Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Julai 07, 2020

Jumanne, Julai, 7, 2020,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa


Hos 8: 4-7, 11-13;
Zab 115: 3-10;
Mt 9: 32-38


WATETEA IMANI!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linaanza kwa kuitafakari zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunamkuta mzaburi akimsisitizia Israeli kwamba amtumainie Bwana. Aachane na miungu mingine ya masanamu kwani miungu hii ni fedha na dhahabu tu na na endapo wataitegemea, wataishia kutokuvuna chochote kwao.
Maneno haya ya zaburi yanatumika kwenye kusisitizia kile kinachozungumziwa katika somo la kwanza ambapo Mwenyezi Mungu kupitia kinywa cha nabii Hosea anamweleza Israeli kwamba aachane na sanamu. Na chanzo cha hili ni pale walipojichagulia wafalme ambao walikuwa hawajaridhiwa na Bwana. Hawa waliwaongoza kwenye uabudu sanamu na kwenye sanamu hizi walizidisha uovu wa kila aina, kila dhambi ilikuwa ndio kitalu chake hapa. Uasherati, mauaji, unyonyaji yote haya chanzo chake kilianzia hapa.
Hili ni fundisho kwetu ndugu zangu. Kweli hata sisi nyakati hizi tumekumbwa na dhambi kama hizi za uabudu sanamu. Siku hizi sanamu zetu ni simu za mkononi. Tunatumia muda mwingi kwenye simu kuliko sehemu nyigine yoyote. Siku hizi kama tunataka kusafiri, hatuangalii tena kama tumebeba vitu kama rozari, cha kwanza ni simu yangu iko wapi tukidhania kwamba tukishakuwa na simu, basi ndio mwisho wa matatizo, yaani shida zote za njiani ndio nimeshatatua. Hili sio kweli ndugu zangu. Sidhani simu kama ndio mtatuzi wa kila kitu chetu tukiwa safarini. Hakikisha unabeba na rozari na uiweke na kuishikashika Zaidi kuliko unavyoshika simu yako. Hapa utaweza kusema kwamba simu yako sio Mungu wako.
Kingine ni tutambue kwamba mara nyingi viongozi wasiomcha Mungu ndio sababu ya maovu mengi tunayoyaona. Hawa huwakwaza watu na kuwafundisha tabia mbaya na mwishowe tunaishia kwenye kumsahau Mungu. Tutambue kwamba kuna baadhi ya viongozi wameishia kutetea na kupigania vitu kama utoaji wa mimba uruhusiwe nchini mwao, au ushoga au uuaji wa watu fulani fulani ufanyike tu. Wapo viongozi wa namna hii walioruhusu hili nchini mwao. Hawa wamekuwa sababu za taifa kuishia kwenye madhambi ya ajabu. Jamani, tuache kujidumbukiza kwenye dhambi namna hii.
Katika injii, Yesu anatuambia kwamba mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache na hivyo tumwombe Bwana wa mavuno atume watenda kazi. Tuombe pia miongoni mwa watenda kazi hawa, kati yao basi wawe ni viongozi bora wa kisiasa, viogozi watakaoweza kututunza vyema, kutufanya tusidumbukie kwenye uovu, watulishe dozi njema, watufanyie mambo mazuri na si watudumbukize kwenye utoaji mimba au kuruhusu mauaji yatendeke kiholela. Viongozi wema pia wanahitajika ndani ya hili shamba la Bwana. Hata kwenye siasa kunahitaji kumwomba Mwenyezi Mungu atupelekee viongozi bora pia.

Maoni


Ingia utoe maoni