Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Juni 02, 2020

Jumanne, Juni 2, 2020,
Tafakari ya kila siku
Juma la 9 la Mwaka wa Kanisa

2Pet. 3:11-15, 17-18
Mk. 12:13-17

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya leo. Leo neno la Bwana katika tafakari tutaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo neno kuu la kututafakarisha linalotumiwa na Mt. Petro ni kwamba tuuone uvumilivu wa Bwana kama nafasi atupayo ili tuweze kutubu na kuokolewa. Kweli huu ni ujumbe muhimu sana. Hii ni kwa sababu kweli Mungu amekuwa akionesha uvumilivu wa ajabu: ngano imekuwa ikikua na magugu na Bwana anaangalia tu-sisi tumekuwa tukijiuliza kwa nini Mungu asingoe haya magugu? Lakini yamekuwa tu siku zote ndani ya shamba la Bwana. Penye watu wema unashangaa panakuwa na mtu mbaya-anayechafua na kudhalilisha na tena mtu huyu kwa baadhi ya nyakati amekuwa akipata nguvu zaidi kuliko wale watu wema na kuwanyanyasa na kuwakandamiza; yote haya yamekuwa yanatendeka na Mungu anaona na usifikiri kwamba alikuwa haoni.

Mwanae mpenzi aliteswa hadi akauawa na Mungu alikuwa anaona na kuangalia tu, mitume wake karibu wote waliteswa mateso makali na kuuawa na wapagani lakini Mungu alikuwako tu-anaona na anafahamu yote. Jina lake limekuwa likitukanwa sana na yeye japokuwa ana nguvu za ajabu kakaa katulia bila kutoa mapigo yoyote. Kuna mwana-anga mmoja alifanikiwa kupaa hadi kufikia kule anga za mbali kabisa na baada ya kuwezeshwa na Mungu kufika kote huko-aliandika kipeperushi chake na kusema-nimefika hadi huku juu mbali kabisa; kule wanakosemaga anakaa Mungu lakini sijakutana na kitu kama Mungu. Ukweli ni kwamba wengi tumetumia huu uvumilivu na ukimya wa Mungu kumtukana na kumwambia ati Mungu hayupo; wengine tukadiriki kuandika ati Mungu tayari amekwisha kufa. Ndivyo ilivyo ndugu zangu.

Lakini tutambue kwamba Mungu kakaa kimya kwa sababu tu ni mwenye huruma, nawaelezeni, siku akinyanyuka huko-mwanadamu hatakuwa na cha kusema. Na kweli kuna siku Mungu ananyanyukaga na kutishia-fikiria mambo kama ya matetemeko-unakuta watu labda ndio wanafurahi, wanajivuna lakini gafla bila hata ya matarajio yao wanapatwa na mapigo mazito kama matetemeko ya ardhi yanayosababisha uharibifu mkubwa. Hivyo, kamwe tusitumie ukimya wa Mungu kumtukana, ukiona kwamba ulikuwa umetenda kosa kubwa lililostahili adhabu kali lakini Mungu hajakufanyia chochote-nakueleza wee anguka magotini kwake, tubu, mwambie Mungu nihurumie. Usitumie ukimya wake kujionesha kwamba yeye ni dhaifu na si Mungu. Watakatifu kama akina Francisco waliweza kuzitumia nyakati kama hizi za ukimya wa Mungu ili kumtukuza na kumjua zaidi. Hivyo tuache majivuno jamani, kamwe tusifikiri kwamba kwa kukaa kimya; basi Mungu ndio kabisa hayupo. Au hana nguvu. Labda wengi wetu tungetamani wezi wote wauawe na Mungu mara moja, maadui wetu wote wanaotutesa wauawe mara moja na Mungu, Mungu awangoe katika shamba lake. Lakini tujue anawapatia wakati wa kutubu. Nasi tujifunze kuutumia muda huu vyema. Ukiona mungu kakumezea basi anguka magotini mwake na kamwe usimtukane.

Katika somo la injili tunakutana na vikundi viwili vilivyo na nia mbaya na visivyopatana-Maherodi na Wafarisayo-lakini leo wanapatana kwa mara ya kwanza kwa lengo la kumtega Yesu akosee ili wamwangamize. Lakini Yesu anatambue nia yao na kwa kweli hawamshindi.
Ndivyo ilivyo ndugu zangu: watu wakishakuchukia, maadui zako wote-hata wale wanao pingana wao kwa wao utashangaa ikifikia ule wakati wa kukusema au kukufanyia ubaya wataungana kwa lengo la kukufanyia huu ubaya. Haya yalimtokea Yesu na kati yetu yanatokea. Na hadi leo Yesu bado kawaacha watu wabaya waendelee kukaa katika shamba lake akiwapatia nafasi ya kuongoka. Cha kufanya ni kuwa kama Yesu, tuhakikishe kwamba hawana cha kutudai, yaani maisha yetu ni safi, bila hatia; hapa tutawaweza. Lakini tukiwa ni watu dhaifu na waovu basi watapata cha kutusumanga nacho na hapa watatuangusha.

Maoni


Ingia utoe maoni