Jumamosi, Mei 16, 2020
Jumamosi, Mei 16, 2020.
Juma la 5 la Pasaka
Mdo 16: 1-10;
Zab 100: 1-3,5 (K. 1);
Yn 15: 18-21.
KUKUTANA NA MATESO
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Kama nilivyokumbushia jana, neno la Bwana, hasa katika somo la injili tunapatiwa habari za sehemu ya wosia wa mwisho alioutoa Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya mateso na kifo chake. Sisi kwa kuwa tunajiandaa kwa sherehe ya kupaa, wosia huu unakuwa ni sehemu yetu ya kutafakari mawazo muhimu anayotuachia Kristo ili tuyaishi kabla ya kwenda kwa Baba. Na endapo tutayaishi, basi yatakuwa ni zawadi, sadaka nzuri yetu kwa Yesu akiwa katika utawala wake. Huu ndio umuhimu wa kuuheshimu wosia huu ndugu zangu. Injili yetu ya leo ni sehemu pia ya wosia huu na leo anawaambia wanafunzi wake kwamba nao pia wategemee kutendewa kile ambacho yeye alifanyiwa. Anawaambia kwamba wasitegemee ati ulimwengu utawapenda. Wasikae siku nzima wakitafuta ulimwengu uwapende. Yesu mwenyewe alikaa akiutendea ulimwengu mwema lakini walio wa ulimwengu hawakumkubali. Hivyo, Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba kwa kuwa wao si wa ulimwengu, hivyo basi wasitegemee kupendwa na ulimwengu. Ndugu zangu, mitume ni watu waliokuwa wamenunuliwa kwa damu ya Yesu na walikuwa tayari kufuata mwongozo wake. Kwa kukubali kumfuata Yesu, moja kwa moja watajikuta wakikosana na ulimwengu kwa sababu watajikuta wakilazimika kuutetea ukweli daima na hili ndilo litakalowakosanisha na ulimwengu. Ukitaka upatane na baadhi ya watu, au kutengeneza urafiki na wengi, lazima uwe mtu wa kungata na kupuliza, lazima uwe mjanja awezaye kusoma mazingira na kubadilika kama kinyonga ili kukabiliana na hatari za mazingira. Mchezo huu tunaweza kuuona vizuri katika siasa. Hata kama umeambiwa umwambie mtu ujumbe huu, ukitaka kutetea maslahi yako, lazima utafute namna itakayokubakiza salama, bila kujionesha ubaya wako tofauti na nabii.
Sasa, ndivyo ulimwengu ulivyo. Wao wanamchukia nabii kwa sababu nabii anapaswa kusema bila kupunguza ukali wowote, atoe Ukweli kamili, ataje kosa lako, na anapaswa kusema hata kama ni hadharani. Hahitaji aje kwako kukuambia hili. Kweli ndugu yangu nakuambia mtu yeyote yule aliyeko hivi, asemaye namna hii, asemaye ukweli bila kuficha-hakika ulimwengu unamchukia-na ndio unasikia kwamba wengi wao wanaanzaga kuwatafutia visa, au kuhatarisha maisha yao na waliojaribu kuongea bila kuficha namna hii wameishia kuchukiwa na kusumangwa na ulimwengu.
Lakini licha ya kusimangwa, maneno yao, damu yao, juhudi zao, ujasiri wao huisaidia sana jamii. Sasa, huu ndio ujumbe Yesu anaoutoa kwa mitume leo na anawaambia kwamba mwanafunzi sio mkubwa kuliko Bwana wake, hivyo wajiandae na wao kukabiliana na pilikapilika kama hizi.
Somo hili ndugu zangu linatuasa juu ya hatari iliyopo mbele ya maisha ya mkristo-hatari ya kubembeleza urafiki kwa kuuficha ukweli. Na hii imeenea sehemu nyingi. Ama kweli ni wachache kati yetu siku hizi waliojasiri wa kuukueleza ukweli. Wengi tunaogopa kupoteza urafiki, kuwaudhi wenzetu, au kuonekana wabaya. Hivyo, tumekuwa tunaacha vitu viharibike ili nisilaumiwe au nisipoteze umaarufu. Tunaogopa kuchukiwa. Lakini nakuambia mambo haya yamewafanya wengi wapoteze haki, maadili yashuke, dhambi kuendelea kushamiri na kuendeleza uadui duniani. Halafu kwa kupindisha mambo, tujue kwamba tunakwaza wenzetu pia. Jamani, anayepindishaga pindishaga mambo haleti faida, kupindisha hakuna baraka. Tuache tabia hizi. Tuishi maisha yetu ya kinabii; yale ya kusema ukweli bila kupindisha. Japokuwa utachukiwa, jua kwamba wengi watafaidi baadaye. Anayepindisha atawaumiza watu tu.
Katika somo la kwanza, tunasikia habari za injili ikiendelea kuhubiriwa na Paulo. Na leo anamchagua msaidizi wake ambaye atakuwa wa karibu sana na fambaye atauacha utume wake mikononi mwake, yaani Timotheo. Huyu atasaidia sana kuhubiri injili na atakuwa anaongozwa sana na Paulo atakuwa anamwandikia sana kumpatia mwongozo namna ya kuishi. Atakuwa anamsisitizia kuishi maisha ya adili, na akazie ukweli kwenye mafundisho yake. Asiishi kwa kumfurahisha mtu bali amfurahishe Mungu. Nasi ndugu tunaalikwa kuwa Timotheo kwa jumuiya zetu. Tuwe kweli manabii. Nabii anahubiri kitu kwasababu ni kweli sio kwasababu ya kufurahisha mtu
Maoni
Ingia utoe maoni