Alhamisi, Juni 04, 2020
“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Alhamisi, Juni, 4, 2020,
Juma la 9 la Mwaka wa Kanisa
2 Tim 2: 8-15;
Zab 25: 4-5, 8-10, 14;
Mk 12: 28-34
UPENDO WA AGAPE!
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika waraka wa pili wa mtume Paulo kwa Timotheo; hapa tunakutana na mtakatifu Paulo akiwa gerezani na mwisho wa utume wake unakaribia. Na hivyo anamtegemea sana Timotheo aendeleze kile alichokianza yaani ile kazi ya Bwana. Na leo Basi anajaribu kumwonya, anamwambia amfikirie Yesu siku zote, ni wa thamani kubwa na ndiyo maana amefungwa kwa sababu yake. Amekubali kufungwa kwa sababu ya wateule wa Mungu wapate kuisikia habari njema na kuokolewa. Hivyo, anamweleza ateseke pamoja na Yesu na aishuhudie injili siku zote kwani Yesu hatamwacha kamwe, hakika atampeleka pale alipo. Ajitahidi kuwa mwaminifu katika kazi yake. Haya ndiyo mawaidha ya Paulo kwa mwanae Timotheo na kwa kweli anamtegemea sana Timotheo.
Ndugu zangu, mimi na wewe ndio Timotheo wa sasa na Mungu anamategemeo mengi sana juu yetu hasa kwenye kuihubiri kuendeleza utume wake. Hivyo, ni lazima tumkumbuke Yesu siku zote, tumfikirie yeye kila wakati, ajae akilini mwetu, tujitahidi kuwa waaminifu siku zote, tusikubali kutoa mwanya kwa ajili ya adui atushike kwenye dhambi au atukamate na kashfa. Tupende maisha ya sadaka. Tujue kwamba kanisa limeweza kufika hapa tulipo kutokana na utayari wa watu waliokuwa tayari kujitoa sadaka. Sisi tusiwe watu wa kutafuta faida yetu kila siku; siku nyingine jamani tukubali kuwaachia wengine, tukubali tuumie ili wengine wafaidi, sio kila siku mimi nitoke na faida. Kama ni hivi basi mimi ni mlafi au mchoyo wa kupindukia, asiye na utii wala upendo-kama kila siku natoka na faida.
Katika injili yetu tunakutana na Yesu akijibu swali la mwanasheria kwamba hakuna amri iliyo kuu kuliko kumpenda Bwana Mungu kwa moyo wote, kwa roho na kwa akili na kumpenda jirani kama nafsi yako. Huyu mwanasheria anamsifu Yesu kwa kutoa jibu zuri vile na yeye analifurahia, na Yesu anamwambia ama kweli hauko mbali na ufalme wa mbinguni. Na kweli hayuko mbali kwani alifurahishwa na jibu la Yesu na kingine ni kwa sababu sasa yeye mwenyewe amejua amri iliyo kuu, yaani matakwa ya Mungu na kwa kitendo hiki cha kujua amri hizi basi hayuko mbali na ufalme wa Mungu. Sisi tuombe kuwa karibu na ufalme wa Mungu.Kwa kuwa karibu na ufalme wa Mungu ni kukubali na kutambua kwamba sisi ni Timotheo wapya, tunategemewa na wengi. Ni kukubali kufikiria juu ya Yesu, kumruhusu ajaze akili zetu na mioyo yetu. Tusijaze akili zetu na mioyo yetu na mapicha au mafilamu ya kiajabu au miziki ya kiajabu, tusijaze mioyo yetu kwa kusikiliza maneno yasiyofaaa, tusijaze mioyo yetu na ulevi. Tusikubali faraja za kiajabu. Faraja yetu ipatikane katika sala, kwa kumfikiria Yesu, kwa kumjaza Yesu akilini mwetu. Hapa ni kuwa karibu na ufalme wa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni