Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Juni 23, 2020

Jumanne, Juni, 23, 2020
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa

2 Fal 19: 9-11, 14-21, 31-36;
Zab 48: 2-4, 10-11;
Mt 7: 6, 12-14.

NJIA NYEMBAMBA!

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Bwana siku ya leo. Leo tafakari yetu itaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Ni zaburi inayoutukuza mji wa Yerusalem kama makao matakatifu ya Mungu na ambamo Mungu ameweka hekalu lake. Huu mji ni ishara ya makao ya Mungu Duniani, mahali alipopachagua Mungu ili aabudiwe hapo. Waisraeli walipaswa kusafiri kuujia mji huu ili kukutana na Mungu. Mungu aliahidi ulinzi wake wa pekee kwa huu mji. Kama wana wa Israeli wangekuwa waaminifu kwa Mungu, basi Mungu aliahidi kuulinda mji huu milele na kuufanya kikao chake na kamwe hangekubali kuruhusu adui yeyote aingie Yerusalem na kuja kuukalia mji huu.

Katika somo la kwanza, tunaona ukweli wa jambo hili kwamba Mungu aliupenda mji huu wa Yerusalem kwa namna ya ajabu. Mfalme wa Waasiria(Waashuru) kama tulivyoona jana katika somo la kwanza, alifanikiwa kuingia Israeli ya kaskazini na kuwachukua mateka watu wake. Sasa, leo kwenye somo la kwanza anataka tena kuingia kwenye mji mkuu wa wana wa Yuda, yaani Yerusalem na anategemea kwamba atawateka na kuwapeleka utumwani kama alivyofanya kwa Israeli ya kaskazini. Mfalme Hezekiah anamlilia Mungu na Mungu anamuokoa kwa namna ya ajabu. Mfalme Sunacherib alifikiri kwamba angeingia kirahisi mjini Yerusalem. Lakini Mungu anamjibu na kumwambia kwamba Yerusalem ni mji wake mkuu na mtakatifu na kamwe hataamuru mji huu uangamizwe hivi hivi. Na Mungu alionesha hili kwa kumrudisha nyuma Sunacheribu, kwa kumfukuza na kumwambia kwamba kamwe hataingia kwenye huu mji. Na kweli hakuiingia. Mungu alituma malaika aliyekwenda na kuwapiga wanajeshi wake na kuwaua na hili liliwafanya watimue mbio na hawakurudi tena. Yerusalem ni mji mtakatifu wa Mungu na Mungu aliulinda.
Lakini tukumbuke kwamba kwa kadiri wana wa Yuda walivyouheshimu mji wa Yerusalem kama mahali patakatifu na kuhakikisha kwamba ndani ya mji huu mambo matakatifu yanatendeka, Ndivyo hivyo na Mungu alivyozidi kuwapatia ulinzi na hakuna taifa lililoweza kufika kwenye mji huu na kuudhuru.

Tukiendelea kusoma kitabu hiki cha pili cha wafalme tutaona kwamba wana wa Yuda walikuja kuruhusu dhambi kutendeka ndani ya Yerusalem, kikao kitakatifu cha Bwana-dhambi kama, Uasherati, uabudu sanamu, uonevu na mauaji yalishamiri ndani ya mji huu na haya yalimkimbiza Bwana ndani ya ule mji na hivyo ukabakia bila ulinzi. Hivyo, mfalme Nebukadneza aliweza kufika na kuuangamiza na kuchoma hekalu la ule mji kwa sababu dhambi za wana wa Israeli zilimkimbiza Bwana Mungu wa Israeli.

Hapa tunalo la kujifunza ndugu zangu. Tutambue kwamba dhambi humkufuru Bwana. Hivyo, tujitahidi kuheshimu nyumba za ibada na vifaa vyote tuvitumiavyo kwa ibaada. Tuviheshimu. Kuna mazingira ambayo ukisha yaingia, hata kama umekumbwa na hasira kiasi gani au na tamaa kiasi gani, yakubidi kuzituliza. Kwa mfano, kama upo mbele ya kanisa au ndani ya kanisa na mtu akikuchokoza au kukukanyaga, jitahidi usimtukane au kumkasirikia, lile ni eneo takatifu sana-liheshimu. Au kama umevaa Rozari au umebeba Biblia au umebeba msalaba-jitahidi usioneshe hali ya kuvutwa na tamaa. Unakuta mtu anatukana matusi na huku kavaa rozari au na Biblia kashika mkononi au yupo mbele ya msalaba. Na mbaya zaidi wengine tunaweza kufanya hata uasherati/ uzinzi tukiwa tumevaa rozari au hata mbele ya matakatifu. Tusiruhusu mambo ya namna hii ndugu zangu. Mungu atatukimbia na sala zetu na zana zetu za ibada tutazikufuru. Kila tuwapo mbele ya matakatifu, tuoneshe heshima kubwa.

Katika somo la injili yetu, Yesu ametuambia kwamba tusiwape vitu vitakatifu au vya dhamani mbwa na nguruwe. Huu ni mwendelezo wa fundisho letu la somo la kwanza kwamba mambo matakatifu yazidi kuheshimiwa. Hapa twaweza kutafakari hii injili ya Yesu kana kwamba inatuambia kwamba kamwe vitu vitakatifu vipewe heshima yake. Ukivichezea chezea mwishowe utashindwa kuona utakatifu ulioko ndani yake na hivyo vitakosa maana kwako na kushindwa kukuongoza kwa Mungu. Mambo matakatifu yapewe heshima yake.
Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni