Jumatatu, Julai 06, 2020
Jumatatu, Julai, 6, 2020,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Hos 2: 16-18, 21-22;
Zab 144: 2-9;
Mt 9: 18-26
UPONYAJI WA IMANI!
Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na ujumbe wa matumaini toka kwa Nabii Hosea: ambapo Mungu anachukua jukumu na kumfikia Israel ili kumpatia matumaini tena.
Israeli alikuwa ameanguka dhambini na alikuwa amekwisha onja taabu na kipigo kikali. Lakini sasa basi Mungu anajitokeza tena, anaamua kumchukua pembeni, mahali pa faragha na kubonga naye na kwa namna hii ataweza tena kumshawishi aache dhambi na kumrudia Mungu. Kweli hili ni tendo la kiupendo kwani ni Mungu mwenyewe anaamua kumwomba Israeli, anamwambia jamani acha dhambi jamani akitegemea kwamba itafikia mahali auchukie uovu tena.
Hapa twajipatia kitu muhimu cha kujifunza ndugu zangu. Wakati mwingine tuwe tayari kuwafuata watu, kuwapeleka pembeni na kuwashauri katika jambo fulani. Nakuambia utakapompeleka mtu pembeni au faragha hakika itakuwa vigumu kuacha kukusikiliza. Wengi tuna ile tabia ya kukosoa watu hadharani kwa nia ya wao kuchekwa na wengine. Hili sio jambo jema. Hapa unaamsha hasira na vionjo vibaya vya watu. Unawataka watu waaibike na hamtaelewana. Hivyo, leo tujifunze na kuthamini mfumo wa kuwapeleka watu pembeni ili tuwaeleze jambo fulani na kusahishana kiamani. Namna hii hudumisha amani na kutufanya tuelewane zaidi na zaidi. Hivyo basi kama tuliwahi kuwatangaza watu hadharani na kushindwa kuelewana basi tubadilike.
Katika somo la injili, Yesu anamponya Mama aliyekuwa akitokwa na damu kwa miaka mingi ajabu. Mama huyu alionesha ujasiri wa kiimani, hakuogopa macho ya watu waliokuwa wakimwangalia bali alikwenda na kumgusa Yesu kwa imani na kupona. Mama huyu aliyajua maumivu yake yeye mwenyewe tu, hakuna mtu kati ya ule umati aliyekuwa akijihusisha naye, akitambua kwamba anaumwa au la. Ni yeye aliyatambua haya na hivyo alichukua jukumu.
Nasi ndugu zangu tuwe kama huyu mama. Ni lazima tuchukue jukumu, tukamguse Yesu. Kila mtu anamatatizo na changamoto zake. Kuwa kama huyu mama. Kuwa wa kwanza kuchukua jukumu, acha kulala. Ukilala utaishia kuteseka tu. Ajuaye mateso unayoyapata, au ugumu unaoupitia ni wewe ndugu zangu. Unaweza kuwa na mwenzi lakini asiyatambue magumu unayopitia. Hivyo, kuwa wa kwanza kuonesha njia, mwite Yesu, mwambie Ee Yesu naangamia na ninakuomba usiniache kabisa kwani mimi ni wako jamani na kabisa usiniache.
Maoni
Ingia utoe maoni