Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Mei 20, 2020

Jumatano, Mei 20, 2020.
Juma la 6 la Pasaka

Mdo 17: 15, 22-18:1;
Zab 148: 1-2,11-14;
Yn 16:12-15.

MUNGU ASIYE JULIKANA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana hasa katika injili yetu bado linazidi kutuandaa kwa ajili ya kupaa kwake Bwana. Kupaa huku kunaambatana na ujio wa Roho Mtakatifu atakayetumwa kwao. Leo Yesu anatuambia kwamba huyu Roho atatuongoza tuufikie ukweli. Huyu Roho atakuwa na lengo la kumshuhudia Yesu tu, hili ndilo lengo na tamanio lake. Hivyo, atatusaidia ulimwengu kuutambua ukweli kwani Roho huyu ataushuhudia ukweli tu.

Ndugu zangu, kwa nini Roho awe na lengo la kuushuhudia ukweli tu? Hii ni kwa sababu kwa kweli ndani ya hii dunia upotofu ni mwingi na watu ni wajanja. Nafikiri mnatambua: kwamba watu wengi wanajitafutia umaarufu na mali. Hivyo, wako tayari kutumia njia yoyote ile. Mmeshasikia wengine wakijiita Yesu, wengine wakisema wametokewa na Bikira Maria, wengine wakijiita kwamba ni nabii kama akina Elia, wengine wakijiita Mungu-na kudai kwamba ndio walioumba mbingu na nchi. Hii ni kweli na imetokea nchi jirani tu. Babu mmoja alijiita Mungu na akapata wafuasi vilelele. Ukweli ni kwamba uwezekano wa kuwapotosha watu hapa ulimwenguni ni mkubwa mno. Ukizungumzia juu ya habari za kifo au juu ya habari za kuponyesha magonjwa kama ukimwi na kansa au habari za kufufua wafu-nakwambia unapata wafuasi na tumeona kila kukicha watu wakipata wafuasi. Hii ni kwa sababu maswala haya yahusuyo kifo na nyakati za mwisho huwaogopesha watu sana na hivyo ni rahisi kwa watu kuwapotosha wengine.

Kanisa lipo tayari nalo kila mara limekuwa likikumbwa na watu kama hawa; baadhi hata ya viongozi wao hugeukia uzushi na mafundisho ya uongo na kuishia kulimega. Lakini shukrani kwa uwepo wa Roho Mtakatifu katika Kanisa. Makundi haya hutokea lakini kwa sababu ya uwepo wa Roho Mtakatifu anayeliongoza kanisa katika ukweli-utashangaa kuona kwamba haya makundi yanaibuka na kuishia na wale waliowafuata wanabakia katika aibu kubwa na kurudi. Huyu ni Roho Mtakatifu anayewaongoza watu katika kanisa, anayechuja kila aina ya Roho chafu. Hivyo, tumshukru Roho Mtakatifu anayeliongoza kanisa. Kwa njia yake wale wanaojitafutiaga umaarufu au kujivuna na kusema ati kanisa haliwezi kusimama bila wao huishia kuabika tu. Sisi tuwe wanyenyekevu; tusije tukajivuna na kufikiri kwamba ati kanisa liko mifukoni mwetu-nakwambia unajikuta unaachwa kama gogo lililoteremshwa na maji na kanisa kusonga mbele. Somo hili pia linatoa onyo kali kwa wale wanaojivunaga na kusema ati wameoteshwa, ati wamenena na malaika, ati wameona Roho-jueni kwamba japokuwa mmeona Roho zenu hizo-lazima mbakie katika utii wa kanisa. La sivyo mtajikuta mkiachwa kama gogo lililosombwa na maji. Tuwe wanyenyekevu.

Katika somo la kwanza, tunamkuta Roho Mtakatifu akiendelea kufanya kazi yake ndani ya kanisa. Yeye anaiwezesha injili kuhubiriwa na pia anampatia mbinu Paulo za kuwahubiria watu wa Atheni (Wayunani). Mji huu ulijawa na wanafilosophia wengi sana kwa kipindi hicho na bila ya kutumia mfumo bora wa kuhubiri, hakika asingefanikiwa. Alifanikiwa kwa sababu Roho wa Bwana alimfundisha mfumo wa kutumia. Nasi tuzidi kuiona na kuishuhudia nguvu ya Roho Mtakatifu maishani mwetu na tumwombe ili nasi atupatie ufasaha wa kuongea na kuhusiana na wenzetu ndani ya jumuiya hasa wale wa imani na tamaduni tofauti-lengo likiwa ni kukuza umoja na uelewano hapa duniani.Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni