Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Mei 21, 2020

Alhamisi, Mei 21, 2020.
Juma la 6 la Pasaka


Mdo 18: 1-8;
Zab 98: 1-4;
Yn 16: 16-20

FURAHI KATIKA BWANA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana Yesu anazidi kusisitizia juu ya kwenda kwa Baba. Leo katika injili anawaambia wanafunzi wake ya kwamba bado kitambo kidogo hawatamuona tena kwani anakwenda kwa Baba. Lakini atakapokwenda kwa Baba atarudi tena hatatuacha yatima. Ama kweli Yesu anakwenda kwa Baba kama shujaa, ametimiza ile kazi aliyotumwa kufanya-ya kumpatanisha mwanadamu na Baba na anarudi mbinguni akiwa amebeba kitu kipya: anarudi akiwa amebeba pia hali ya uanadamu-hali ambayo hakuwa nayo hapo mwanzo na anaingia akiwa ameongeza mwili wa Kibinadamu katika Umungu wake wa asili. Kwa tendo hili, inamaanisha kwamba ama kweli mwanadamu amepatanishwa na Baba, amefanikiwa kuirudisha ile hadhi ya mwanadamu aliyopoteza mwanadamu mwenyewe, ameuuleta uanadamu karibu zaidi na Mungu. Hivyo, akiwa huko, yeye atakuwa mwakilishi bora na mwombezi bora wa mwanadamu. Hii ndiyo habari njema ambayo injili ya leo inatutangazia.

Katika somo la kwanza, tunamkuta Paulo akiendelea kukazana na utume wake huko katika mji wa Korintho. Japokuwa anakataliwa na watu, bado anaendelea kuuhubiri ujumbe wa Kristo kwa watu wa mataifa; Wayahudi wanapokataa, anakwenda kwa watu wengine, akijua kwamba wote hawawezi kuwakakataa kumsikiliza. Hivyo hakati tamaa au kulala. Hawa wakimkatalia, anakwenda kwa wengine. Nasi tumwige mtakatifu Paulo. Tukishindwa hapa, tujaribu pengine. Hatuwezi kushindwa kila mahali. Kuna mahali tutakubalika. Hata kama ni kwenye masomo, ukishidwa somo hili au upande huu, jaribu mwingine, hata kama ni kwenye kusuluhisha migogoro-njia hii ikishindwa jaribu nyingine, hata kama ni kwenye kusali-jaribu mbinu mbalimbali-ukishindwa hii, jaribu nyingine, usitumie namna moja tu. Hata kama ni biashara jaribu njia mbalimbali. Ukishindwa hii jaribu nyingine, usikate tamaa. Mungu atakufungulia tu.

Maoni


Ingia utoe maoni