Jumanne, Mei 26, 2020
Jumanne, Mei 26, 2020,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 20: 17-27;
Zab 68: 10-11, 20-21(K. 33);
Yn 17: 1-11.
UTUME WA KUTIMIZA!
Ndugu zangu wapendwa, tuko katika kipindi kitakatifu cha Novena ya Roho Mtakatifu. Ni kipindi ambacho tunamuomba Roho Mtakatifu apate kutushukia na mapaji yake kama alivyofanya hapo mwanzo. Na kweli Roho huyu anahitajika ili aweze kuyapatia maji maisha yetu pale yalipoanza kuonyesha mnyauko. Pamoja na nia zetu nyingine, hii ibakie kuwa nia yetu ndugu zangu.
Tukiingia katika tafakari ya neno la Bwana leo tunaanza na injilii yetu. Hapa tunakutana na Yesu akiendelea kuwaombea wanafunzi wake kwa ile sala yake ya kikuhani. Katika sala hii, Yesu anashuhudia waziwazi kwamba yeye ametimiza wajibu wake kisawasawa na kwa utii mkubwa kama alivyotumwa na Baba. Halafu baada ya kutimiza hiyo kazi, Yesu anamuomba Baba kwamba asisahau kumtukuza-asimsahau katika utukufu wake. Hili ni ombi la ajabu. Yesu alijua kwamba ametenda mambo yote kama inavyotakiwa lakini hadai utukufu kwa nguvu. Tazama anaomba Baba asimuache-nadhani ni wachache kati yetu wangeweza kufanya ombi kama hili baada ya kufanya kazi kubwa kama Yesu. Lakini Yesu anaomba. Maneno haya yatutie moyo hasa kwa wale tunaoonaga utii kama utumwa. Yatutie moyo na wale ambao tunafanya kazi na mabosi wasiohangaika hata kututambua. Yawatie moyo na wale wanaoishi kati ya watu wenye wivu na wasiotaka maendeleo yao.
Yesu pia anawaombea wanafunzi wake wapate kuwa na umoja na watii yale mafundisho ya kweli. Katika kuwa na umoja, Yesu anautolea umoja wake na Baba kama mfano tunaopaswa kuuishi. Jinsi yeye alivyommoja na Baba, wanafunzi nao waige hili. Hapa kwenye umoja bado tunahitaji kufanya bidii kwani bado hatujafaulu. Umoja wetu unapaswa kuuiga ule wa Baba na Mwana-je, mimi huwa nauiga umoja huu?-kweli?-hapa kwa kweli kila mmoja wetu aanguke tu miguuni kwa Baba na kumwomba msamaha. Umoja wangu na mwenzangu au hata na mke wangu au hata katika utume bado haujafikia hapa. Tuwe wapole; tumwombe tu Mungu msamaha kwa hili.
Katika somo la kwanza, tunakutana na Paulo akitoa hotuba yake ya mwisho huko Efeso. Hotuba hii ni miongoni mwa hotuba za mwisho kabisa na kwa kiasi kikubwa ilifunga utume wake kwa watu wa mataifa ingawa huu haukuwa mwisho wake wa utume kwani baada ya hapa alikwenda Yerusalem na kukamatwa na kuwekwa kizuizini Roma na baadaye kuachiliwa lakini baada ya muda mfupi alikufa kifo shahidi. Katika hotuba hii, Paulo anamuiga Yesu kama tulivyoona katika injili ya leo. Yeye anasema kwamba amejitolea kufanya kazi yake kiaminifu, anakiri kuifanya kiaminifu kweli, anasema kwamba hakumkwaza yoyote na hakuiba au kula cha mtu bure. Anawasihi wale wazee waendeleze ile kazi ya Bwana na anaona uchungu kwani kutakuja waalimu wengi wa uongo lakini anawasihi wamtegemee Mungu. Mwenyewe anahisi kwamba mwisho wake wa utume unafikia ukingoni na kweli anawaambia kwamba hatarudi tena Efeso na hili kweli lilitokea kwani alienda Roma na kifo dini kilimkuta.
Hotuba ya mtume Paulo ni hotuba iliyotolewa na shujaa, askari aliyekuwa mbele kwenye mstari wa mapambano. Hotuba hii inakuwa kama tarumbeta yake ya ushindi kwamba ama kweli nimepigana na nimewaletea ushindi-nilipigana na waaalimu wa uongo, nikapigana na ushirikina, na Wayahudi na maovu na kuwaachia Imani. Mimi mwenyewe nilikuwa mstari wa mbele. Hivyo anaasa waendeleze hili na anatoa hotuba hii kwa ujasiri.
Hotuba hii ndugu zangu itutie moyo. Nasi ifikie mahali tutoe hotuba kama hii. Sio rahisi kuweza kuitoa hotuba kama hii yenye kutafakarisha ushujaa kama huu wa Paulo-shujaa wa matendo mema na imani. Ifikie mahali nawe ndugu yangu katika maisha yako-hata kama ni wakati wa kufa au wakati wa kuhama mahali au labda unafanya jubilei ya miaka 25 ya ndoa au ya utawa utoe maneno kama haya. Kweli ni ya kishujaa. Tuombe ili nasi siku moja tutoe "speech" kama hii maishani mwetu-hasa wakati wa kifo chetu
Maoni
Ingia utoe maoni