Jumatatu, Mei 18, 2020
Jumatatu, Mei 18, 2020.
Juma la 6 la Pasaka
Mdo 16: 11-15;
Zab 149: 1-6, 9;
Yn 15:26 - 16:4.
ROHO MTAKATIFU: MSAIDIZI
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tupo katika kipindi cha Pasaka na tafakari ya neno la Bwana hasa katika injili yetu inatuandaa kwa ajili ya kupaa kwa Bwana. Leo katika injili Yesu anaanza kwa kuwapatia mitume wake matumaini kwamba kutakuwepo na Roho Mtakatifu atakayewaongoza, atakayewakumbusha kila kitu walichojifunza, na atakaye endelea kumshuhudia Kristo, na atakayeuwezesha ujumbee wake uweze kuenezwa kila mahali. Hivyo, wajiandae kumpokea na kumkaribisha huyo Roho.
Lakini Yesu anawapatia tena tahadhari. Kipindi Yesu akiwa duniani, wanafunzi hawakuteswa au kupigwa viboko au kuitwa mbele ya baraza na kuhojiwa. Hii ni kwa sababu Yesu alikuwepo kila wakati. Mwanafunzi akipatwa na tatizo; Yesu alikuja mara moja na kumtetea, na kutoa majibu. Wanafunzi walipokamatwa na kuulizwa lolote Bwana alikuja na kujibu. Hivyo walikuwa hawajawahi kupata shida ya aina yeyote ile ya kuchapwa kiboko kwani Bwana harusi alikuwa pamoja nao akiwatetea. Lakini leo Yesu anawapatia tahadhari kwamba watachapwa viboko na kufungwa na kuitwa mbele ya baraza na hivyo wajiandae. Yeye hatakuwepo wakati huo; atakayekuwapo ni Roho Mtakatifu. Hivyo, basi wajiadae kumkaribisha Roho Mtakatifu kwani ndiye atakayewasaidia kupambana na hali yeyote ile ngumu. Wakimuacha wajue kwamba wataonewa kweli.
Ndugu zangu, huu utabiri wote wa Yesu ulitimia. Mara baada tu ya kupaa kwake, wanafunzi wake walianza kuhubiri na hivyo walijikuta mikononi mwa viongozi wa kidini wa Kiyahudi. Ni Roho Mtakatifu mwenyewe ndiye aliyeweza kuwasaidia ndugu zangu.
Hii hali waliyokumbana nayo wanafunzi wa Yesu ni hali ambayo hata sisi katika maisha tunakumbana nayo. Kuna wakati ambapo unajikuta kwamba upo mikononi mwa wazazi wako; chochote kikitokea basi wao ndio wameshajibu, hata kama umefanya kosa wao ndio wanaofanya mipango yote. Hiki nakifananisha na kile kipindi cha Yesu na wanafunzi wake wakiwa pamoja duniani. Lakini kipindi kinakujanga unajikuta upo mwenyewe-kipindi cha kuwajibika wewe kama wewe. Uongoze maisha yako, ujipangie mambo, ujue ni maadili gani ufuate au la. Wengi wanapofikia katika hatua hii, mambo huwa magumu na wengi huishia kufanya mambo ya ajabu (hadi dunia inaamua kuwafundisha adabu). Hiki kipindi haimaanishi kwamba unakutaga hamna watu wa kukuongoza; unakuta wapo lakini ni wewe tu ukubali kuwasikiliza na kuwaiga miongozo yao. Ukikataa hali huwa mbaya kwako. Wanaokubali mwongozo yao wanastawi vyema-lakini hakuna atakayekuja kukushikia kiboko. Vile vile kwa mitume; wao kwa kipindi hiki ilikuwa ni juu yao kushirikiana na huyu Roho au la. Hakika walishirikiana naye na kufaidi. Vile vile kwa baadhi yetu. Mifano mizuri ya kuigwa ulimwenguni, watu wema wa kutufundisha maadili na sala wapo, wa kutusaidia wapo-swali ni je, upo tayari? Lazima tuwe tayari kushirikiana nao. Wengi tunapotea, wengi tunaishia kufuata tamaduni za ajabu, wengi tunaishia hata kubadili dini-hasa kina dada ili waolewe-yote haya yanatokea kwa sababu tumekataa kushirikiana au kusikiliza mwongozo wa wale wenye mifano mizuri ndani ya jumuiya zetu.
Somo la kwanza laelezea habari jinsi Paulo anapopeleka habari njema ya Kristo mfufuka hadi huko Philip. Huko hakukuwa na yeyote anayemfahamu. Lakini alijitokeza Mama mmoja aitwaye Lydia aliyewakaribisha nyumbani mwake na kusaidia waeneze injili. Hapa kwa kweli tujifunze juu ya umuhimu wa mwanamke katika kuieneza injili. Kweli akina mama wamechangia mchango mkubwa sana katika ukuaji wa kanisa na hadi sasa wao ndio wanaokuwa wa kwanza kuhudhuria jumuiya, kanisani ndio wapo, kwenye harambee ndio wako. Angalia vikundi vya akina mama kama WAWATA vilivyo na nguvu. Sehemu nyingi unashangaa kusikia kwamba wawata ndio watoaji wa misaada wakuu (kina baba mko wapi? Labda mwaweza kujitetea na kusema kwamba hizo pesa wanazitoaga kwetu). Utashangaa kuona jinsi mwanamke anavyosaidia ukuaji wa kanisa. Kwenye usafi kanisani wapo. Kila mahali wapo. Hivyo basi, naona ni vizuri popote tulipo tujaribu kuwawezesha akina mama waendelee kusaidia zaidi katika kazi ya ukuaji wa injili. Watalifikisha kanisa mbali kwa hakika. Lakini pia wanaume tuamke zaidi, tunajitahidi lakini bado tunahitaji majitoleo zaidi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni