Jumapili, Mei 31, 2020
Jumapili, Mei 31, 2020.
Dominika ya Pentekoste
Sherehe ya Pentekoste
Mdo 2: 1-11;
Zab, 104: 1, 24, 29-31, 34;
1 Kor 12:3-7, 12-13 au Rom 8:8-17
Yn 20:19-23 au Yn 14:15-16, 23-26
WEKA ULIMWENGU KWENYE MOTO WA MAPENDO YA MUNGU
‘Pentekoste’ ni neno la Kigiriki lenye maana ya “Hamsini”. Wakristo wanasherekea sherehe hii siku hamsini baada ya Pasaka (Mdo 2). Ikiwa ni tamaduni iliyotoka Agano la Kale, yenye maana ya “sikukuu ya mavuno” katika siku ya hamsini baada ya “Pasaka ya Wayahudi” (Kut. 23:16, Hes. 28:26-31, Kum. 16:19-21). Siku hii ilikuja kuwa muhimu kwa Wakristo kwasababu, majuma saba baada ya ufufuko wa Yesu, wakati wa sikukuu ya mavuno ya Wayahudi, Roho Mtakatifu aliwashukia wafuasi wa kwanza wa Yesu, akiwapa nguvu na uwezo wakumtangaza Kristo na kuwakusanya pamoja kama Kanisa. Kama Wayahudi walivyokuwa wakitoa matunda ya mazao yao ya kwanza, wakijiandaa kwa mvua kwa ajili ya mazao yajayo; wafuasi, mazao ya kwanza ya utume wa Kristo yaliyoiva, wanapokea mvua ya Roho Mtakatifu, Roho atakaye wafanya wakue na kuwa mazao na mbegu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Katika Siku hii, umoja wa watu wa Mungu kama Kanisa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ulianza.
Roho Mtakatifu alitumwa kama Yesu alivyo ahidi, ili kukamilisha kilele cha ufunuo wa upendo wa Mungu. Roho Mtakatifu hajiweki kwa Wayahudi peke yao, bali anafunua upendo wa Mungu usio na mipaka kwa watu wote, akileta Baraka, matunda katika nchi ambayo ilikuwa imelaaniwa kipindi cha Adamu na Eva. Lugha iliyoleta mtafaruku nakutoelewana katika mnara wa Babeli, inakuwa kiunganisho kikuu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ukosefu wa urafiki na umoja na Mungu uliopotea katika Edeni, Roho Mtakatifu anaurudisha tena kwa kuwa na Kanisa daima.
Pentekoste tunasheherekea kazi na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu kama waumini na Kanisa. Mungu amemimina juu yenu wote Roho Mtakatifu (Rom 8:1-11) na tunapaswa kuishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu anatusaidia kumkiri Yesu kwamba ni Bwana wetu (1 Kor 12:3), akituwezesha kumtumikia Mungu (1 Kor 12:4-11), akituunganisha pamoja kama Mwili wa Kristu (1 Kor 12:12-13), anatusaidia kusali (Rom 8:26), anatuombea ndani ya Mungu Baba (Rom 8:27). Roho Mtakatifu anatuongoza (Gal 5:25) na Roho Mtakatifu anatusaidia tuishi kama Yesu (Gal 5:22-23).
Baba Mtakatifu Fransisko anamuita Roho Mtakatifu “Upendo” unaokosekana ndani ya familia zetu na Ulimwenguni. Katika ujumbe wake wa siku hizi tuu ndani ya “Amoris Laetitia”, “Furaha ya Upendo” anamuonesha Roho Mtakatifu kama mfano halisi wa Familia za Kikristo na Kanisa.
“Upendo ndani ya familia ya Kimungu, ni Roho Mtakatifu….tunaweza kutambua upendo wa Mungu ndani ya Roho Mtakatifu….kwa njia ya Kanisa, ndoa na familia zinapokea neema za Roho Mtakatifu kutoka kwa Kristo, ili tuweze kutoa ushuhuda wa Injili ya Upendo wa Mungu.”
Baba Mtakatifu anazialika familia zote za Kikristo “kila wakati kualika usaidizi wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza umoja wenu, ili neema zake ziweze kutawala katika kila jambo mnalokutana nalo”. Pia anasema, bila Roho Mtakatifu umoja wa familia za Kikristo hauwezekani. “hakuna hata moja kati ya haya, litakalo wezekana bila kusali kwa Roho Mtakatifu ili amimine neema zake, nguvu zake na moto wa Roho, kutufanya wake, kutuongoza na kubadili mapendo yetu kwa kila hali”
Leo tunaitwa, tuweze kujali kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu binafsi, familia, jumuiya na Kanisa zima. Je sisi ni vyombo vya kazi ya Roho Mtakatifu? Je, tumekuwa wasikivu wakati Roho Mtakatifu anapotuongoza? Matunda ya Roho Mtakatifu (Upendo, furaha, Amani nk.) yanakuwa ndani mwangu? Sisi wote tunaishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu lakini katika viwango tofauti. Tunazuiwa na uoga wetu, dhambi zetu, Mapungufu yetu na uharibifu wetu wa kila siku unaotufanya tushindwe kuhisi uwepo wa zawadi ya Mungu ya Upendo ‘Roho Mtakatifu’. Pentekoste inatupa tena wakati wa kuhisi moto wa Roho Mtakatifu na kuuweka Ulimwengu kwenye moto wa upendo wa Mungu.
Sala:
Nivuvie nguvu ya Roho Mtakatifu Bwana, ili mawazo yangu yaweze kuwa matakatifu. Nivuvie pia nguvu ya Roho Mtakatifu ili kazi yangu iweze kuwa takatifu. Gusa moyo wangu Roho Mtakatifu, niweze kupenda vile vitakatifu tu. Nipe ujasiri Roho Mtakatifu ili niweze kulinda kila kilicho kitakatifu. Nilinde Roho Mtakatifu, ili niweze kuwa Mtakatifu daima. Roho Mtakatifu, nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni