Alhamisi, Juni 18, 2020
Alhamisi, Juni 18, 2020.
Juma la 11 la Mwaka
YbS. 48:1 – 14
Mt. 6:7-15
BABA YETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Wimbo huu unatoka katika zaburi ya 96 na kiitikio chake kinasema “furahini katika Bwana enyi wenye haki.” Haya ni maneno aliyoyasema Daudi na yeye katika maisha yake, alipata kugundua kwamba wenye haki kwa kweli wanayo kila sababu ya kufurahia na kushangilia mbele ya Bwana-wale wasiomtesa yeyote, wafuatao mausia ya Bwana, wale wanaokubali kutumia cha kwao kwa ajili ya Bwana. Daudi anasema “hawa wanayokila sababu ya kufurahia.”
Zaburi hii katika tafakari yetu ya neno la Mungu leo inamhusu moja kwa moja nabii Elia tunayemsikia katika somo la kwanza. Yoshua Bin Sira anamuelezea kama Mchamungu aliyeishi kinabii, akatabiri kwa jina la Bwana, akaweza kufunga mbingu ili dunia isinyeshe, akalishwa na Mungu kwa namna ya ajabu, akakingwa na maadui waliotaka kumuangamiza, akapewa muujiza wa kuonana na Mungu mlimani sinai, na mwishowe akapewa tuzo la kupandishwa mbinguni bila kupita kifo. Yote hii ilikuwa ni zawadi au tuzo aliyojaliwa na mwenyezi Mungu. Kweli Elia alikuwa mtu mwenye haki na mbele ya Mungu kwa hakika alipata upendeleo wa ajabu.
Nasi ndugu zangu kama Elia tujifunze kuwa watu wenye haki. Tuone fahari katika kumtumikia Bwana na kutenda mema. Wengi kati yetu huwa tunafikiri kwamba kuna raha kubwa katika kutenda dhambi. Tunafikiria ati tunakafahari Fulani. Lakini hili sio kweli. Hii ni kwa sababu ile raha unayofikiri kwamba unaipata sio raha-mara nyingi unakuta kwamba kuna anayeteseka kwa ajili ya hiyo raha yako. Labda tuchukulie mfano wa dhambi kama ya majivuno-ili niweze kujivuna, lazima kutakuwa na wengine nitakaolazimika kuwakanyagia chini na kujionesha kwamba mimi ni bora kuliko wao, kwamba kuna vitu wao hawawezi lakini mimi nipo bora. Au ili niweze kuwa tajiri kwa kudhulumu, kuna watakaolazimika kunyanganywa mali zao ili niwe tajiri. Hivyo, unakuta kwamba siku zote hakuna raha iliyoko katika kutenda dhambi. Dhambi yangu husababisha kilio na maumivu kwa wengine. Ndivyo ilivyo. Lakini kutenda haki ndiko kwenye raha Zaidi kwani haki humfanya mwingine naye afurahi na hata kupata afya Zaidi. Basi ndugu zangu sisi tupende kuwa watu wenye haki. Tutafakari jinsi yatima wengi, wajane, na vilema na viwete wanaoteseka kwa ajili ya kunyimwa haki zao. Wengi wao sasa ni maskini kwa sababu tu walinyimwa haki zao. Baadhi walishakufa kwa sababu tu ya kukosa haki. Sisi tusikubali tutawaliwe na ukosefu wa haki.
Katika injili yetu, Yesu anatufundisha namna ya kusali na leo anatumia sala ya Baba yetu. Tunachogundua katika sala hii ni kwamba Yesu anatuambia kwamba tunapokwenda mbele ya Mungu kwa ajili ya kusali, basi lazima ukute tumejiandaa. Kwanza tumpatie Mungu utukufu wake, halafu tumweleze na shida zetu, na kumwomba atuepushe na dhambi kwani haya ni mambo yanayotutenga naye. Sala hii itufundishe hasa kwenye zile sehemu tunazokosea katika sala. Wengi tunakuja kanisani lakini huwa hatuanzi kwa kuukiri ukuu wa Mungu wetu-kwamba yeye aweza, yeye ndiye yeye, yeye ni mkuu haswa. Halafu cha pili ni kwamba tunashindwa kumweleza Mungu shida zetu-tunakaa mwanzo hadi mwisho bila ya kumweleza chochote. Pia huwa hatumuombi atuepushe na nafasi za dhambi. Sala hii itusaidie Zaidi na Zaidi kwenye kujifunza kuvuna neema zinazopatikana katika sala
Maoni
Ingia utoe maoni