Jumamosi, Juni 27, 2020
Jumamosi, Juni, 27, 2020,
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa
Omb 2: 2, 10-14, 18-19;
Zab 74: 1-7, 20-21;
Mt 8: 5-17
KILIO CHA SALA!!
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuuangalia wimbo wa katikati ambapo tunakutana na zaburi ya maombolezo na mzaburi analia akimuomba Mungu asiwatupe, awaangalie jamani kwa sababu wamevamiwa na mataifa ya kipagani yaliyowadhalilisha na kuubomoa mji wao na hekalu lao na kupandisha bendera zao za kipagani kwenye miji yao kuonesha kwamba sasa wanatawaliwa na taifa la kipagani. Mzaburi anakasirika sana na hili jambo na anamuomba Mungu afanye kitu asikubali waendelee kudhalilishwa hivyo. Mzaburi anakumbukia jinsi hawa wapagani walivyoshambulia na kulikufuru hekalu lao, jinsi walivyochoma patakatifu na kuua watu kwa kuwatupa kama takataka kwenye barabara na miili yao kuliwa na ndege-kweli kilimsikitisha sana huyu mzaburi na hivyo anamwomba Mungu na kumwambia kwamba kamwe asiwaache waendelee kudhalilishwa hivi.
Hili linalozungumziwa na mzaburi tunaliona kwenye somo la kwanza ambapo mwandishi wa kitabu cha Maombolezo, yule aliyekuwa amebaki na kushuhudia udhalilishaji wote waliotendewa, sasa yeye anasimama na kuandika maombolezo yake kwa Mungu. Anaandika jinsi alivyowaona wazee, na watoto na wale mabinti wakiwa katika huzuni ndani ya ule mji ambao mwanzoni ulikuwa ukishamiri uhai na kupendeza. Anaandika jinsi moyo wake ulivyouma alivyowaona watoto vichanga vikianguka kwa majeraha na kwa kukosa chakula. Hivyo, mwandishi anawaambia watu ya kwamba jamani tumlilie Mungu, tusimwache, tumwombe ili aje kwetu atuondolee hii aibu.
Somo hili laelezea hali halisi tunayoiona sasa hasa kwa Afrika yetu ya vita. Ukiangalia Sudani ya Kusini, Kongo na Somalia haya ndiyo yanayotokea. Wazee wanakimbia hali wamebeba magodoro yao na kukimbia kama watoto. Nchi ilikuwa yao, wameijenga miaka na miaka na sasa vinatokea vivijana vinagombania madaraka na kuwafanya wazee wateseke hivyo. Utaona jinsi watoto hasa kule Sudan ya Kusini na Somalia wakizimia kwa njaa, hawana chakula, mbavu zimetoka kwa utapiamlo, na nzi na kipindupindu kinawaumiza. Wanalia wapewe chakula hakuna.
Na kwa bahati mbaya sisi baadhi ya Waafrika hatuna tabia ya kuchangia wenzetu. Utashangaa watoto wanangangania kunyonya toka kwa mama ambaye naye anakufa njaa-atapata wapi maziwa jamani? Ebu tuone huruma ndugu zangu. Tuache kugombania madaraka kiasi cha kuteketeza roho za watu. Ebu fikiria kilio cha hawa watoto na wazeee? Yaani sisi vijana badala ya kuwalipa fadhili kwa kututunzia nchi sasa tunawaletea vita? Ebu fikiria hawa watoto mateso tunayowapa? Angalieni wale watoto waliokonda hadi mbavu kutoka-tunawatendea haki? Jamani tubadilike. Tuache tamaa na uroho wa madaraka. Hii ianze na sisi na ianze leo.
Katika somo la injili tunakutana na Yesu akiisifu Imani ya akida mmoja ambaye hakuwa Myahudi lakini alionesha imani kubwa kwa Yesu kuliko hata Wayahudi wenyewe na Yesu alifurahishwa sana na kusema kwamba hakika watatoka watu toka mashariki na magharibi na kuuingia ufalme wa Mungu lakini wale waliokuwa wanajivuna na kufikiri kwamba ufalme wa mbinguni ni wa kwao wataishia kuukosa. Sisi ndugu zangu tuingie hili kundi la hawa akida. Tusikubali kujitambulisha na lile kundi la wanajiona kwamba hawahitaji tabibu. Tujione kuwa wenye njaa na hivyo tumlilie Mungu aje kwetu. Aje kwetu atutie imani, tulie kama yule mwandishi anayeomboleza kwenye somo la kwanza-nasi tuomboleze kwa sababu ya dhambi zetu, kwa ajili ya vichanga vinavyotolewa mimba kila siku, kwa ajili ya watoto na akina mama wanaouawa kwa sababu ya vita, kwa ajili ya wakimbizi wanaokosa kusoma na kuishia kuteseka tu. Haya yawe ndio maombolezo yetu jamani.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni