Jumatano, Juni 03, 2020
Jumatano, Juni, 3, 2020,
Juma la 9 la Mwaka wa Kanisa
2 Tim1: 1-3, 6-12;
Zab 122: 1-2;
Mk 12: 18-27.
MIMI NI UFUFUO NA UZIMA!
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu katika siku ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunamkuta mtume Paulo akimpatia Timotheo, mtoto wake wa kiroho na mshirika wake mkubwa ambaye basi Paulo aliweka matumaini sana kwake akitegemea kwamba baada ya hata yeye kufa, yeye ndiye atakaye endeleza utume wake wa kulijenga kanisa. Na kweli Timotheo alifanya kazi hii kwa uaminifu na ndio maana Paulo alionesha sana matumaini kwake.
Leo basi anamweleza kwamba kwa kweli anamshukuru Mungu kwa zawadi ya huyu Timotheo na anamweleza kwamba anamtegemea sana katika kueneza injili. Hivyo anamsihi kwamba kamwe usiionee aibu injili, na wala asione haya kwa sababu Paulo ati kafungwa. Bali anapaswa kushiriki katika kuihubiri habari njema kwa nguvu zote. Asikate tamaa kwani habari njema ni mali ya Kristo na Kristo atailinda salama milele. Mawaidha haya yalihitajika kwa huyu kijana Timotheo ili asikate tamaa kwa sababu kipindi hiki kulikuwa na uadui mkubwa sana dhidi ya ukristo. Na kweli Timotheo alifungua moyo wake na kuruhusu mawaidha haya kumtia moyo na kuanza upya.
Kweli Timotheo ni mfano kwetu. Tatizo tunalokumbana nalo sisi nyakati hizi ni kwamba huwa tunapewaga mawaidha tena mazuri: na Maaskofu wetu, na Baba mtakatifu, na mapadre wetu-lakini jamani huwa hatufunguagi mioyo yetu na wengi huwa hatuaminiani-tunaona kana kwamba tunadanganywa tu, hili ndilo tatizo kubwa sana kwenye ukristo na ndio maana hatusongi mbele. Unahubiri lakini mwingine anasema huyu anatudanganya tu, na cha ajabu ni kwamba tumeshapitisha huu moyo wa kutokuaminiana hadi kwa vijana na watoto wetu. Inafika mahali nao wanaona kwamba hata kile kinachohubiriwa kanisani ni uongo tu; ni kudanganyana. Lakini nikuambie ukweli-kama kina Timotheo wangemuona Paulo kwamba kila anachowaambia ni usanii kweli kazi yake isingeendelezwa. Jamani tujifunze kuyapokea mawaidha ya viongozi wetu wa kanisa, wao husema kwa jina la kanisa, kila wanaposema kwa jina la kanisa-hiki wanachosema turuhusu kitutie moyo. Tuache tabia ya kuona kwamba kila kinachosemwa ni usanii. Tusijione wajuaji kupita kiasi, kuna wakati wa kusikiliza, wa kumwacha Mungu anene kupitia viongozi wetu wa kanisa.
Katika somo la injili leo tunamkuta Yesu akitumia mfano aliopewa na Masadukayo, wa mwanamke aliyeolewa na wanaume saba na wote kufariki na Yesu kuelezea kwamba maisha ya mbinguni sio kama ya hapa duniani. Na vitu tunavyopewa hapa duniani ni kutusaidia sisi tuweze kufika maisha ya mbinguni. Hivyo tuwe na hekima katika kutumia mali na urafiki wote wa hapa duniani.
Tuhakikishe kwamba yanatufikisha kwa baba, tusikubali vitu kama urafiki vitupeleke pembeni. Nasema hivi kwa sababu kuna wengi kati yetu ambao tumeharibiwa na urafiki mbaya, baadhi tumewadharau wazazi au wake zetu kwa sababu ya rafiki tu-ni rafiki kanifanya nitende dhambi nyingi hivi. Huu sio urafiki wa Kimungu. Rafiki anayesababisha majanga hivi angalau kumwacha. Yesu alisema kama mguu wako unakukosesha uukate. Kama rafiki yako anakukosesha kata urafiki naye. Angalau kuishi bila huyo rafiki lakini kwa raha na amani na upendo na watu wote kuliko kuwa na huyo rafiki na labda akupatie umaarufu au pesa za kutosha lakini kumbe anakufanya uikosee jamii kiasi hicho na kutenda dhambi daima. Haya mambo yanawahusu hasa wale wanaodanganywa na marafiki wabaya na kuwadharau wazazi wao, au wengine wake zao, usifungwe na raha za kutenda uovu ukaikosa Mbingu. Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni