Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Mei 30, 2020

Jumamosi, Mei 30, 2020.
Juma la 7 la Pasaka

Mdo 28: 16-20, 30-31;
Zab 11: 4-5, 7 (R. 7);
Yn 21: 20-25

KUMFAHAMU YESU!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Bado tupo katika kipindi cha novena na leo ni siku ya mwisho, siku ya tisa, siku ya neema. Siku ya kujiandaa kwa kumpokea Roho Mtakatifu kwa siku ya Pentekoste. Na leo tafakari ya neno la Mungu tukianza kwa kuiangalia injili yetu, injili yetu inatuongoza tutakayosoma leo inafunga sehemu ya injili ya kitabu cha Yohane kuashiria kwamba kipindi cha pasaka, na habari za Kristo baada ya kufufuka basi ndio zinafikia ukingoni. Hata kwenye somo letu la kwanza leo, sehemu ya kitabu cha matendo ya mitume tutakayosoma ni sehemu inayofunga hiki kitabu; yote haya ni kuonesha kwamba kipindi cha pasaka ndio tunakifunga kifunga. Habari za Kristo mfufuka zimeweza kuenea kwa watu hao wote kwa nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu. Wengi wameamini na mitume wamekazana kwa namna ya ajabu na hivyo ni juu yetu kuiga mfano wao hasa katika suala la kukazana kuipenda kazi ya Bwana. Hili ndilo lililo la muhimu.

Sasa katika injili yetu ya leo, Petro anaulizia hatma ya yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu. Yeye jana aliambiwa hatma yake kwamba watatokea watu watakaomfunga na kumpeleka asikopenda akimaanisha atakufa kifo gani na kweli Petro alikufa kifo dini. Petro aliposikia kwamba Yesu amemtabiria hatma yenye ugumu namna hiyo, basi alitaka kujua hatma ya yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu. Sababu za kufanya hivi labda yawezekana kwamba Petro aliona kwamba Yesu amemtabiria mwisho mgumu sana-hivyo yawezekana kwamba Petro alijiona kana kwamba Yesu anampatia adhabu kutokana na lile kosa lake la kumsaliti; hivyo alitaka kuulizia na mwisho wa yule anayempenda ili aweze kupima mwisho wake na yeye ili mwishowe alinganishe. Lakini Yesu anamwambia Petro hiyo sio juu yako; ni juu yangu mimi.

Ndugu zangu, Petro alikuwa miongoni mwa wanafunzi wenye umri mkubwa kuliko wale wengine. Pia alichaguliwa kuwa kiongozi wa wengine. Uongozi ni utumishi na majitoleo na sio ubosi. Hivyo kama kiongozi ilimbidi awe wa kwanza kuwaonesha wenzake njia, afuate ile njia ya Bwana wake. Hii haikuwa adhabu bali ulikuwa ni upendo mkubwa kwa Petro na kwa njia ya uhodari wake, aliweza kuwatia moyo mitume wengine. Somo hili ndugu zangu litupatie matumaini hasa kwa baadhi yetu tulio viongozi, wazazi au wenye wadogo wanaotegemea uongozi toka kwao. Lazima tuwe mstari wa mbele katika kuliongoza hili kundi na tusiwe wa kukata tamaa kwani tutaliangusha kundi lote. Mara nyingi mtoto wa kwanza ndiye anayepataga shida kuliko wenzake. Mtoto huyu anapofaulu kuwa hodari na kuwaongoza wenzake, mwishowe huiletea familia maendeleo makubwa.
Hivyo basi kila mmoja wetu anaalikwa kuwa Petro mahali pale anapoishi. Tuoneshe mfano, tuwe sababu za kuwatia moyo wenzetu ili wasirudi nyuma au kukata tamaa.

Paulo katika somo la kwanza anatupatia mfano wa askari bora aliyepambana hadi mwisho bila kuogopa ugumu wowote. Huku kupambana kwake kuliwasaidia sana wale wakristo wa makanisa aliyoanzisha waweze kusonga mbele. Wao walipomuona Paulo akivumilia yote hayo, nao walikuwa na moyo wa kupambana hivi hivi, nao hawakuogopa kifungo wakawa mstari wa mbele kuihubiri injili. Nasi tuepukane na ile hali ya kuwa watu wakata tamaa; mkata tamaa huwarudisha wenzake nyuma na kuifanya jamii yote ianguke. Tuepukane na hali hii. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni