Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Mei 19, 2020

Jumanne, Tarehe 19, 2020,
Juma la 6 la Pasaka

Mdo 16: 22-34;
Zab 138: 1-3,7-8 (K. 7);
Yn 16:5-11.

MAISHA NDANI YA ROHO MTAKATIFU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Ndugu wapendwa, tafakari ya neno la Mungu hasa katika injili bado inazidi kutuandaa kwa kipindi cha kupaa Bwana. Katika injili ya leo, tunaambiwa Yesu anatuambia kwamba kupaa kwake sio kwa kutuacha yatima. Tafakari ya jana nilisisitiza kwamba wakati Yesu akiwapo ulimwenguni, haikusikika popote kwamba wanafunzi wamefungwa gerezani au kupigwa kwa sababu Yesu alikuwako na alikuwa tayari kutoa majibu kwa yeyote aliyekuwa anapambana nao. Kwa kupaa kwake, haamaanishi kwamba ndio hawatapata mtetezi. Bado wataendelea kumpata mtetezi na huyu mtetezi ndiye Roho Mtakatifu ambaye watahitaji kushirikiana naye wakati tatizo lolote litakalotokea. Kweli wanafunzi waliweza kushirikiana na huyu Roho Mtakatifu na waliweza kufaulu katika mengi.-waliweza kuanzisha makanisa mahali pengi na kupambana na uzushi mbalimbali. Na wale waliokuja baada ya mitume, yaani viongozi na waalimu wengi wa kanisa, nao waliweza kushirikiana na Roho Mtakatifu. Chochote walichofanya kilikuwa kwa ajili ya kanisa, walijiepusha kufanya chochote kwa ajili ya faida binafsi au umaarufu. Walimuomba Roho Mtakatifu aliongoze kanisa lake. Na kwa njia hii waliweza kufaulu kupambana na uzushi mbalimbali ndani ya Kanisa na kupambana na makaisari kama akina Nero, Domitian, Kaligula, na Diocletian. Wote hawa walijaribu kuliangamiza kanisa lakini kwa sababu kanisa limejengwa juu Kristo na linaongozwa na Roho Mtakatifu na si juu ya matakwa ya mtu binafsi, basi waliishia kushindwa. Na hii ni kweli-kama kusingekuwa na Roho Mtakatifu-jinsi hawa makaisari walivyokuwa na nguvu, nakwambia kanisa lisingefika popote. Huu ni ujumbe wa matumaini kwetu.

Nasi jamani tuelewe kwamba kanisa si la binadamu, si la Padre, si la katekista. Kanisa ni la Mungu. Lipo ili nilitumikie na japokuwa mchango wangu katika kanisa unahitajika na ni wa muhimu sana, ukweli unabakia palepale kwamba hata nikikataa kulitumikia kanisa, kanisa litabakia pale pale; ni la Mungu. Hivyo, tunapokuwa waamini na viongozi kanisani, tufanye hii kazi kwa unyenyekevu. Lazima nitambue kwamba mchango wangu ni muhimu ndani ya kanisa na kweli kanisa linanihitaji. Lakini nisifikie kiwango cha kujiona kwamba bila mimi kanisa litavunjika-weeee? Nani kakuambia! Wewe jione kama mchezaji katika timu, ambaye unahitaji kucheza kwa umakini katika namba yako ili timu ifanikiwe. Lakini ujue kwamba hata wachezaji muhimu katika timu kuna wakati unafika muda wao unakwisha na wanaondoka. Kunatokea machipukizi tena mengine na timu inazidi kusonga mbele. Wewe jione kama mtumishi asiye na faida aliyefanya kazi yake, basi, atakuja mwingine naye atafanya sehemu yake lakini usikubali kujivuna.

Katika somo la kwanza tunakutana na ujumbe wa Kristo mfufuka ukiendelea kutangazwa kwenye pande mbalimbali. Sasa wapo Philipi na wakiwa huko, kile Yesu alichowatabiria kwamba watakutana na magumu katika utume-watu watawakamata, kuwachapa viboko na kuwafunga gerezani-leo kimetokea kwa hawa watu. Lakini kama alivyosema kwamba atakuwa nao daima akiwatetea kweli ujumbe huu unatimia kwao. Leo basi anatokea malaika wa Mungu anawaokoa na kitendo hiki kinawaogopesha kila mmoja kiasi kwamba hata yule Askari anaomba kubatiza. Kweli Yesu alichoahidi hadanganyi. Tukio hili litutie matumaini na sisi kwamba Yesu atakuwa nasi sikuzote akituokoa. Hivyo, tuzidi kumtumainia kila wakati jamani. Kama aliweza kuwafanyia akina Paulo hivi, tena muujiza mkubwa kama huu, ata mimi atanifanyia na mimi pia. Hatakubali nifungwe katika shida zangu daima, mtumainie atakufungua tu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni