Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 01, 2020

Jumatano, Julai 1, 2020.
Juma la 13 la Mwaka wa Kanisa

Amo 5:14-15.21-24;
Zab 50:7-13.16-17;
Mt 8: 28-34

UTUOPOE MAOVUNI!

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la misa Takatifu. Leo tafakari yetu ya neno la Mungu itaanza kwa kuiangalia zaburi ya wimbo wetu wa katikati. Mzaburi anasisitiza kwamba ataonyesha wokovu wake kwa wale walio wanyofu wa moyo. Yeye sio kwamba anaangalia sana juu ya ngombe au vitu mtu anavyotoa kwa ajili yake. Yeye huangalia moyo wa mtu, huruma yake, jinsi anavyojali maskini, jinsi alivyomnyenyekevu. Hiki ndicho kinachompendezesha Mungu.
Ujumbe wa zaburi hii unatumika kwenye kutilia mkazo kile kinachosemwa kwenye somo la kwanza na nabii Amosi. Yeye anawaeleza wana wa Israeli hasa wale walio na uwezo waliojitahidi kutoa sadaka nyingi mbele ya watu lakini walikuwa wanadhulumu. Yeye anasema kwamba sadaka za namna hii huwa hazimpendezi. Hivyo, anasisitiza kwamba ni lazima wabadilishe mioyo yao, wawe wanyofu na ndio atawapatia wokovu.

Hiki anachokisema nabii leo bado kina umuhimu wake hasa kwa nyakati zetu. Sisi unakuta tunakazania kupata pesa, hata kuwa mafisadi ili tupate pesa, halafu tunakuja kanisani tunachangia michango mingi, tunasifiwa, tunapewa rozari, tunabarikiwa nyumba zetu, tunajiona kana kwamba kama ukiiba halafu ukaja kutoa baadhi ya ile fedha kanisani, na bahati nzuri tukasifiwa na mapadre na waamini, basi dhambi zetu zinasahaulika. Hili sio kweli ndugu zangu. Tusivimbishwe kichwa na huku kusifiwa na waamini na maporoko na kusahau dhambi zetu. Mungu apenda tubadilike, na tuwe wanyofu wa moyo. Tukiiba turudishe tulivyoiiba na sio kufikiri kwamba kwa kuvitoa msaada, basi dhambi hii hufutwa.

Somo hili pia latuhusu hasa sisi tunaosifiwaga, sifiwaga sana kwa baadhi ya mambo, labda kwa ujuzi fulani, au kipaji. Mara nyingi sifa hizi zinatufanya tubweteke na kusahau uovu wetu. Hivyo, kwa kila sifa tuipokeayo, iangalie na uichunguze jinsi ilivyoweza kukufanya wewe kuusahau uovu wako.

Kwenye somo la injili, tunamkuta Yesu akiwafukuza pepo waliokuwa ndani ya watu wawili na kuruhusu wale pepo wawaingie nguruwe. Hapa Yesu anaonesha kwamba mwanadamu ni bora kuliko nguruwe. Lakini kwa wale watu wa lile eneo walishtushwa na kukasirika kwa kitendo cha Yesu kusababisha kuangamia kwa nguruwe wao kwani waliishia kumwomba Yesu aondoke mjini kwao. Wao waliona nguruwe kuwa bora kuliko afya za wale watu.

Hivi sisi ndivyo tulivyo; wengi kati yetu. Una mtu ambaye ukikwangua gari yake-labda Mercedes benz-atakupiga risasi. Au, hapa si tunafanya kama hawa watu waliomwambia Yesu aondoke? Si tunaona mali kuwa muhimu kulio binadamu? Na nikuambie, mtu ukiwa mgonjwa, ukiwa unatumia matumizi makubwa kuliko mapato-halooo!-watu-hata baaadhi ya ndugu zako watakuombea ufe-kwani wanaona kwamba unawaingizia hasara. Ndivyo maisha yalivyo ndugu zangu. Lakini sisi tusichoke kuwa na upendo. Kwa waliowahi kukumbwa na tukio kama hili, basi poleni sana. Zidini kumtumainia Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni