Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Julai 03, 2020

Ijumaa, Julai 3, 2020.
Juma la 13 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mt. Tomasi Mtume.

Ef 2: 19-22;
Zab 116: 1-2;
Yn 20: 24-29.

KUTOA USHUHUDA KWA YESU MFUFUKA!

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo tunaadhimisha sikukuu ya Tomasi Mtume. Leo tafakari ya neno la Bwana inaanza kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wetu wa katikati. Hapa tunakutana na zaburi ya furaha; mzaburi anamshangilia Mungu na kumtukuza kutokana na upendo wake mkuu kwake na matendo makuu ya Mungu aliyoyaonyesha machoni pa mataifa.

Hii shukrani na furaha ya mzaburi inatumika kuelezea furaha aliyoipata mtume Tomasi baada ya kumwona Yesu amefufuka toka wafu. Mtume huyu alionja pendo la Yesu jinsi lilivyo: pendo lililodhihirishwa na makovu ya misumari mikononi na alama ya mkuki kwenye ubavu wa Yesu. Yeye alitaka pia kukiweka kidole chake kwenye makovu haya na lengo lake lilikuwa ni kumdhihirisha Yesu wa kweli: kwake yeye-Yesu wa kweli ni yule mwenye yale makovu, yule aliyeteseka kwa ajili yake. Huyu ndiye atakayemsadiki na kumwita kuwa Bwana wake na Mungu wake. Makovu ya Yesu yalikuwa ishara ya pekee kwake: ishara ya uwepo wa Yesu mwenyewe, ishara ya upendo na Umungu wake. Huyu ndiye Tomasi wetu.

Nasi ndugu zangu kama Tomasi tunaalikwa kuona ukuu wa makovu ya Yesu, hii ni ishara ya upendo wa Yesu kwetu-na ishara ya Umasiha wake. Hivyo tuyaheshimu madonda haya. Yatufundishe na sisi tuwe na utayari wa kukubali kuwa na majeraha kwa ajili ya wengine. Mfano, mama aliyezaa kwa operation-jeraha lake huwa ishara ya upendo kwa mtoto wake na kila akiyaangalia majeraha haya, yeye huwa sababu ya kufurahi na kushangilia kwani majeraha haya humkumbushia historia nzuri ya jinsi alivyoteseka kwa ajili ya wengine. Au dereva aliyepata majeraha kwa sababu ya kukazana ili kuwaokoa abiria wake, lile jeraha huwa sababu ya ushindi kwake akiwakumbushia watu jinsi alivyojitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Hata mwizi-majeraha yake huweza kuwa sababu ya mabadiliko-anaweza kuyaangalia majeraha yake na kusema-jamani-yabidi nibadilike, nisibakie hivi, majeraha yaweza kumkumbushia maumivu yake yote na hivyo yakamfanya abadilike vizuri sana. Hii ndiyo thamani ya majeraha. Kila mtu leo basi namwalika auchunguze mwili wake. aangalie majeraha yalipo ndani yake na avune kitu chema toka ndani ya majeraha hayo.

Katika somo la kwanza, Paulo anawaambia wakristo wa Efeso kwamba wao ni rafiki, watu wa nyumbani kwake Mungu, waliojengwa kwenye msingi wa watakatifu na Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Sisi ndio hawa watu wa karibu namna hii ndugu zangu. Watu tuliojengwa chini ya huu msingi mtakatifu. Hivyo basi naomba tutambue cheo chetu hiki na tuwe wakristo hai. Zaidi naomba pia tusiache kutambua umuhimu wa majeraha yetu sisi-hasa yaliyomo ndani ya mwili wetu. Yaweza kuwa sababu za kutufanya tubadilike vyema.

Maoni


Ingia utoe maoni