Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Julai 02, 2020

Alhamisi, Julai 2, 2020,
Juma la 13 la Mwaka wa Kanisa

Amo 7: 10-17;
Zab 18: 8-11;
Mt 9: 1-8

NINI MAANA YA UKWELI?

Ndugu zangu wapendwa, karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu. Neno la Bwana leo tafakari yake tuanze kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha nabii Amosi. Hapa tunakutana na nabii akifanyiwa hila na kuhani mmoja aliyeitwa Amaziah. Kuhani huyu alikuwa kibaraka wa mfalme Jeroboamu. Yeye kwa maisha yake yote alikuwa na lengo la kumpamba mfalme Jeroboam. Mfalme huyu alifanya uovu lakini kuhani huyu hakumweleza uovu wake, kuhani huyu alilinda maslahi yake, kuhakikisha kwamba anapata kipato cha kutosha toka kwenye madhabahu yake. Hivyo, alipambana sana na nabii Amosi kwani Amosi alikuwa nabii wa kweli aliyemkosoa mfalme Jeroboamu. Alionekana kuwa tishio kwa ufalme wake na maisha ya huyu kuhani Amaziah. Hivyo anamuonya leo Amosi anafukuzwa hadharani na Amaziah na kuambiwa kwamba asionekane kabisa kwenye miji ya Israeli akitabiri. Pale wanahitajika wengine, wanao-mpamba mfalme kama yeye. Amosi anakasirishwa na hili na kutoa unabii wa laana kwa huyu Amaziah.

Ndugu zangu, Amazia alifanya unabii wa kimaslahi. Hivyo alichunga sana kile alichoongea mdomoni, alichagua maneno ya kuongea na yatakayomfurahisha mfalme. Kwa kufanya hivi, mfalme Jeroboamu alizidi kutenda dhambi, na hakuna aliyemrekebisha, hivyo aliishia kuudumbukiza ufalme kwenye dhambi nyingi zaidi. Kilichotokea kwa mfalme huyu ndicho kitakachotokea kwetu sisi endapo kama nasi tutakuwa tayari kutupa ahadi yetu ya unabii kwa kutetea maslahi yetu. mfano, kama mzazi ataogopa kumwambia ukweli mtoto wake kwa hofu kwamba mtoto huyu atakasirika na hivyo kumnyima mahitaji yake-mtoto huyu ataishia kuharibika na mwishowe mtoto huyu atakuwa wa ajabu hata kwa mzazi mwenyewe na hivyo atapata hasara Zaidi.

Au mwalimu anapoogopa kumwambia mwanafunzi ukweli lengo likiwa ni kulinda urafiki, ama kweli ataishia kumharibu huyo mwanafunzi. Mwanafunzi ataishia kuwa na tabia mbaya, atashindwa kutambua wajibu wake na ataishia kuwa na tabia kama za kiudanganyifu kwenye mitihani na hivyo mwanafunzi yule atakuwa hovyo kwa jamii. Atailetea maporomoko zaidi. Lakini mwalimu au mzazi anayesema ukweli, anayemkosoa mtoto au mwanfunzi wake, mwanzoni tunaweza kuwachukia, kuwaita wanoko, kuwatungia majina mbalimbali lakini nakwambia mwishowe huwa tunaishiaga kuwakumbuka na kusema ama kweli huyu ndiye aliyetufundisha na kutusaidia kimaisha. Sifa unakuja kuipata mwishoni. Hata watu wa Israeli walikuja kumkumbuka Amosi mwishoni na kuanza kumlaumu Amaziah.

Hivyo ni fundisho kwetu sisi. Tujifunze kuona ubora wa wale wanaotuambia ukweli, halafu wale wanaosemaga semaga uongo tu, wakitupepea pepea tu lazima tujifunze namna ya kuona ndani yao uovu au ubaya utakaotupata mbeleni. Mara nyingi watoto waliolelewa na mzazi mkali-japokuwa humchukia mwanzoni lakini mwishowe huishia kumshukuru mzazi wao. Nasi ndugu zangu tuwe watu wa kusema ukweli, tusiwe wa kupuliza na kusawazisha sawazisha tu. Watu wa namna hii wameipotosha na kuiletea jamii madhara makubwa. Sehemu nyingi zina shida kutokana na tabia za namna hii. Tabia za kifisadi na udokozi zilianza kutokana na watu kutokuambiana ukweli. Watu wengi wamenyimwa haki kutokana na sisi kushindwa kuambiana ukweli na kutoa ushahidi wa uongo. Tuache tabia kama hizi ili kisije kikatupata kilichompata mfalme Jeroboamu na Amazia na jamii yote ya watu wa Israeli waliongozwa na Jeroboam na kumfuata Amaziah.

Katika somo la injili leo, Yesu anamponya mgonjwa mmoja aliyekuwa amekumbwa na ugonjwa wa kuparalyze. Yeye anamponya. Lakini cha ajabu kuna baadhi ya watu hawaoni hili kama jambo la kiupendo, wao mara moja hawafurahii kile kinachofanywa na Yesu bali wanaishia kwenye kutafuta makandokando, kwenye kuangalia Yesu amesema nini wakati wa kumponya. Kwangu mimi nashangaa-ilikuwaje hawa watu wakashindwa kuona huu uponyaji na kuishia kutafuta tu makosa ya Yesu? Yaani hawakufurahi kuona kwamba mtu aliyekuwa mgonjwa, hajiwezi lakini sasa ndio kaweza kuongea-hawakufurahishwa naye bali waliishia kutafuta makosa kwenye alichosema Yesu? Daah! Jamani-tuache kuwindana namna hii.

Wakati mwingine wenzetu unakuta wametenda matendo mema lakini tukaishia kushindwa kuona wema wao tukaishia kujikumbushia chuki tuliyonayo juu yao. Ama kweli chuki ni adui wa ukweli, mwenye chuki juu ya mwenzake hataweza kuona jambo jema linalotendwa naye. Lakini kama mtu unampenda utaona wema. Wengi tumeishia kushikilia jambo la uongo kwa sababu ukweli unashikiliwa na yule tunayemchukia. Hivyo, tukaona afadhali kushikilia jambo la uongo kuliko kuushikilia ukweli kwani kuushika ukweli ni kuungana na adui yetu na hivi ndivyo wote tulioishia kwenye upotoshaji. Tuondoe chuki kati yetu.
Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni