Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Juni 11, 2020

Alhamisi, Juni 11, 2020,
Juma la 10 la mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mt. Barnaba Mtume.

Mdo 11: 21-26, 13: 1-3;
Zab 97: 1-6;
Mt 10: 7-13

PEANENI MOYO!

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya leo tunapoadhimisha sikuu ya mtakatifu Barnaba mtume. Somo la kwanza linatupatia habari za Barnaba akitumwa na mitume toka Yerusalem kulihudumia kanisa la Antiokia. Na kweli huyu Barnaba alijitahidi sana kulilisha kanisa hili la Antiokia kiasi kwamba lilikuja kuwa ndio kanisa lililochangia sana kwenye uinjilishaji na umisionari wa ukristo kwa makanisa mengi. Kanisa hili lilisaidia kuieneza injili hasa kwa watu wa mataifa. Waliosaidia sana walikuwa ni Paulo na Barnaba. Na Barnaba alikuwa na mchango wa pekee kwa hili kanisa kama tunavyosikia katika somo la kwanza. Yeye alikuwa na upeo wa ajabu. Alikwenda Tarso na kwenda kumleta Paulo. Alijua kwamba kweli Paulo atakuwa na mchango mkubwa kwa kanisa. Paulo alikuwa bado hajakubalika kwenye lile kanisa la mwanzo kwa sababu wengi walimhofia kwamba sio mtume kweli. Walimuona kwamba bado anaweza kuja kuwatesa tena. Lakini Barnaba alisaidia sana kuwaelewesha watu kwamba Paulo kweli ameongoka na Bwana kamtokea na hivyo tayari ni mfuasi hodari wa Yesu.Tunasikia katika somo hili kwamba kwa pamoja walichaguliwa kwenda umisionari na kutumwa na lile kanisa la Antiokia.

Katika somo la injili, tunakutana na maagizo waliyopewa wanafunzi wa Yesu wakati wa kuhubiri injili. Waliambiwa wawasaidie watu kwenye magonjwa yao. Wawaponye ili jamani wapate unafuu wa ugonjwa wao. Halafu waliambiwa wawatoe pepo yaani wawaokoe watu kutoka vifungo vya shetani; halafu waliambiwa wawe wakarimu kwenye kutoa huduma hizi, wasidai pesa kwa sababu wamepewa tu bure na hivyo watoe bure. Waliambiwa wasibebe fedha yaani wasihangaikie sana na ati watakula nini-wakishafanya kazi zao watu watawalisha. Na waliambiwa wawe watu wa Amani-kila nyumba watakayoingia waisalimu kwa jina la amani.

Ndugu zangu, Barnaba na Paulo walizifuata kanuni hizi kisawasawa hasa kwenye safari zao za kimisionari na kutokana na hili, waliweza kuwafikia wengi sana na kuanzisha makanisa ya kutosha.
Sisi ndugu zangu ndio Barnaba wa sasa. Tuishi kama Barnaba. Yeye aligundua vipaji vya Paulo na kuweza kumleta kwenye ile jamii ya wakristo na kweli kanisa lilimfaidi sana Paulo. Kweli kusingekuwa na Barnaba, kweli Paulo angefia na vipaji vyake huko na kanisa lisingefaulu. Japokuwa Paulo alikuja kuwa maarufu kuliko Barnaba, Barnaba hakusita kwenda kumchukua kwani alijua kwamba kazi ya Bwana haihitaji kushindana. Na hili ndilo tunaloalikwa kufuata ndugu zangu. Kila mmoja awe Barnaba. Kuna wengi wangeweza kuisaidia jamii lakini wamekosa wa kuwavuta na kuwaleta juu ili waisaidie. Kuna wengine wamekataliwa na jamii kwa sababu tu ya kutokueleweka na baadhi ya watu na hivyo wanahitaji watu kama akina Barnaba wawatetee. Hivyo, tuwe kama Barnaba. Tuwainue wale ambao twajua kwamba hakika waweza kuisaidia jamii na wale wanaosemwa vibaya bila haki tuwainue tena.

Halafu kama Barnaba, tuwe na moyo wa kupenda kazi ya Bwana. Tusigombane au kutafuta umaarufu kwenye kazi ya Bwana. Anayepaswa kupatiwa umaarufu ni Mungu mwenyewe. Mara nyingi uhubiri wa injili umerudi nyuma kwa sababu ya kutokuelewana kati yetu sisi wahubiri, tunataka sifa binafsi, nataka mimi nitukuzwe kuliko Kristo. Pia maslahi binafsi-kupenda fedha, mali, yote haya huiangamiza kazi ya Bwana. Tumweke Kristo mbele ya yote. Mtakatifu Barnaba utuombee.

Maoni


Ingia utoe maoni