Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Juni 12, 2020

Ijumaa, Juni 12, 2020,
Juma la 10 la mwaka wa Kanisa

1Fal 19: 9, 11-16;
Zab 26: 7-9, 13-14;
Mt 5: 27-32

MOYO ULIYO SAFI!

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Mungu inaanza kwa kuuangalia wimbo wetu wa katikati na maneno tunayokutana nayo ni mzaburi akiutafuta uso wa Bwana. Haya maneno ya Zaburi yalisemwa na Daudi alipokuwa katika shida mbalimbali. Aliutafuta uso wa Bwana kwa matumaini akitegemea kwamba Bwana atajionesha kwake na kusikiliza malalamiko yake na kumletea ahueni maishani mwake. Na kweli Bwana alikubali kumwonesha Daudi uso wake.

Lakini leo katika somo la kwanza, anayeutafuta uso wa Bwana ni nabii Elia-huyu yupo katika huzuni kubwa, amechoka kukimbizwa na maadui-mama wa kipagani aitwaye Jezebeli aliyetaka kumteketeza kwa sababu ya kumshuhudia Bwana Mungu wa Israeli. Elia ametembea kwa siku arobaini mchana na usiku hadi kwenye mlima wa Mungu na akiwa huko anautafuta uso wa Bwana. Na kweli Bwana anajitokeza kwake na kumtia moyo na kumwelekeza namna ya kufanya na Elia anapata tena ahueni maishani. Kweli Elia alikutana na uso wa Bwana.

Nasi kama Elia ndugu zangu, kila siku tunakimbizwa na maadui wetu. Kuna njaa, maisha magumu, magonjwa, wezi, watu wenye roho mbaya pamoja na tamaa na dhambi zetu sisi wenyewe. Tuutafute uso wa Bwana. Basi tuutafute uso wa Bwana kama Elia na hakika Bwana atakuja kwetu.
Pili ni namna Elia alivyotegemea Mungu aje kwake. Elia alifikiria kwamba angekuwako kwenye zile ngurumo au tetemeko. Lakini Mungu alikuwako ndani ya sauti tulivu. Kiwewe na Shida za Elia zilimfanya afikiri kwamba Mungu angekuja kwake kwa hali ya nguvu sana, kwa ngurumo kali. Lakini cha ajabu ni kwamba Mungu anakuja ndani ya sauti tulivu kabisa. Hapa tunalojambo kubwa la kujifunza: sisi wakati labda tunasumbuliwa na maadui wakatili sana, tunategemeaga Mungu aje kwetu kwa nguvu kweli, atoe kipigo cha ajabu na kuangamiza kila mtu. Lakini mara nyingi Mungu huja kwa utulivu na kumpatia huyo mtu nafasi ya kujirekebisha. Ndivyo ilivyo ndugu zangu: mara nyingi penye utulivu na subira ndipo panapokuwa na maendeleo. Fujo hazituleteagi chochote. Hivyo, basi tuzidishe subira na tuache papara.

Katika injili yetu tunakutana na Yesu akitueleza kwamba kama kuna kiungo kinacho tukosesha ni afadhali kukikata kuliko kukiacha na kukufanya uingie kwenye jehanamu. Somo hili litufanye tuachane na marafiki wabaya hasa wale wanaoshauri tutende dhambi na wakikuona unakemea dhambi ndio chanzo cha kukuchukia na kukuita mnafiki. Tukumbuke kwamba kuna marafiki ambao wakikuona umelewa, au umevunja mtu au umelazwa maabusu-ndio wanakupenda, wanakufurahia, wanakutembelea nyumbani kwako, wanakuja na kucheka na wewe. Wakisikia kwamba umefanya uasherati tena hadharani, wanafurahi na kukuona kweli wewe ndiwe mtu, mjanja kabisa na watakuchekea sana na kukukaribisha kwenye sherehe zao za pombe. Lakini wakikuona umeachana na maovu, basi ndio mwisho. Marafiki kama hawa, achana nao, kata urafiki huu. Tafakari hii iturekebishe hasa wale ambao ni wanachama wa kundi la marafiki wanaoshinda baa hasa wikiendi yote. Wakitoka baa hii watakwenda ile, wakitoka hii watakwenda ile, basi jamani, mwenye marafki kama hawa, tujichunguze, kweli hawa marafiki wanatutakia mema? Nakushauri achana nao. Wanataka uwe maskini. Mungu atutie nguvu.

Maoni


Ingia utoe maoni