Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Juni 10, 2020

Jumatano, Juni 10, 2020
Juma la 10 la Mwaka

1 Fal. 18:20-39
Mt 5: 17-19.


SHERIA YA UPENDO!
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari yetu asubuhi ya leo. Tafakari ya neno la Bwana leo inaongozwa na wimbo wetu wa katikati toka zaburi ya 16 na kiitikio chetu kinasema “Mungu unifadhi mimi kwa maana nakukimbilia.” Haya ni maneno aliyoyaimba Daudi alipokuwa akimuomba Mungu usalama: amlinde na maadui. Daudi kwenye maisha yake, alikabiliwa na maadui wenye nguvu kama akina Sauli, akina Goliathi, na akina Absalom aliyekuwa mtoto wake. Daudi kila mara alipokumbana na magumu haya, alimuomba Mungu usalama akimsihi asimtupe. Na katika kuomba huku, kila mara alitoa ahadi kwa Mungu: alimwambia kwamba hakika wewe ndiwe utakayekuwa Mungu wangu daima nitakayekutumikia na kamwe sintahangaika na miungu mingine. Na alikuwa na matumaini kwamba akishamuweka Mungu mbele, hakika hatashindwa katika lolote.

Leo katika masomo yetu tunaona kwamba anayemuomba Mungu usalama ni Nabii Elia na hili tunalisikia katika somo la kwanza. Yeye alikuwa akiwindwa na mke wa mfalme Ahabu aitwaye Jezebel kutokana na yeye kuwa nabii wa Mungu. Na hivyo alikataa kuwaabudu miungu mingine iliyoletwa na huyu mke wa mfalme Ahabu. Tendo hili lilimfanya atake kuuawa. Na hivyo, leo anaamua kumwambia Mungu kwamba aende mlima Karmeli na hapo apate kuwaonesha kwamba kweli Mungu wa Israeli ndiye Mungu wa kweli. miungu mingine sio kitu. Na hivyo anaomba wachinje wanyama wa kuteketezwa kama sadaka na Mungu atakayeshusha moto kuteketeza sadaka hizi ndiye atakayeonekana kuwa Mungu wa kweli. Wanaanza manabii wa wale miungu ya uongo kuomba ili mungu wao ashushe moto iteketeze zile sadaka lakini hakuna moto unaoshuka.

Anaingia Elia kwa unyenyekevu kabisa kuomba Mungu asikatae kushusha moto kwani endapo asingeshusha, basi ingekuwa ndio mwisho wake. Hakika wangalimuua. Mungu anasikiliza sala yake na kushusha moto. Na Elia anafurahi, na anaahidi kumtumikia Mungu na watu wanaona na kuamini kwamba kweli Bwana Mungu wa Israeli ndiye Mungu.

Hapa tunalo kubwa la kujifunza. Kweli Daudi na Elia walimuomba Mungu awafadhili na kweli aliwafadhili na kuwaondoa katika aibu za kushindwa. Nasi ndugu zangu tunapataga nafasi ya kushiriki katika matukio mbalimbali na mashindano mbalimbali na mitihani mbalimbali. Kweli sala zetu tushirikipo kwenye mashindano au mitihani au interview kama hii-lazima kumuomba Mungu atufadhili, tusifedheheke ndugu zangu. Kufeli vitu kama mitihani kweli huwa vinamfanya mtu anyongonyee kweli. Na kweli ikitokea umefeli hasa mtihani-hata kama ni testi tu-lazima ujisikie vibaya sana-wengine huwa wanachana karatasi au kuficha au hata kubadili ile maksi ili wasichekwe na marafiki au wadogo au wake zao.
Jamani, kila tuingiapo kwenye haya mapambano, tumwombe Mungu tusifedheheke. Na hata kama tunaingia kwenye mashindano kama ya interview ya kuomba kazi au kwenye kugombea uongozi au kutafuta scholarship. Lazima kumuomba Mungu jamani tusifedheheke. Lakini pia tusisahau kumtumikia huyu Mungu baada ya kutufanyia mazuri yote haya na kumfanya abakie kuwa Mungu wetu daima. Hili lazima kumwomba Mungu sana ndugu zangu.

Kingine ni kwamba tutambue kwamba pale unapoeleza stori yako ya jinsi Mungu alivyowahi kukusaidia hasa mbele ya watu-huu unakuwa ni ushuhuda na kweli unakuwa kana kwamba ndio unaihubiri injili na kumshuhudia Mungu. kweli hili linakuwa jambo jema.
Nabii Elia alikuwa pia tayari kumtetea Mungu dhidi ya wale waliokuwa wanamtukana. Nyakati zetu jina la Mungu huwa linatukanwa na baadhi ya watu. Kweli tujiepushe na watu kama hawa-tusijiunge nao kulitukana jina la Mungu. Na wala tusi-like page zao. Jina la Mungu tuliweke takatifu na tukisikia mtu akilitukana lazima kumwonya.

Maneno ya shangilio leo yanatuambia kwamba tumwombe Mungu atusaidie kuzielewa na kuzishika njia zake. Na hili ndilo Elia analopambana nalo leo na hli ndilo Yesu analosema leo katika injili kwamba kamwe tushike neno lake kama lilivyo bila ya kupunguza. Kweli suala hili la kupunguza ukali wa maneno ya kiinjili na kuipatia maana nyingine ndio umekithiri sana leo hii. Siku hizi tunalegeza sana sheria za Mungu kwa kuzipatia maelezo mapya. Hii imefanya dhambi nyingi zitendwe sana. Wapo kati yetu tunaotumia biblia kuhalalisha ulevi, Ndoa za wake wengi na uasherati. Jamani, hapa tunalichafua neno la Mungu. Sheria ya Mungu ibakie takatifu siku zote

Maoni


Ingia utoe maoni