Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 08, 2020

Jumatano, Julai, 8, 2020,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. benedikto Abati

Hos 10: 1-3, 7-8, 12;
Zab 104: 2-7;
Mt 10: 1-7


KUWA MMISIONARI!

Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunamkuta mzaburi akisisitizia kwamba ni lazima tumtafute Bwana, tuweze kuuona ukuu wake na kukumbana na kuutafakari utakatifu wake kila wakati. Hii ndiyo namna mojawapo ya kuutambua ukuu wa Mungu na kufuata mausia yake.
Zaburi hii inatumika kwenye kukolezea ujumbe wa nabii Hosea katika somo la kwanza. Hapa nabii anawaeleza wana wa Israeli kwamba wakati wa kumtafuta Bwana kwao ndio umewadia. Wajue kwamba walikuwa wameendekeza kila aina ya dhambi, na Bwana akawaadhibu tena kwa ukali mkuu sana. Wakajikuta wanakazana kwenye kufanya mambo fulani fulani lakini wakawa hawafanikiwagi, wanajikuta wanalima lakini hawavuni, yote haya chanzo chake ni kutokumtambua Mwenyezi Mungu na kuukiri ukuu wake. Sasa, anawaeleza leo kwamba yote haya yatabadilika ile siku watakapomgeukia Bwana na kuutafuta uso wake na kumwelekea Bwana.
Hili ni fundisho kubwa kwetu sisi. Nasi kama hawa, tumeamua kujitafutia njia zetu na namna ya kuishi. Tumeamua kujichimbia visima vyetu; tukakumbatia uasherati, na madhulumu, na uonevu. Na kwa sababu hiyo tukaishia kwenye kuwa watu wa mwisho na waliorudi nyuma sana. Lakini ile siku tutakapomtafuta Bwana, na kutamani maongozi yake, hiyo siku ndio mambo yatakapobadilika na kuwa mapya kabisa. Basi tumtafute Bwana. Najua wengi kati yetu tuna dhambi zetu na matatizo yetu lakini yafaa tumgeukie Bwana na tusiendekeze zaidi mambo yahusuyo ugomvi au fujo au dhuluma kati yetu. Hapa tutaweza kubadilika na kuwa viumbe vipya.
Katika injili, tunaambiwa kwamba Yesu aliwachagua wale mitume kumi na wawili na kuwapa uwezo juu ya magonjwa yote, pepo wote na udhaifu wa kila aina. Hii yamaanisha kwamba wale mitume walikuwako ili wenyeji waishi, wafurahie, watu wafarijike, walikuwa kwa ajili ya manufaaa ya wengine. Nasi tutambue kwamba sisi tupo kwa ajili ya manufaa ya wengine. Ebu tujiulize, je?, tunasaidiaga wengine, ni wagonjwa wangapi wamewahi kuja na kupata pumziko chini yangu? Nikionaga wagonjwa huwa naenda kuwasaidia?, je, ni wenye pepo wangapi huwa nimewezaga kuwasaidia? Jamani, tufanye bidii zaidi. Bado hatujaweza kutumia vipawa vyetu vyema. Tukazane sana tuweze kutimiza wajibu zetu kisawasawa.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni