Jumatano, Mei 27, 2020
Jumatano, Mei 27, 2020,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 20 : 28-38
Yn. 17:11-19
sala ya kuwaombea wanafunzi
Ndugu wapendwa, karibuni tena kwa tafakari ya neno la Bwana leo. Bado tupo katika kipindi cha Novena tukimuomba Roho Mtakatifu na tunazidi kumshukuru kwa neema zake kwani kwa hakika hata mimi (labda hata na wewe) umekwisha kuanza kuona matunda ya hizi neema zipatikanazo kwa kusali novena kipindi hiki. Tuzidi kumwomba Mungu azidi kutubariki.
Katika neno la Bwana leo, tukianza na injili yetu, tunakutana na Yesu akiendelea kutoa sala ya kuwaombea wanafunzi wake hali akijiandaa kuagana nao. Anaomba Mungu awalinde ili wabakie katika umoja. Yesu mwenyewe anasema kwamba yeye alipokuwa pamoja nao aliwalinda na kuwaongoza vyema. Alihakikisha kwamba hawadumbukii shimoni na alijitahidi kweli lakini mmoja wao alikataa huu mwongozo wa Yesu na kuona kwamba hauhitaji na hivyo akachagua njia yake mwenyewe na huko alikamatwa na shetani aliyempotosha. Huyu ndiye Yuda Iscariot. Wale waliofuata mwongozo wake angalau kidogo tu Yesu anaomba kwamba Mungu awalinde na yule mwovu na kuwatakasa katika kweli.
Katika injili hii Yesu anakuwa mfano kwetu kwamba kila aliyekabidhiwa na kundi, lazima ajiandae kujitoa sadakaa kwa ajili yake na kuliongoza katika mwongozo sahihi. Sio kuliacha ili liangamie. Hili linakuwa somo hasa kwa baadhi yetu ambao ni viongozi; uongozi ni kujitoa sadaka, ni utayari wa kuhakikisha kwamba wenzangu wanakula kwanza, wanapata mahitaji yao kwanza halafu mimi baadaye. Furaha yangu ni pale wenzangu wanaposhiba kwanza na sio mimi nishibe. Kama mambo ndio yako hivi, basi wengi wetu hapa kwa kweli tunahitaji tumwombe Mungu msamaha kwanza. Hii ni kwa sababu wengi tunachukuliaga nafasi za cheo kama sehemu za sisi kufaidi juu ya vichwa vya wengine. Hapa ni kutenda kinyume cha alivyotenda Bwana wetu Yesu Kristo ambaye tunasema tunamwamini. Somo hili tena linatoa onyo kali kwa wale akina baadhi yetu ambao tunatabia za kufanya mahusiano ya kimapenzi hasa nje ya ndoa zetu. Unapofanya mapenzi na mtu, jua kwamba kuna uwezekano wa kiumbe kuzaliwa. Wasichana wanaofanya mapenzi na wanaume wengi wameishia kuzaa watoto ambao hata baba zao hawajulikani. Watoto wa namna hii huishia kutekelekezwa. Najua ni kweli wengi wetu tunaudhaifu wa kutenda dhambi hizi za kufanya mapenzi nje ya ndoa. Hii ni dhambi. Lakini dhambi inaongezeka Zaidi pale ninapofanya mapenzi bila kutambua kwamba kile kitendo changu chaweza kuzalisha tunda gani. Na je, huwa ninakuwa tayari kufuatilia kilichotokea baada ya dhambi yangu ili niwe tayari kumtunza huyo mtoto. Jamani, kama umetenda dhambi ya uzinzi/uasherati, basi fuatilia pia na yule mtoto atakayezaliwa ili umtunze ili dhambi zisiongezeke zaidi kuliko kuacha yule mtoto azaliwe kama asiyekuwa na Baba (kwa sababu labda mama atakuwa ametembea na wengi) na hivyo yule mtoto kuteseka zaidi. Na kwa wale wazazi tunaowatelekezaga watoto tuache tabia hizi. Tuige mfano wa Yesu.
Katika somo la kwanza Paulo naye anatoa hotuba yake ya mwisho ambaye anajionyesha pia kama askari mwaminifu aliyepigana kwa ajili ya Kristo huko Efeso. Hivyo anaondoka akijisifia historia nzuri ya imani na mfano wa maisha. Hivyo anawaambia wale wa Efeso kwamba ni kazi kwao. Kila linalohitajika alikwisha waonesha mfano. Hivyo wanatakiwa watende kwa kadiri walichoona toka kwake na sio toka kwa waalimu wa uongo ambao Paulo anasema kwamba wangeivamia Efeso. Hili ni somo kubwa kwetu. Sisi tulipokeaga mfano mzuri toka kwa wazazi, waalimu wetu na wazee wetu. Tujiulize, je hivi sasa ninatenda kuendana na kile alichonifundisha mama yangu? Hivi kweli haya maisha ninayoishi sasa niliyajifunza au ninamuiga nani. Je, ukataji wangu wa nywele unafanana na ule wa baba au mama yangu? Maneno yangu, uvaaji wangu unafanana na ule wa mwalimu wangu? Hivi vimini ninaviiga kwa mama yangu? Jiulize. Mara nyingi tunashindwa kwa sababu huwa hatuwaigi wale mifano yetu ya kiimani. Tunaishia kuiga wanamuziki, wachezaji mpira, kila kitu tunaiga kwao. Ukataji wa nywele wa wachezaji kama akina Balotel, jinsi wanavyochukuaga wasichana mbalimbali, namna wanavyovaa, jinsi wanavyovaaga vimini, jinsi wanavyofuga nywele, wanavyoongea, yote hayo. Hata akifukuza mke na wewe unafukuza. Tambua tunu njema za imani kutoka kwa wazee wako walio kurithisha imani. Tutafakari haya
Maoni
Ingia utoe maoni