu. Zaburi ya wimbo wa katikati inakumbukia jinsi huruma hizi toka kwa Mungu, jinsi zilivyokuu na hivyo mzaburi anamwambia Mungu kamwe asiache kuwaonesha huruma hizi, aendelee kuuangaza uso wake juu yao ili basi nao wapate kuokoka.
Hapa tunapata somo muhimu kwetu sisi ndugu zangu. Nasi tunalo jukumu la kuikimbilia huruma ya Mungu. Tupatwapo na shida au kila tutendapo kosa, tukumbuke kwamba kuna huruma ya Mungu na kweli tuipatie nafasi hii huruma ya Mungu. Hili ni jambo la muhimu sana. Lakini pia changamoto inayojitokeza ni uwezekano wa kuichezea huruma ya Mungu. Kuiona huruma ya Mungu kama udhaifu wa Mungu, kuona kwamba pale Mungu anapozidisha huruma yake kwa kuamua kukaa kimya bila kutuadhibu, sisi hufikiria kwamba Mungu ameshindwa au Mungu hana nguvu na wengine tunaishia kusema kwamba Mungu hayupo. Hili ni tukano kubwa sana kwa Mungu. tutambue kwamba huruma ya Mungu ndiyo inayoiifadhi dunia, inayoifanya iendelee kuwako hadi leo. Mungu angekuwa na hasira za kujibu kila dhambi, nakueleza kweli duniani kusingekuwa na binadamu. Wote tunaishi kwa sababu ya huruma ya Mungu. Wezi na mafisadi wameweza kuendelea kupumua kwa sababu ya huruma ya Mungu inayowataka wabadilike na kweli kama Mungu angejibu mapigo yao, wangalikwishaangamia mara moja.
Basi tujifunze kuitumia vyema huruma ya Mungu, kila tutendapo dhambi, tuungame na kumwomba toba kweli. Tusiichezee na kuiona kama udhaifu wa Mungu au kama kiashirio cha kutokuwepo kwa Mungu. Kila mwenye dhambi aungame na ajue kwamba ni huruma ya Mungu imemwezesha kuendelea kuishi.
Katika injili, tunakutana na Yesu akiwapatia mitume maagizo ya namna ya kulihubiri neno la Bwana. Anawaambia kwamba washike njia sahihi kwenye kulihubiri neno hili, wafanye kazi hii kiaminifu na wanaambiwa kwamba endapo kama hawatapokelewa na mji fulani, basi wakungute mavumbi yao miguuni kama ishara kwao. Ndivyo inavyoelezewa. Lakini hadi tufikie hatua ya kukunguta mavumbi, inatubidi tuwe tumekwisha onesha jitihada za kutosha na kukataliwa na wenzetu.
Lakini shida ya nyakati zetu ni kwamba baadhi yetu tunatumia sehemu hii ya injili vibaya-kitu kidogo tu mtu unatishia watu kwa kukunguta mavumbi. Jamani, mambo yasiwe maraisi hivi. Usikungute mavumbi kabla ya wewe kutumia jitihada za kutosha hali ukikataliwa. Basi tuombe neema ya kuwa wavumilivu na tusitumie sehemu hii vibaya. Kama ni mzazi, si kila mara utumie sehemu hii ya injili kwa mtoto wako. Ongeza jitihada zaidi kwenye kumfunda mtoto wako kuliko kila siku kukunguta mavumbi.
Maoni
Ingia utoe maoni