Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Juni 01, 2020

Jumatatu, Juni 1, 2020,
Tafakari ya kila siku
Juma la 9 la Mwaka wa Kanisa

2 Pet 1: 2-7;
Zab 90: 1-2, 14-16;
Mk 12: 1-12

MUNGU ANAYETUJALI (MWEMA)!

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu itaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunamkuta mwandishi wa
Barua ya pili ya mtume Petro akiwaambia waaamini kwamba wameitwa ili wawe watakatifu; na pia Mungu mwenyewe amewajalia karama na vipaji vitakavyowawezesha kufikia hii safari yao ya utakatifu. Maneno haya aliyasema kwa sababu kwa kipindi hiki cha mwishoni mwa karne ya kwanza, kulitokea manabii wengi wa uongo na pia falsafa nyingi za kiuongo zilizokuwa zinafundisha mambo tofauti. Walimu wa uongo walikuwa na lengo la kutafuta umaarufu na pesa na walijaribu kurahisisha maisha ya kikristo, yaani maadili yake waliyafanya legelege kinyume kabisa cha injili. Na walianza kupata wafuasi kwani baadhi ya wakristo walianza kuwaiga. Hivyo, mwandishi wa somo la leo anawaambia wakristo hawa kwamba wameitwa ili wawe watakatifu na hivyo wakazanie utakatifu.

Anawaeleza kwamba kuutafuta utakatifu sio kwamba ni kugumu kwani Mungu mwenyewe anatoaga msaada na nyenzo zitakazowasaidia kuupata huu utakatifu. Wazo hili linafanana na barua iliyotolewa hivi karibuni ya Papa wetu Francisco iitwayo *Gaudete Exsultate* inayotualika kukazania kuwa watakatifu. Papa anasema tunao mfano wa watakatifu wanaotusaidia katika hii tamaa yetu ya kuwa watakatifu-hivyo utakatifu ni kitu kinachowezekana na kila mmoja akikazanie.

Somo hili ndugu zangu lina mengi ya kujifunza hasa juu ya kuutafuta utakatifu. Kweli kuutafuta utakatifu ni jambo jema. Nawaelezeni ndugu zangu; mtakatifu akiwapo hata mmoja tu kwenye kijiji au mji au hata nchi kweli anaiokoa ile nchi, au kijiji au mji. Hii ni kweli ndugu zangu. Kwa mfano wake tu, wengi wanatiwa moyo, wengi wanasaidiwa ajabu. Labda nitoe mfano: sio kwamba namtangaza Mandela kuwa mtakatifu-lakini fikiria uwepo wake yeye mwenyewe tu ndani ya taifa lile la Afrika kusini, uwepo wa mtu kama huyo jinsi ulivyoweza kulisaidia taifa hili! Fikirieni jamani. Nakwambia waovu mia huogopa kufanya uovu wao kwa sababu ya uwepo wa mtakatifu mmoja tu. Sasa, ukitaka kuwatambua wao ni nani-ngoja huyo mtakatifu aondoke-utajua kwamba kuna uovu. Ukweli ni kwamba hata sisi tumeweza kufikia hapa tulipo kwa sababu tulisaidiwa na uwepo wa utakatifu katika jamii. Hivyo ndugu zangu tukazane, tuwe na watakatifu kwenye jamii zetu jamani. Uwepo wa Francisko mmoja aliweza kuibadili dunia. Tuombe tuwe na watakatifu. Wakati mwingine tunaishiaga kufurahia maisha ya dhambi tukifikiria kwamba ni mazuri-weee? Ngoja maisha ya dhambi yakutende na ndipo utakapotambua ubaya wa maisha hayo. Nakuambia hakuna jambo zuri kama kuwa na mtakatifu katika jamii. Mmoja tu huleta maajabu.

Katika injili yetu ya leo twamkuta Yesu akiwa kama mtakatifu mmoja kati ya viongozi wa Kiyahudi elfu waovu. Hawa waliwaua manabii, watajaribu tena kumwua Mwana pekee wa Mungu kama tutakavyosikia katika injili yetu. Lakini Yesu kama mtakatifu anawaambia ukweli wao na tumesikia kwamba walitaka kumdhuru lakini wakawaogopa watu. Somo hili linatupa ujumbe mzito hasa sisi ambao tuna tabia ya kutumia nguvu kufukia ukweli-wale wanaotoa pesa ili ushahidi upindishwe, wale wanao diriki hata kuua ili ushahidi upotee kwa leno la wao kuendelea bila kuguswa. Ndugu zangu, mambo haya yatakuwa na mwisho wake. Waliofanya hivi mwisho wao ulifika tu. Sisi tuwe wakweli, tuutafute utakatifu, tusifikiri kwamba nguvu zetu za kuongea, nguvu zetu za mwili, marafiki tulionao, pesa au vyeo tulivyonavyo au akili niliyonayo inaweza kunifikisha mbali sana. Itanisaidia labda kuepuka vizingiti vichache tu lakini sitafika popote. Sisi tuwe tu wakweli na watu wa kuutafuta utakatifu. Jamanii tusitumie cheo au akili yetu au madaraka yetu au wingi wa marafiki zetu kujivuna na kujiona kwamba twajua kila kitu.

Maoni


Ingia utoe maoni