Alhamisi, Juni 25, 2020
Alhamisi, Juni, 25, 2020,
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa
2 Fal 24: 8-17;
Zab 78: 1-5, 8-9;
Mt 7: 21-29
Ee Mungu nakuomba ufanye kitu jamani, usituache.
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo, neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Hapa tunakutana na zaburi ya maombolezo ambapo mzaburi anaomboleza kuanguka kwa Yerusalem. Mzaburi anasikitika jinsi wapagani walivyovamia na kuunguza mji wa Yerusalem na kuua watu wengi sana na kuacha miili yao iliwe na ndege. Mzaburi analalamika na kuomboleza kwani wapagani wameunguza kila mahali na hakuna mahali palipobakia kwa ajili ya kutolea dhabihu, analalamika tena kwa sababu wemeondolewa mfalme, hawana tena mfalme. Analalamika tena kwa sababu wanadharauliwa na mataifa jirani, wanawacheka, wanaonekana kwamba wao si kitu. Hivyo, mzaburi anamwambia Mungu, je, haya mambo yatakuwa hivi hadi lini? Hivyo, anasema ee Mungu nakuomba ufanye kitu jamani, usituache.
Anacholalamika mzaburi huyu ndicho tunachokiona katika somo la kwanza. Kweli mfalme Nebukadneza anaingia Yerusalem, anauunguza mji ule, anaharibu hekalu, anawaondolea mfalme wao na kumpeleka utumwani na kumweka mfalme kibaraka. Anawachukua wale watu maarufu na waliokuwa na ujuzi maalum na kuwahamisha. Hivyo, lile taifa linabakia katika hali ya kudharaulika sana. Mataifa jirani kama taifa la Edomu liliwacheka sana walipoona wamepigwa kipigo kikali hivi. Hivyo, yule mzaburi aliomboleza kuomba Mungu asiwaache wabakie kwenye hali hii milele. na kweli Mungu alikuja kwao. Sala ya huyu mzaburi ilisikika masikioni mwa Mungu na alikuja kwao kuwaokoa.
Sisi nasi ndugu zangu wengi wetu tupo kama hawa wana wa Israeli. Kweli tumetenda dhambi na wengi wetu tumekwisha pokea vipigo vya maana. Tumechakaa kwa magonjwa, chuki, kusengenywa, kuchukiwa, kudharauliwa, umaskini, njaa, vyote hivi vimetupiga. Tunafanya kazi lakini mambo hayaendi. Baadhi tunajikuta tukinyanyaswa hata na vibosi vidogo tu. Au kutokana na kazi ninayofanya-inabidi nijishushe nitoe shikamoo hata kwa mtoto mdogo lengo likiwa ni yeye kumshawishi anunue kitu changu. Mfano, kina mama wanaotembezaga mboga majumbani mwa watu-inawabidi wasalimie kila mtu-hata kama ni mtoto mdogo inabidi tu amsalim lengo likiwa ni kuvutia pozi la mboga zake kununuliwa. Yote haya yanatupiga ndugu zangu.
Tunachopaswa kufanya ni kumlilia Mungu, ni kuomboleza kama mzaburi wetu anavyoomboleza leo. Tumwambie Mungu, je, mambo yatakuwa hivi hadi lini? Nitalazimika kusalimia hata vitoto vidogo hadi lini? Nitakula chakula kisicho na virutubisho muhimu hadi lini? Kweli twahitaji kumlilia Mungu naye Mungu atatuinua kama alivyojibu hii sala ya mwombolezaji wa zaburi yetu hii. Alilia akamwambia Mungu, je, haya mateso yatakuwa hadi lini? Nawewe mwambie Mungu hivyo hivyo-je, haya mateso yatakuwa hivi hadi lini? Hizi fedheha zitaendelea hivi hadi lini? Hakika atafanya kitu ndugu zangu.
Kwenye injili yetu tunamkuta Yesu akisema kwamba siyo wale wanaomuita Bwana Bwana ndio watakaoingia kwenye ufalme wa mbinguni. Ni wale tu wanaolisikia neno la Mungu na kulishika na hawa wanafananishwa na mtu ajengaye nyumba yake kwenye mwamba ambapo mvua, na mafuriko haiwezi kuifanya kitu. Tunajifunza mengi, wengi wetu tunasali sana hata pengine kuongoza sala kanisani lakini matendo yetu yapo mbali mnoo, tumejaa chuki, wivu hatakutesa labda wapangaji au wafanyakazi wetu. Na bado tunatumia dini kama sehemu ya kujifichia na kuita Bwana Bwana. Tusimpende Mungu kwakisingizio cha kumuacha jirani. Tunachosali kifanane na matendo yetu. Na huku ndiko kujenga msingi kwenye mwamba .
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni