Jumapili, Mei 24, 2020
Jumapili, Mei 24, 2020.
SHEREHE YA KUPAA BWANA WETU YESU KRISTO MBINGUNI
Mdo 1:1-11
Zab 47: 1-2, 5-6, 7-8, (K)
Ef 1:17-23
Mt 28:16-20
WAHUJAJI WA KUELEKEA MBINGUNI!
Mdo 1:1-11
Zab 47: 1-2, 5-6, 7-8, (K)
Ef 1:17-23
Mt 28:16-20
WAHUJAJI WA KUELEKEA MBINGUNI!
Ndugu zangu wapendwa, leo tunaadhimisha sherehe ya kupaa kwa Bwana mbinguni. Fundisho juu ya kupaa ni fundisho la kidogma na limewekwa katika kanuni ya imani ya kanisa Katoliki kama fundisho linalotakiwa kusadikiwa na kuheshimiwa ndani ya kanisa zima. Hii ni sherehe ambayo kwetu inafufua matumaini. Kristo anapopaa, anapaa kama shujaa, yeye mwenyewe anazo hizo nguvu za kupaa pamoja naye, hahitaji kusaidiwa, anajipeleka mbinguni mwenyewe. Ndugu zangu, tulikuwa tunasikia kila siku katika injili Yesu akisema kwamba anaondoka kwenda kwa Baba. Sasa ile siku imetimia na kabla ya kuondoka anatuachia utume wa kufanya na anatuahidia Roho Mtakatifu atakayesafiri pamoja nasi katika kuukamilisha utume huo na pia anaahidi kurudi tena-na hapa atataka matunda ya ule utume aliotuachia na hapo basi atatoa hukumu. Hili ndilo la pekee katika sherehe hii ndugu zangu.
Labda tuziangalie nyimbo zetu kidogo: wimbo wa mwanzo unatoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume: enyi watu wa Galilaya mbona mmesimama mkitazama mbinguni. Haya ni maneno yaliyosemwa na malaika kwa wale wanafunzi waliokuwa wanabakia kujiuliza ati huyo Yesu amepaa paa je, anarudi, itakuwaje, sasa malaika waliwahakikishia kwamba Yesu amepaa na hakika atarudi lakini hakusema lini. Suali hili liliwachanganya wale Wakristo wa mwanzo na kuanza kusubiria aje ili awapeleke mbinguni. Walikuwa hawafanyi hata kazi. Hivyo ujumbe huu wa malaika unawaasa na kuwaambia kwamba waache kupoteza muda: waende watimize ule utume aliowaambia; wakafanye utume waache kukaa tu, acheni uvivu; nendeni mkafanye kazi.
Wimbo wa katikati ni zaburi iliyoimbwa na mtu mmoja aliyeitwa Asaph aliyekuwa mwangalizi wa muziki mtakatifu wa hekalu kipindi cha ufalme wa Daudi. Zaburi hii inatukuza ukuu wa Mungu na ni wimbo uliotumika hasa wakati ambapo labda Waisraeli walikuwa wameshinda vita hivyo walikuwa wakimtukuza Mungu kwamba kweli ameonesha nguvu zake mbele ya adui. Kwetu zaburi hii tunaitumia kusherekea kupaa kwa Bwana wetu kwa kuonesha kwamba hakika kupaa huku ni ushindi kwa Yesu, ni Yesu ameshinda vita tena vikali kabisa. Hivyo, tuna kila sababu ya kushangilia ushindi wa Yesu. Yesu kwa kweli leo anakwenda mbinguni kama shujaa, kama jemedari wa vita, anakwenda akiwa ameshinda vita vikali kabisa. Anakwenda kupewa mamlaka yake.
Tukianza kwa kuliangalia somo la kwanza, somo hili linaelezea tukio hili la kupaa na jinsi alivyopaa na ujumbe aliouacha kabla ya kupaa. Somo hili linatuambia kwamba huyu mwandishi wake aliwahi kuandika kitabu kingine ambapo alielezea simulizi ya maisha ya Yesu. Na anasema kwamba katika kitabu hiki kipya sasa ambapo hili somo jingine linatoka, basi yeye ataelezea kilichofanywa na wale mitume, jinsi kanisa lilivyoenea baada ya kupaa kwa Yesu. Na hapa twaweza kusema kwamba ataonesha jinsi nguvu ya Roho Mtakatifu itakavyokuwa inafanya kazi ndani ya kanisa; Roho Mtakatifu aliyeahidiwa katika ile injili.
Hivyo basi katika somo hili, anaeleza wanafunzi wakiwa wamekusanyika na Yesu katika faraja baada ya ufufuko wake; na hapa sasa inaonekana kwamba walikuwa sasa ndio wanaanza kumwamini amini sasa na kuona kweli amefufuka. Mwanzoni kama tulivyokuwa tunaona walikuwa wanaona shaka. Lakini sasa inaonekana kwamba ilikuwa amekwishawatokea kwa muda mwingi sasaa na hivyo wamekwisha mzoea na kumwamini. Hivyo sasa wanaanza kwa kueleza ya moyoni: wanamuuliza, je, leo ndio siku ya kuiletea Israeli ukombozi: yaani walikuwa wanafikiri kwamba Yesu ni jemadari wa kidunia, sasa amefufuka sasa wanamuuliza, je, ndio siku ya kutuletea ukombozi wakidhania kwamba ndio wakati wa kuwaokoa katika mikono ya Kirumi waliokuwa wanatawala na sisi tupate vimadaraka huko.
Yesu japokuwa anapinga mtazamo wao huo, yeye hawajibu moja kwa moja lakini jibu lake linaeleweka; kwamba utawale wake sio wa kibinadamu, wa kutawala kama wafalme wa dunia. Utawala wake ni wa kutangaza habari njema ya upendo ulimwenguni na kila mahali wasikie utawala wake. Hivyo, anawaambia kwamba iliyopo wajihusishe na utume wake na sio kudai madaraka. Anawaahidia kwamba kutakuwako na nguvu ya Roho Mtakatifu itakayowajia na kuwasaidia katika utume huu hadi wafikie miisho ya dunia. Wakiwa wanamtazama, alinyakuliwa na kupaa mbinguni.
Injili yetu pia inaelezea tena tukio hili la kupaa. Inasema pia kwamba wakati huu Yesu alikuwa amekusanyika pamoja na wafuasi wake. kabla ya kupaa anawapatia utume wa kuitangaza habari njema na kubatiza watu na aaminiye aokoke. Pia anawaahidia kwamba atakuwa pamoja nao na atawapatia miujiza mbalimbali itakayo wathibitishia kile wanachokifanya ili watu waamini. Anaahidi pia kuwalinda na kuwaepusha na vyakula vyote vya sumu au wanyama wabaya kama nyoka. Injili inatuambia kwamba wanafunzi nao walishika njia wakaanza kulitii neno lake hili. Hawakuhangaika kutafuta utawala wa kidunia. Hivi ndivyo masomo yetu yanavyoelezea juu ya kupaa kwa Bwana leo.
Ndugu zangu, tukiyachunguza masomo haya, twajifunza yafuatayo: kwanza, Yesu anapaa mbinguni kama shujaa-shujaa aliyemaliza kazi yake. Amekuja duniani, amekamilisha utume wake wa kumpatanisha mwanadamu na Mungu, kafuta lile kosa la wazazi wetu na sasa anapaa kwenda mbinguni kwa Baba baada ya kumaliza kazi yake. Hivyo, anakwenda mbinguni akiwa ameshinda: kama jemedari aliyeshinda vita sasa na huko atashangiliwa vya kutosha na kupewa tuzo, na mbingu itashangilia na malaika watashangilia kama tulivyosikia katika wimbo wa katikati. Aliteseka sana lakini sasa anarudi kama shujaa wa vita.
Halafu, anapopaa, anapaa kwa nguvu zake mwenyewe. Yeye hapalizwi kama Bikira Maria au hachukuliwi kwa nguvu za upepo wa kisulisuli kama Elia alivyopelekwa mbinguni kwa nguvu za upepo huu au hana mabawa kama malaika. Kitendo cha malaika kuwa na mabawa ni kiashirio kwamba hata hizo nguvu zao na kushuka na kurudi toka mbinguni wamezipewa. Lakini Yesu anapaa mwenyewe kuonyesha kwamba ananguvu nyingi ajabu za kujipeleka mbinguni. Sisi hatuna nguvu kama hizo. Halafu, kupaa kwake kunaonesha kwamba yeye ana nguvu juu ya viumbe vyote hata nguvu ya dunia ya kuvuta viumbe chini. Ili ndege aweze hata kupaa juu, lazima awe na mabawa. Lakini Yesu hakuwa nayo kuonesha kwamba ile (force of gravity) yenyewe iko chini yake. Ikikutana na yeye inashindwa. Hii ni ishara ya nguvu za Yesu.
Halafu anapopaa mbinguni, anakwenda mbinguni na kitu ambacho hakuwa nacho hapo mwanzoni; Anarudi akiwa kabeba uanadamu. Mwanzoni hakuwa nao. Sasa ana asili mbili Umungu na ubinadamu, weli kaenda mbinguni kama mwakilishi, na mwombezi wetu. Kaenda akiwa na ubinadamu. Hii yamaanisha kwamba Yesu kweli alikuja kuupatia uanadamu uzima wa milele na hata anapopaa kwenda mbinguni, kweli huko anakwenda kutuandalia makao kwani kabeba uanadamu wetu. Amekwisha utakatifuza uanadamu wetu sasa. HIli ni jambo la maana sana kwetu. Yamaanisha kwamba uanadamu sasa umepatiwa maana. Sasa anakwenda kutufungulia maisha ya umilele na hivyo yafaa tufurahi.
Hivyo, sherehe hii ni sherehe inayotuongezea Imani Zaidi. Inabidi tuione kama sherehe iliyotuletea ukombozi mkubwa sana. Sherehe ambayo milango ya mbinguni imefunguliwa kwa ajili yetu.
Lakini hii ni sherehe inayotuambia tufanye kitu. Tumesikia katika somo la kwanza malaika wakiwaambia wale watu wa Galilaya wasisimame wakishangaa na kutazama mbinguni, wajue kwamba atakuja tena na huko atataka malipo, ya ule utume aliowaachia kufanya. Hivyo, wasibakie ati bila kufanya chochotte wakimlilia Yesu aje kwao au vipi. Wafanye alichowaambia. Unakumbuka wale wakirsto wa mwanzo walikuwa baadhi yao wanakaa tu, wakisema Kristo atakuja karibuni. Hivyo hawakulima au kufanya kazi. Ujumbe wa leo uliwataka wakakazane juu ya utume, watangaze neno la Mungu na Yesu atakuja na atakapokuja anataka injili ikutwe imekwisha tangazwa kila mahali na si awakute wakiwa bado wamejifungia ndani.
Kwanza mitume leo tumesikia wakiulizia juu ya Israeli kurudishiwa ufalme. Wanauliza hivi kwa sababu hadi sasa akili zao zilikuwa bado hazijaelewa nini walichokuwa wanapaswa kufanya. Walikuwa bado hawajauelewa utume wao. Lakini cha ajabu kitatokea; baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, watabadilika kabisa, hawatajiuliza tena juu ya ati Israeli kurudishiwa ufalme na Warumi; hakuna kabisa. Wataanza kuhubiri mbele kwa mbele. Ina maana gani? Hii yamaanisha kwamba kwa kweli bila Roho Mtakatifu, sisi hatuna kitu chochote. Nakwambia; bila Roho Mtakatifu hata ukiambiwa uone faida ya kanisa, faida ya kusali, faida ya kuja kanisani kila siku, faida ya kujiunga na utawa hutapata. Lakini ukiwa na Roho Mtakatifu ndio kila kitu. Tazama jinsi alivyowabadilisha mitume. Hivyo, na sisi tusiache kuhakikisha kwamba kabla ya kufanya chochote, Roho Mtakatifu lazima tumwombe; hata kama nipo utawani lazima nimwombe Roho, Roho Mtakatifu ndiye mtoaji wa maana, ndiye atoae nguvu yote hivyo hakika tusije tukamuacha.
Yesu kapaa lakini kaacha kazi ya sisi tufanya-ambayo ni kuhakikisha kwamba injili yake inahubiriwa duniani kote na atakaye amini hakika ataokoka. Sisi ni lazima tuchunge sana. Sisi kama wakristo jukumu letu ni kuhakikisha kwamba injili inahubiriwa kila mahali. Watu wote waisikie. Ni jukumu langu kuhakikisha nasaidia hili. Lazima nijiulize, je, mimi hadi sasa nimeshasaidia vipi injili ihubiriwe? Nimeshafanya nini ambacho kimeisaidia injili? Nimejitahidi hata kumsaidia mtoto wangu aende hata utawani ili akaihubiri injili? Ninajitahidigi kutoa michango ya ujenzi wa kanisa-nikipita mahali na kukuta labda kuna kanisa linajengwa-huwa hata nachangiaga mchango? Labda wewe umekwenda kusali parokia fulani ukakuta wanajenga kanisa-wewe unafanyaga je, huwa unachangia hata kidogo? Lazima ujiulize, ujikosoe, uone kweli kwamba ama kweli unachangia katika kazi ya uenezaji injili.
Lakini tutambue kwamba ujumbe wetu uweze kuwa na kitu kama hiki, lazima tuwe kweli na maadili, wakweli na watu wanaosali ili kweli ujumbe wetu uwafikie wengi kwa sababu kuhubiri nako kwahitaji namna yake jamani. Si kila kitu unajihubiria au kuongea ongea tu. Kuna namna yake.
Pili, Yesu amepaa mbinguni peke yake, yeye alikuwa na nguvu za kwenda huko mbinguni mwenyewe. Hakuhitaji mabawa kama malaika au upepo wa kisulisuli kama Elia. Lakini sisi hatuna nguvu za kwenda huko. Lazima upelekwe na hili ndilo sababu ya wewe kuja kanisani, kuja kuomba, kumlilia Yesu atupeleke huko. Hivyo basi usichoke kumlilia yesu. Leo kaonyesha kwamba yeye ana nguvu za kwenda huko. Hivyo, basi sisi tumlilie tumwambie tupeleke Baba huko ulikoelekea leo. Mwombe, mwambie ee Baba tupeleke huko naye atakuja tu.
Yesu anarudi mbinguni kama shujaa. Kafanya kazi yake aliyotumwa; katetea mafundisho ya kweli, Imani ameilinda. Watakatifu kama akina Paulo walifanya hivihivi pia. Walikufa kishujaa, walirudi wakiwa kama makomandoo wa kivita walipokufa. Kweli walikuwa wamemaliza kazi waliyokuwa wamekabidhiwa. Na sisi ndugu zangu tuwe na tamanio kama hili. Lazima nasi tufikiapo mwisho wetu, turudi kishujaa, tukiwa tumeutetea ukweli, usirudi na deni la mtu, na watoto wanaokulilia, na pesa ukizoiba, au na aibu usoni mwako; rudi kama shujaa kweli ukiwa hudaiwi au kulaumiwa na mtu. Hivyo, tujiandae vyema, tutumie sakrament, tushike wajibu wetu, tupokelewe na Mungu kama mashujaa.
Yesu kaenda mbinguni kama mwombezi wetu kwa sababu kapaa hali pia akiwa amebeba ubinadamu na hivyo yeye ni mwombezi. Yeye ni mwakilishi wetu, ni furaha ilioje?
Yesu anapokwenda, wale mitume wanabakia katika sala hadi Roho Mtakatifu atakapokuja. Nami nakueleza ndugu yangu, hakuna kitu kizuri, hakuna zawadi tuwezayo kumpatia Kristo kama kubakia pamoja katika sala. Nikuambie-kuweza kusali kwa pamoja kila siku, kila mwaka, nakwambia ni kwa neema ya Mungu. Si kitu kirahisi ndugu yangu. Kusali pamoja< mmh! Kwanza ni kati ya zawadi kubwa tunaweza kumpa Bwana wetu na shetani kwa kweli anaiogopa sana. Hivyo, siku zote tubakie katika sala hasa ya pamoja katika hii Novena tuianzayo. Sala ya Pamoja siomchezo
Maoni
Ingia utoe maoni