Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Juni 13, 2020

Jumamosi Juni 13, 2020.
Juma la 11 la Mwaka

1Fal 19:19-21
Mt 5: 33-37

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana inaanza kwa kuliangalia somo la Injili. Hapa tunamkuta Yesu anakataza juu ya kuapa-anasema kamwe tusiape wala kwa jina la Mungu, wala kwa mji wa Mungu, au hekalu au hata kwa kiungo chako mwenyewe. Yesu anashauri watu kuwa wakweli kwa kile wanachokisema na hakuna haja ya wao kuongeza maneno ya ziada. Maneno yote ya ziada ni kutoka kwa yule muovu.

Yesu anasema hivi kwa sababu kusema kweli, Mungu amekuwa mhusika wa kutapeliwa na mwanadamu siku zote. Yaani mwanadamu huwa wakati wa shida tunafika mbele ya Mungu na kunyenyekea kweli na kumwambia Mungu atusaidie, atuangalie kwa macho yake, na huwa tunaahidi mengi kweli ya ajabu. Mfano, mwanafunzi anayejiandaa na mtihani mgumu husali sana na kuweka ahadi nyingi mbele ya Mungu-labda ooh!ee Mungu nitakuwa mtu mwema, nitakuwa naenda kanisani kila siku, lakini subiri mtihani upite na mbaya Zaidi afaulu vizuri, Mungu anasahaulika. Au tukipatwa na ugonjwa au ajali-huwa tunanyongonyea sana. Huwa tunasali, tunaahidi mengi lakini nikishapona, namsahau Mungu. na mbaya Zaidi itokee siku tumeonja kidogo kapombe, huwa tunaongea maneno ya majivuno ajabu kana kwamba sisi ndio miungu ya huku duniani.

Basi Yesu leo anasema kwamba tuache kumfanya Mungu kuwa mtoto. Huku ni kumchezea na kumdharau. Na ubaya ni kwamba wengi wetu huwa tunaona Mungu akikaa kimya baada ya kumdanganya na kufikiria kwamba ati ni dhaifu au Mungu hayupo. Sio hivyo ndugu zangu. Mungu anatuonea tu huruma. Angeamua kuturudi kwa hakika wengi wetu ungekuta tumekwisha angamia. Hivyo, kukaa huku kimya kwa Mungu tukuone kama huruma yake na si udhaifu.

Somo hili kweli linawagusa wengi. Hii ni kwa sababu karibu kila mmoja wetu aliwahi kuwa muongo mbele ya Mungu: amewahi kumdanganya tu. Tumewahi kuapa sana. Hivyo, ni siku ya kuanguka magotini na kumwambia Mungu azidi kutusamehe na atuhurumie kwa udhaifu huu.

Somo hili pili litufunze tuache utapeli hasa kwa wageni. Wengi wetu hasa tunapowaona watu wageni wasiotufahamu, huwa tunatabia ya kutowahurumia-kama ni mwenye duka anaweza kumtapeli na kumwambia anunue bidhaa mbovu. Vijana wengi wamewatapeli mabinti na kuishia kuwasababishia magumu maishani mwao kwa sababu ya utapeli tu. Leo tunaaswa tuache tabia hizi.

Katika somo la kwanza, tunakutana na habari za kuitwa kwa nabii Elisha. Yeye anaacha yote na kumfuata Elia. Yeye anapoambiwa amfuate na anapoomba kwenda kuwaaga wazazi wake, kweli anatimiza ahadi yake hii na kurudi. Huu ni mfano wa kuigwa wa mtu asiyetapeli. Wengi wetu tukiwaambia wenzetu kwamba tunakwenda kuaga nyumbani na kurudi, wengi hawarudi. Mfano, wa vijana wanaochagua kwenda malezi ya upadre; inapofikia kipindi na kuomba ruhusa ya kwenda kuaga nyumbani, mara nyingi hawarudi. Vijana wengi wamewatelekeza wake zao kwa kuwadanganya kwamba wanakwenda kutafuta fedha au kazi na kuwarudia na kumbe wakaishia kuoa wengine. Hivyo basi tujifunze toka kwa Elisha. Tutumize viapo vyetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni